1Mtaalam wa Mitambo akitoa maelezo kwa viongozi
mbalimbali waliohudhuria kwenye ya uzinduzi wa Kituo cha kurushia matangazo ya Redio
ya TBC eneo la Kisaki – Morogoro leo Julai, 2021.
Na John Mapepele, WHUSM
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe Innocent Bashungwa amesema
hadi kufikia Mwezi Septemba, mwaka huu usikivu wa Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC) utapanda kuzifikia Wilaya 120 sawa na 76% kutoka Wilaya
103 ambapo ni sawa na 64% za usikivu wa sasa ili kuhahakikisha
wananchi wote wanapata habari kwa uhakika.
Mhe. Bashungwa
ameyasema hayo leo Julai 30, 2021 kwenye uzinduzi wa kituo cha kurushia
matangazo ya redio eneo la Kisaki mkoani Morogoro ambapo amesema katika
Bajeti ya Maendeleo ya Wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021, TBC
inatekeleza miradi ya upanuzi wa usikivu katika Wilaya za Karagwe
(Kagera), Same (Kilimanjaro), Sikonge (Tabora), Kahama (Shinyanga),
Bunda (Mara), Nkasi (Rukwa) na Kasulu (Kigoma)ambapo amefafanua kuwa
kukamilika kwa miradi hii kutawezesha usikivu wa TBC kufikia 76% ya nchi
nzima.
“Nataka
kuwahakikishia wananchi wote kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya
Uongozi shupavu wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania inakusudia kupanua usikivu wa redio za TBC nchi nzima”
amesisitiza Mhe. Bashungwa
Ameyataja maeneo mengine ambayo
miradi inaendelea kutekelezwa kwa ushirikiano wa TBC na UCSAF kuwa ni
pamoja na wilaya za Ngara (Kagera), Kyela (Mbeya), Ruangwa (Lindi),
Kilombero/Mlimba (Morogoro), Ludewa (Njombe), Tanganyika (Katavi),
Makete (Njombe), Uvinza (Kigoma), Mbinga (Ruvuma) na Ngorongoro
(Arusha).
Pia ametoa wito kwa Shirika la Umeme nchini (TANESCO)
kupeleka miundombinu ya umeme kwa vituo vyote ambavyo vinatumia genereta
mfano Karagwe ili kuendelea kupunguza gharama za uendeshaji wa miradi
hii.
“Kabla ya mradi kuanza kutekelezwa TBC, TANESCO na UCSAF
kaeni pamoja mjadiliane namna ya kutekeleza miradi hii kwa ufanisi ili
kutatua shida zinazowakabili wananchi wetu kwa kukosa huduma ya Habari
na Mawasiliano” amesisitiza Mhe. Bashungwa
Kwa upande mwingine
ameiomba Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS na TAMISEMI kupitia TARURA
waone namna ya kuwezesha kufikika eneo hilo la mradi wa Kisaki kwa
urahisi zaidi.
“Ombi hili ni sambamba na maeneo mengine yenye
mitambo ya kurusha matangazo ambayo miundombinu yake haiko vizuri mfano
eneo la Mnyusi- Tanga, Imagi – Dodoma, Matogoro – Songea na Mlima
kampuni – Katavi)”. Ameongeza Mhe. Bashungwa.
Amesema kuwa
Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (Ibara 125) inaelekeza Serikali
kuhakikisha kuwa inawekeza katika uimarishaji wa miundombinu ya
utangazaji kwa TBC.
Mhe. Bashungwa amefafanua kuwa kwa namna ya
pekee ibara ya 125 (f) inalekeza kuwa Serikali itahakikisha kuwa
“inaimarisha Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kwa kulijengea uwezo
wa rasilimaliwatu, fedha na vifaa vya kisasa ili liweze kufikisha
matangazo ya redio na televisheni nchini kote kwa ubora na usikivu
mzuri….”.
Aidha amesema Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa
wa Miaka mitano (2020/2021 – 2025/2026) umeainisha vipaumbele vyake
katika uwekezaji wa miundombinu ya Utangazaji ya TBC, ikiwemo upanuzi wa
usikivu wa redio, pamoja na miundombinu yake.
Ameisihi
Menejimenti ya Shirika hilo kuendelea kuwa wabunifu katika kuhabarisha
umma na kuwahakikishia kwamba Wizara yake itaendelea kuwapatia msaada
wowote wanaohitaji ili kutimiza malengo yake. Amelitaka TBC kuhakikisha
linaandaa maudhui yatakayokidhi matakwa ya jamii nzima ya watanzania
katika kukuza uzalendo, kudumisha mila na desturi za Watanzania na
kulinda tunu za Taifa.
Pia amelipongeza TBC kwa kazi nzuri
wanayoifanya ya kuwahabarisha wananchi wa makundi yote, ambapo amesema
anatambua jitihada zinazofanywa za kukamilisha uzinduzi wa chaneli mpya
ya televisheni ya TBC2 itakuwa mahususi kwa ajili ya vipindi vya vijana,
michezo na burudani ambayo ujenzi wa studio zake umekamilika
Mikocheni, Dar es Salaam.
Amewashukuru wadau wote ambao
wanafanikisha utekelezaji wa mradi wa usikivu wa TBC hapa nchini.
Amewataja baadhi ya wadau hao kuwa ni pamoja na Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Huduma za Maendeleo ya jamii,Wizara ya Mawasiliano na
Teknolojia ya Habari na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa
kuendelea kufadhili miradi hii ya Upanuzi wa Usikivu ambayo inatarajiwa
kutatua changamoto za Usikivu hivyo kuwezesha wananchi kupata huduma ya
habari na Mawasiliano kwa urahisi zaidi.
Amesema uzinduzi wa
kituo hiki ni hatua muhimu katika kutekeleza malengo Serikali katika
kufisha habari kwa wananchi wote, mahala popote kwa lengo la
kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha kwa njia ya redio, televisheni na
mitandao ya kijamii. TBC kikiwa ni chombo cha Utangazaji cha Umma,
kimetekeleza jukumu hili kwa vitendo.
Matangazo ya
Redio za TBC kupitia kituo hiki yanatarajiwa kuwafikia wananchi katika
vijiji vya Mvuha, Dhutumi, Bwakila Chini, Dakawa, Mngazi,
Milengwelengwe, Sesenga, Nyalutanga, Mdokonyole, Gomelo, Kisaki Station,
Matambwe, Kolelo, Lukange, Mgata, Ngerengere, Singisa na kwingineko).
Maeneo mengine yatakayonufaika na mradi huu ni katika Wilaya za jirani
za Kilombero, Rufiji na Kilwa.
“Kuzinduliwa kwa matangazo ya
Redio katika kituo hiki cha Kisaki, ni utekelezaji wa Ilani ya CCM (2021
– 2025), ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu kuzinduliwa kwake”.amesisitiza
Mhe. Bashungwa.