Home Mchanganyiko DC MGEMA ATANGAZA VITA NA WEZI WA MIUNDOMBINU YA UMEME

DC MGEMA ATANGAZA VITA NA WEZI WA MIUNDOMBINU YA UMEME

0

Mkuu wa wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Pololet Mgema akiangalia uharibifu wa miundimbonu ya umeme katika Transifoma  iliyopo katika mtaa wa Mabatini kata ya Misufini Manispaa ya Songea uliofanywa na watu wasiofahamika ambao wamekata waya mkubwa unaotoa umeme kwenye Transifoma na kupeleka kwenye nguzo kabla ya kwenda kwa wateja.

Meneja wa Shirika la Umeme(Tanesco)Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Frolence Mwakasege akimuonesha jana mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema Transifoma ambayo imeshindwa kufanya kazi baada ya watu wasiofahamika kukata waya unaosambaza umeme kutoka kwenye Transifoma hiyo kwenda kwa wateja katika mtaa wa Mabatini  Manispaa ya Songea.

Picha zote na Muhidin Amri

…………………………………………………………………….

Na Muhidin Amri,Songea

MKUU wa wilaya ya Songea Pololet Mgema,ametangaza vita dhidi ya waharifu  na watu wanaojihusisha na wizi wa miundombinu ya umeme na miradi ya kimkakati  inayotekelezwa yenye lengo la kuchochea kukua kwa uchumi katika maeneo mbalimbali  wilayani Songea.

Mgema ametoa kauli hiyo jana wakati akiongea na  wakazi wa Mtaa wa  Mabatini kata ya Misufini kufuatia watu wasiofahamika kufanya uharibifu  na kuiba waya mkubwa(Kopa)  katika moja ya Transifoma inayosambaza umeme  na kusababisha  ukosefu wa umeme  na hasara kubwa kwa Tanesco.

Amesema, kuanzia sasa Serikali haitakuwa na huruma kwa mtu au kikundi cha watu wanaojihusisha na vitendo vya uharifu hasa kwenye miundombinu ambayo inajengwa kwa fedha nyingi za walipa kodi.

Amesema, umeme ni nishati muhimu  kwa uchumi wa nchi,kwa hiyo ni wajibu wa kila mmoja kuwa mlinzi na kulinda miundombinu hiyo  inayojengwa kwa lengo la kuchochea na kuharakisha maendeleo.

Mkuu wa wilaya, amewataka wananchi kutoa taarifa na kuwafichua watu wanaojihusisha na matukio ya wizi wa miundombinu ya umeme na miradi mingine inayotekelezwa katika wilaya hiyo  na mkoa wa Ruvuma, kwani vitendo hivyo vinarudisha nyuma  malengo ya Serikali ya kuboresha huduma za kijamii.

Mgema ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama,amewaomba watendaji wa wa Serikali ngazi mbalimbali katika manispaa ya Songea,wenyeviti wa mitaa na viongozi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kukomesha vitendo hivyo vinavyorudisha  nyuma maendeleo.

Kwa upande wake meneja wa shirika la umeme Tanesco mkoa wa Ruvuma Frolence Mwakasege ameeleza kuwa,  tukio hilo  limetokea  majira ya saa saba usiku kuamkia jana(leo) katika mtaa huo jirani na Msikiti wa mkoa na hilo ni tukio la sita kutokea katika Manispaa ya Songea.

Amesema,  watu wanaodhaniwa kuwa ni wezi, wamekata fensi ndogo ya waya  iliyojengwa kuzunguka eneo la Transifoma  na kwenda kukata waya mkubwa wenye urefu wa mita 20 unaotoka kwenye Transifoma  hadi katika nguzo kabla ya kupeleka umeme kwenye  makazi ya watu .

Aidha amesema,  wizi huo umelisababishia shirika hasara ya zaidi ya shilingi milioni 12 kwani waya ulioibiwa ni wa gharama kubwa ambapo bei ya mita moja ni kati ya shilingi 180,000 hadi 200,000 na amewataka wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona vitendo vya  watu kuhujumu miundombinu  ya shirika hilo.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mwakasege,mbali na tukio  la jana,pia katika wilaya ya Mbinga  kumewahi kutokea wizi wa aina hiyo ambapo watu wameharibu miundombinu ya Tanesco na kuiba baadhi ya vifaa na tayari wamefikishwa katika vyombo vya sheria  kwa kosa la kuhujumu miundombinu ya umeme.

Amesema,serikali imekuwa ikijitihadi sana kuboresha miundombinu yake,hata hivyo baadhi ya watu wachache wanarudisha nyuma juhudi  hizo  kwa kuharibu kwa makusudi miundombinu ya umeme na kuisababishia Serikali hasara kubwa.

Mwakasege,ameiomba jamii kushirikiana na Tanesco kulinda na kuwa walinzi wa  miundombinu ya umeme kwani nishati hiyo ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mabatini  Hashimu Nakamu ,amelaani tukio hilo  kwani limesababisha  wananchi  wa mtaa huo na mtaa jirani wa Msikitini  kukosa baadhi ya huduma muhimu.

Amesema, kuanzia sasa wataanza rasmi ulinzi wa jadi(Sungusungu)katika mtaa wao ili kukomesha kabisa  tabia ya  watu wachache wanaojihusisha na vitendo vya uharifu  ikiwemo  kuhujumu miundombinu na miradi  inayojengwa na serikali  yenye lengo la kuchochea maendeleo.