Home Mchanganyiko HALMASHAURI YA MADABA KINARA MIKOPO YA MAKUNDI MAALUM

HALMASHAURI YA MADABA KINARA MIKOPO YA MAKUNDI MAALUM

0

Na Muhidin Amri,
Madaba

HALMASHAURI ya wilaya Madaba mkoani Ruvuma, imetoa jumla ya Sh.87,000,000 sawa na asilimia 100 kama mikopo isiokuwa na riba kwa makundi maalum ya vijana,wanawake na walemavu kwa mwaka wa fedha ulioishia Mwezi Juni 2021.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Shafi Mpenda amesema hayo  katika hafla fupi ya kukabidhi vyeti kwa  viongozi wa vikundi vya kijamii vilivyofanikiwa kusajiliwa kwa njia ya mfumo mpya  wa mtandao(Online).

Mpenda amesema,mwaka wa fedha  2019/2020  Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani ilitoa kiasi cha Sh.30,000,000 kati ya hizo  vikundi  12 vya wanawake vilipata Sh.25,300,000, kikundi 1 cha vijana Sh.3,000,000 na kikundi 1 cha walemavu kilipata Sh.2,000,000.

Amesema, kwa mwaka wa fedha 2020/2021  Halmashauri iliweka lengo la kutoa mikopo ya Sh,74,000,000  hata hivyo, wamefanikiwa  kutoa  Sh. milioni 87 kati ya hizo wanawake  wamepata Sh.58,338,000,vijana Sh 19 na walemavu wamepata Sh.10.

Kwa mujibu wa Mpenda, hayo ni mafanikio makubwa kupatikana  tangu Halmashauri ya Madaba ilipoanzishwa rasmi mwaka 2015 na wataendelea kuboresha kiwango  cha mikopo kadri Halmashauri itakavyofanya vizuri kwenye makusanyo yake ya ndani.

Aidha amesema, Halmashauri imeanza kufanya utambuzi  rasmi wa vikundi  123 vya kijamii  vilivyosajiliwa kwa mfumo wa mtandao  na utekelezaji wa maagizo ya Serikali  kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inavyotakaza.

Amesema,hatua hiyo imesaidia  kuongeza mahusiano kati ya ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri na wana vikundi wenyewe ambao kupitia hafla hiyo watafahamu wapi pa kwenda pindi wanapohitaji mikopo au huduma nyingine ambazo zinahitaji  ushauri na msaada wa  wataalam.

Mpenda ameeleza kuwa,lengo la  kukutana na wana vikundi  lina lenga kufahamiana, kutengeneza mkakati na utaratibu mzuri utakaosaidia kuboresha vikundi hivyo kupitia idara ya maendeleo ya jamii na namna wana vikundi wanavyoweza kupata elimu juu ya kuendesha vikundi.

Amesema,Halmashauri ya wilaya Madaba itaendelea kutoa ushirikiano kwa wanananchi ili vikundi vinavyoanzishwa na kuibuliwa  ili viwe na tija na viwasaidie kuboresha maisha yao kupitia miradi  husika,  na kuitumia ofisi ya Mkurugenzi na wataalam waliopo kupata huduma bora na kutoa taarifa pale wanapoona kuna changamoto katika uendeshaji wa vikundi vyao.

Kwa upande wake Afisa maendeleo ya jamii  msaidizi wa Halmashauri hiyo Bashiru Mgwasa amesema,jumla ya vikundi  114 vimesajiliwa kati ya hivyo vya wanawake 48,vijana 16 watu  wa kundi  maalum 8 na mchanganyiko 42.

Mgwasa amesema, jumla ya wanachama waliosajiliwa kupitia vikundi hivyo ni 1680 kati yao wanaume 443,wanawake 1237 na vikundi hivyo  vinatoka katika vijiji 22 vilivyopo katika kata zote 8 za Halmashauri ya wilaya Madaba.

Amesema, kwa kuwa vikundi hivyo vinajishughulisha na masuala ya fedha na vinatoa fursa kwa watu kujiendesha kiuchumi,ni muhimu kuwa na kanuni na taratibu za namna  bora ya kujiendesha kwa kuzingatia  misingi ya utawala bora ikiwemo uwazi na uwajibikaji katika vikundi.

Hata hivyo amesema, changamoto kubwa ni baadhi ya maeneo katika kuna tatizo la upatikanaji wa mtandao(Network) kama Mateteleka,Ngadinda,Maweso,Ifinga na Igawisenga jambo lililosababisha vikundi vilivyopo katika maeneo hayo kutosajiiwa kwa mfumo wa mtandao.

Kwa upande Mwenyekiti wa Halmashauri ya Madaba Theofanes Mlelwa amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Shafi Mpenda kwa kusimamia vizuri suala la mikopo kwa makundi ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.

Hata hivyo,ameagiza  Idara ya maendeleo ya jamii kuendelea kuvitambua vikundi katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa  na kutoa mikopo kwa wananchi hasa wenye mahitaji maalum ili waweze kujitegemea na kuondokana na umaskini.