Home Burudani KWAHERI WAZIRI ALLY MWOKOA JAHAZI LA JUWATA.

KWAHERI WAZIRI ALLY MWOKOA JAHAZI LA JUWATA.

0

**************************

Adeladius Makwega

Chamwino-WHUSM

JULAI 25, 2021 ni siku itakayokumbukwa milele  kwa wapenzi wa muziki nchini Tanzania, kwani ni siku ambayo  ndugu  yetu, rafiki yetu, kaka yetu, baba  yetu na mzee wetu Waziri Ally Seifu (Waziri Njenje ) amezikwa huku kwao Pongwe, Mkoani Tanga.

Walio wengi wanamfahamu Waziri Ally kama Kiongozi tu wa-The Kilimanjaro Band(Wana Njenje) bila ya kufahamu kuwa  gwiji huyu aliwahi kufanya kazi kubwa sana za  muziki wa dansi akiwa na  bendi kongwe za wakati huo nchini Tanzania.

Kumuenzi mwanamuziki huyu, leo hii nakata mbuga hadi mwaka 1979 na nakukuta na na wimbo wa Sogea Karibu ulioimbwa na wana Juwata Jazz Band (Wana J.J.B) ambayo ilikuwa bendi inayomilikiwa na Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania(JUWATA).

Akiwa na wana J.J.B Waziri Ally alifanya kazi kubwa sana kuliokoa jahazi la  Juwata Jazz  Band katika wimbo  huo vinginevyo wimbo huo usingerekodiwa au kuwa kama ulivyo leo hii.

Nisimalize  uhondo ebu soma  mashairi ya  wimbo huo:

                            Sogea karibu, Nikueleze

                            Usije shangaa, Imekuwaje

                           

                            Upate fahamu sasa, Nakueleza

                            Ndoa yetu (changa), Imevunjika

                            Nilikupeleka kwa wakwe zako, Ukaonane na ndugu zangu ehhh

                            Hata mama yako  alifurahi sana, Ndugu zangu walikupenda sana

                            Lengo letu dada ni kuoana, Kama tukichunga heshima yetu ehhh.

                           

                            Ehh Bwana Waziri Waziri(Kinanda kinachezwa)

                           

                            Nilikupeleka kwa wakwe zako, Ukaonane na ndugu zangu ehhh

                            Hata mama yako  alifurahi sana, Ndugu zangu walikupenda sana

                            Lengo letu dada ni kuoana, Kama tukichunga heshima yetu ehhh.

                            Sasa nasikia, Umefanya visa vingi ee,

                            Hata mama yangu, Umthamieee

                            Ikiwa mambo yenyewe ni hivyo, Mbona mazito

                            Dada mimi nimeshindwa, Siwezi kukuoa tena.

                          

                            Nilikueleza toka zamani, Kitu kimoja,

                         Uchunge  heshima kwa wakwe zako, Ukapuuza

                       

                         Sasa nasikia, Umefanya visa vingi ee,

                         Hata mama yangu, Umthamieee

                     

                         Maji yakishamwagika, Hayazoleki

                         Kilichobakia sasa ni majuto

                         Nenda kwenu kwa salama

                         Sasa nasikia, Umefanya visa vingi ee,

                         Hata mama yangu, Umthamieee

                     

                                 Ponda

Mashairi ya wimbo huu  yametungwa na  Kakere Besela mnamo mwaka 1979 ndani ya   albam ya Mpenzi Zarina yenye nyimbo nane nazo ni Mpenzi Zarina, Mwana Acha Wizi, Uzuri si Shani, Epuka Tabia Mbaya, Sogea Karibu, Vijana Tujitokeze, Selemani, na Talaka. Sogea Karibu uliimbwa na Hassan Bitchuka na unapousikiliza utabaini kuwa  kinanda  kimepigwa  kwa ustadi mkubwa mno, hiyo ni kazi yake  Waziri Ally.

 “Sababu kubwa  za kupigwa  kinanda  sehemu kubwa   ya wimbo huu ni kuwa wapigaji wa vyombo vya upepo (Tarumbeta na Sax) waligoma kwa  sababu wakidai kuwa  wimbo huo ni mbaya mara baada ya mashairi kutungwa na wakati wa mazoezi ndipo mzozo huo uliibuka.” Anasema Masoud Masoud Mtangazaji Mkongwe wa TBC ambaye pia ni mdau wa muziki wa dansi nchini.

Masoud Masoud anasema kuwa mgogoro huo ukiwa chini ya uongozi wa  mwanamuziki Joseph Lusungu wakaamua kutoshiriki katika kazi hiyo. Cha kushangaza  wimbo huo  uliporekodiwa Waziri Ally aliziba  pengo la waliofanya mgomo huo na Bwana Waziri Ally  akakipiga kinanda  kwa ustadi mkubwa.

“Sogea Karibu  ukawa wimbo maarufu sana kati ya miaka 1970 na 1990 na hilo likawa mshangao mkubwa sana  si kwa akina Joseph  Lusungu tu bali  kwa Watanzania wote na wapenzi wa muziki wa dansi.” Anasema  Masoud Masoud.

Waziri Ally ameonyesha ubunifu na umahiri mkubwa hata ukiangalia  nyimbo  zake na mtindo wake akiwa na Wananjenje utabaini kuwa ilikuwa ni ngumu mtu kusikia muziki wake  pahala pengine bali kwa ni Wananjenje tu anasema kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya  Sanaa wa Wizara ya Habari , Utamaduni , Sanaa na MIchezo Ndugu Mfaume Said.

“ Alichokifanya  katika wimbo wa Sogea Karibu ni Uzalendo wa Kimuziki maana wengine waligoma kuimba na kurekodi lakini  yeye akaamua  kuokoa jahazi la muziki  lakini pia aliokoa  jahazi la Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania (JUWATA) kwani wafanyakzi wanamsemo wao kuwa Solidarity Forever-Mshikamano Daima.” Aliongeza Kaimu Mkurugenzi  huyo wa Maendeleo ya Sanaa wa Wizara ya Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo.

Naweka  kalamu yangu chini katika makala haya kwa kusema Waziri Ally anawaaga-akisema Pongwe Kwaheri, Tanga Kwaheri, CHAMUDATA Kwaheri, Wapenzi wa muziki wa Tanzania Kwaheri, The Kilimanjaro Band Kwaheri na Watanzania Kwaherini.