Home Mchanganyiko CCM PWANI YAIUNGA MKONO SERIKALI KUINGILIA SAKATA LA TOZO ZA MIAMALA-MANENO

CCM PWANI YAIUNGA MKONO SERIKALI KUINGILIA SAKATA LA TOZO ZA MIAMALA-MANENO

0
……………………………………………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
CHAMA Cha Mapinduzi mkoani Pwani , chini ya halmashauri Kuu yake ya CCM,imeunga mkono hatua na mwenendo wa Mwenyekiti wa CCM Taifa ,Samia Suluhu ,kuingilia kati sakata la tozo za miamala linalotikisa kwa sasa ,ili kuwaondolea makali wananchi.
Kimeweka bayana ,hatua ya kusikiliza kilio cha watanzania kuhusu kurejesha tozo za awali za miamala itasaidia kupunguza ama kuondoa malalamiko hayo ambayo yamekuwa wimbo kwa sasa.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani ,Ramadhani Maneno aliyasema hayo ofisini kwake wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na masuala mbalimbali ya utekelezaji wa ilani .
Alisema ,kwa niaba ya wanaCCM na halmashauri kuu mkoa , Rais Samia ameagiza mawaziri wenye dhamana wakae chini na wadau kuzungumzia suala hilo kwa kina ili lipatiwe ufumbuzi.
Maneno alielezea ,CCM ilimkabidhi mwenyekiti wa CCM Taifa ilani ,ambapo ndani ya ilani imeelekezwa mambo mbalimbali ikiwemo kusikiliza kero za wananchi na kuangalia namna ya kuzitatua .
“Kwa hili Rais Samia ,amemuunga mkono ilani iliyomuweka madarakani ,na sisi kwa kauli moja tunamuunga mkono “
Mwenyekiti huyo mkoa alibainisha ,anaimani serikali haitoishia hapo kwa kuwa ikimaliza kusikiliza na kujua mwelekeo itatoa majibu namna itakavyoleta ufumbuzi wa suala hili .
Kwa upande wa wananchi Kibaha akiwemo Kelvin Emil na Salimu Mdoe walieleza ,serikali idhamirie kutatua changamoto hii haraka ,pasipo kuchelewesha matokeo kama suala la punguzo katika vifurushi .
Kelvin alieleza ,vifurushi gharama ilipanda na wananchi wamepiga kelele lakini wanashangaa kuona limeibuka suala jingine la maumivu mengine ya tozo za miamala.
“Yaani ni simu ,vifurushi, tozo ,kiukweli tunaumia sisi wananchi wa chini, ujue vijijini kuna watanzania ambao wanatumiwa fedha na watoto na ndugu zao ,mashuleni wanafunzi ,ada mashulenj hivi hawa hawajaangaliwa kweli ,Hatujakataa serikali ina mipango mizuri ila wangebanwa walichonacho na sio mlolongo unaobana hadi maskini ” alifafanua Kelvin .
Alisema suala hili limekuwa na athari kwa wahangaikaji ,wamachinga ,wafanyakazi wa ndani ,madereva boda boda .
Nae Mdoe alisema kwamba ,bora serikali imeingilia kati suala hili maana ingekaa kimya ,wapo wengi waliokuwa wanaumia .
Aliiomba serikali kuendelea kusikiliza kero za wananchi na kuzifanyia kazi na ilete matokeo ya haraka kwa maslahi ya wananchi, na serikali kijumla.
Hivi karibuni waziri wa TAMISEMI Ummy Mwalimu alieleza ,tozo hizi zinamanufaa kwa wananchi kwa kutatua masuala ya maendeleo katika sekta ya elimu ,afya,miundombinu ya barabara vijijini .
Hata hivyo licha ya serikali kuona umuhimu wa watanzania kushirikiana kutatua changamoto mbalimbali zinazogusa jamii lakini imegeuka maumivu na kuisisitiza serikali kuvalia njuga punguzo la tozo hizi ili zisiendelee kuumiza wanyonge .