Home Mchanganyiko NAIBU WAZIRI ATEMBELEA MGODI WA MAKAA YA MAWE WA RUVUMA COAL

NAIBU WAZIRI ATEMBELEA MGODI WA MAKAA YA MAWE WA RUVUMA COAL

0

Mkurugenzi wa Kampuni ya Ruvuma Coal Ltd inayochimba makaa ya mawe katika kijiji cha Sara  na Paraadiso wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Ryan Weinard kushotoa akimueleza jambo Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande katikati aliyetembelea mgodi huo juu ya uzalishaji na soko la makaa hayo,kulia mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande wa kwanza kushoto akikagua sehemu ya shehena ya makaa ya mawe katika Mgodi wa Ruvuma Coal Ltd uliopo kijiji cha Paradiso wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, yanayosubiri kusafirishwa kwenda katika maeneo mbalimbali,katikati Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo na kulia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Juma Mnwele.

Picha na Muhidin Amri,

……………………………………………………………………..

Na Muhidin Amri,Mbinga

ZAIDI ya wananchi  224 kati yao 100  kutoka katika vijiji vinavyozunguka Mgodi wa Ruvuma Coal Ltd, unaojihusisha na uchimbaji wa makaa ya mawe katika vijiji vya Ruanda na Sara wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamepata ajira  ya kudumu tangu kuanzishwa kwa mgodi huo katika kipindi cha mwaka mmoja.

Meneja wa mgodi huo Benedict Mushingwe amesema hayo, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa usimamizi na utunzaji mazingira  kwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande.

Amesema,kampuni  kupitia mgodi wa Ruvuma Coal Ltd ilifanya uamuzi wa kuchimba madini ya makaa ya mawe ili kuitikia wito wa Serikali wa kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda kwa kuwa makaa ya mawe ni chanzo cha nishati yenye bei rahisi katika uendeshaji wa mitambo na viwanda.

Amesema, tangu mgodi huo ulipoanzishwa mwaka mmoja uliopita kumekuwa na faida nyingi  zilizopatikana ikiwemo kutoa kandarasi kwa kampuni  nyingine kama vileTNR, Suma Jkt  na Avco ambazo zimechangia kutoa ajira kwa watu 227.

Mushingwe ametaja faida  nyingine zilizopatikana tangu kuanzishwa kwa mgodi huo ni kuchochea ukuaji wa uchumi na biashara kama maduka na vifaa vya ujenzi,mama na baba lishe na huduma za kifedha.

Aidha amesema,mgodi unanunua bidhaa mbalimbali kama nyama,matunda na mboga mboga zinazozalishwa na vijiji vinavyozunguka mgodi kwa ajili ya wafanyakazi wake hali iliyosaidia sana kuchochea kukua kwa uchumi na maisha ya wananchi wa vijiji vinavyozunguka mgodi.

Pia Mgodi wa Ruvuma  Coal Ltd unalipa kodi kwa Mamlaka ya mapato(TRA)malipo ya Mrahaba Tume ya madini,malipo ya tozo kwa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga na kuchangia miradi ya maendeleo ya jamii kwa vijiji vinavyozunguka mgodi.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande amesema, Serikali inapenda  kuwakaribisha wawekezaji kuja nchini kuwekeza kwenye migodi  kwa  maslahi ya wananchi na nchi yetu.

Hata hivyo,amewataka wamiliki wa migodi ya makaa ya mawe kuzingatia sheria na taratibu za uhifadhi wa mazingira katika maeneo wanayochimba, kwa kupanda miti  na yahakikishe yanakuwa na mpango madhubuti kurejesha ardhi katika hali ya awali mara baada ya shughuli ya uchimbaji kukamilika ili kulinda afya za binadamu wanaoishi  kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi huo.

Amesema,mazingira ndio uhai wa binadamu,hivyo ni lazima kuyatunza na kuyalinda kwa gharama yoyote na ameagiza magari yote yanayosafirisha makaa ya mawe kudhibiti vumbi kwa kufunga maturubai wakati wa kusafirisha ili lisisambae  hadi kwenye makazi ya watu.

Naibu Waziri Chande,amemuamgiza Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo  kushirikiana na watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha madereva wa malori na  wamiliki wa migodi wanatekeleza sheria za usalama na utekelezaji wa usimamizi na utunzaji wa mazingira.

“uwekezaji wowote ni lazima uzingatie Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004,ikiwa ni pamoja na kufanya tathimini ya athari ya mazingira kwa kuwa ni takwa la kisheria”amesema.

Amewataka wataalam wa Baraza la Taifa la usimamizi wa mazingira(NEMC) kanda ya Kusini, kufanya  ukaguzi wa mara kwa mara kwenye migodi  ili kuhakikisha masuala ya uzingatiaji wa sheria ya mazingira yanakuwa endelevu.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo amesema, zipo changamoto za kimazingira  zinazotokana na shughuli za migodi  kwa baadhi ya  makampuni kutozingatia taratibu za kimazingira kwa kumwaga maji katika maeneo ya mgodi na  barabarani pale yanaposafirisha makaa ya mawe kwenda katika maeneo mbalimbali.

Aidha amemueleza Naibu Waziri Chande  kuwa,kucheleweshwa kwa mchakato wa ulipaji wa fidia  kwenye maeneo ya uchimbaji hasa kampuni ya Ruvuma Coal Ltd ambayo hadi sasa bado haijalipa fidia kwa wananchi  vya Sara na  Ruanda waliochukuliwa maeneo yao kupisha shughuli za uchimbaji kumepelekea kuwepo kwa malalamiko mengi.

Amesema, baadhi ya makampuni  kuhifadhi makaa ya mawe kwa muda mrefu zaidi ya miezi sita bila kuzingatia taratibu za kiusalama na kimazingira, hivyo kuhatarisha usalama wa wananchi wa vijiji vinavyozunguka migodi hiyo