Home Mchanganyiko KAMATI YA UCHUMI, UJENZI NA MAZINGIRA BUSEGA YATEMBELEA VIWANDA VYA KUCHAMBUA PAMBA...

KAMATI YA UCHUMI, UJENZI NA MAZINGIRA BUSEGA YATEMBELEA VIWANDA VYA KUCHAMBUA PAMBA NA UZALISHAJI WA MAFUTA

0

****************************

Na Mariane Mariane Mgombere

Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Busega imetembelea Viwanda vidogo vya Uzalishaji wa mafuta ya kupikia na uchambuaji wa Pamba. Ziara hiyo imefanyika siku ya tarehe 02 Agosti 2021 ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Charles Lukale.

Wajumbe wa kamati hiyo walifika katika kiwanda cha uzalishaji mafuta kijulikanacho kama LAMADI OIL na kujionea njia zinazotumika kuzalisha mafuta ya kupipikia yanayotokana na zao la Pamba. Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Charles Lukale amesema kamati hiyo imetembelea Viwanda hivyo ikiwa ni sehemu ya kujifunza ili kupata ujuzi ambao unaweza kuisaidia Halmashauri kuwekeza katika Viwanda.

Mkurugenzi wa Kiwanda LAMADI OIL, Bw. Makubi Joseph amesema licha ya kiwanda hicho kuzalisha lita takribani 1,890 kwa siku bado kuna uhaba wa upatikanaji wa Pamba ya kutosha ili kufanya uzalishaji kuwa mkubwa zaidi. Aidha, Bw. Joseph amesema uzalishaji mdogo pia unachangiwa kwa kutokuwa na mtaji wa kutosha, kwani imekuwa ni changamoto kubwa wanapoenda kuomba mikopo katika baadhi ya taasisi za fedha.

Kamati hiyo pia imetembelea kiwanda cha kuchambua Pamba na kukamua Mafuta kijulikanacho kama CHESANO COTTON LIMITED na kuridhishwa na hali ya Uzalishaji wake ambapo kwa siku kina uwezo wa kuzalisha Pamba nyuzi zaidi ya tani 26,000. Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bw. Peter Bahinya anasema uzalishaji wa kiwanda unategemea zaidi upatikanaji wa Pamba, lakini ana imani kubwa kwamba msimu wa uzalishaji wa Pamba ujao kutakuwa na upatikanaji mkubwa wa Pamba.

Kwa kiasi kikubwa wajumbe wa kamati hiyo wameridhishwa na Uzalishaji wa Mafuta na uchambuaji wa Pamba, ambao unafanyika Wilayani Busega, kwani kupitia Viwanda hivyo kumekuwa na fursa kwa wananchi wa Busega, lakini imewataka wawekezaji wengine kuja kuwekeza Busega. Aidha, wameitaka Ofisi ya Mkurugrnzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega kufuatilia kwa ukaribu kodi itokanayo kna Viwanda hivyo na vingine ili kuongeza ukusanyaji wa mapato.