Home Mchanganyiko SIMANJIRO WAADHIMISHA KWA KAZI SIKU 100 ZA RAIS SAMIA 

SIMANJIRO WAADHIMISHA KWA KAZI SIKU 100 ZA RAIS SAMIA 

0

 …………………………………………………………..

Na Gift Thadey, Mirerani

Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara na wanachama wa CCM wa eneo hilo, wameathimisha siku 100 za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kusafisha mazingira ya kituo cha afya Mirerani, wamejitolea damu na kukabidhi msaada wa vifaa vya kufanyika usafi.

 

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Katibu wa UVCCM Wilaya ya Simanjiro, Bakari Mwacha amesema badala ya kusherehekea siku 100 za Rais Samia kwa kufanya semina au makongamano wameona washiriki madhimisho hayo kwa kufanya kazi ya kijamii.

 

Mwacha amesema vijana na wananchama wa CCM wamesafisha mazingira ya kituo cha afya Mirerani, wamejitolea damu na kukabidhi vifaa vya usafi ili kuadhimisha siku 100 za Rais Samia.

 

Amesema wamenunua vifaa vya kusafisha mazingira vya gharama ya shilingi 220,000 ikiwemo makarai, madekio, mafyekeo, mavyagio na kujitolea unit 14 za damu.

 

Mgeni rasmi wa shughuli hiyo, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Simanjiro, Ally Kidunda amewapongeza vijana na wanachama wa chama hicho kwa kushiriki shughuli hizo.

 

Kidunda amesema kituo hicho cha afya Mirerani, kinahudumia wananchi wa kata za Mirerani, Endiamtu, Shambarai, Naisinyai na kata jirani za mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

 

Amesema damu waliyojitolea itawasaidia wanawake wajawazito watakaohitajika kufanyiwa upasuaji, watu watakaopata ajali na kulazimika kuongezewa damu ikiwemo wachimbaji madini.

 

Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mirerani, Dk Deogratius Mazengo amewashukuru wote waliojitokeza kujitolea, kutoa msaada wa vifaa vya usafi na kusafisha mazingira.

 

“Hapa ni nyumbani kwa wagonjwa hivyo siyo vyema kuwa na mazingira machafu, tunawapongeza wale wote waliojitokeza na kufanya haya yote kwa manufaa ya jamii inayotuzunguka,” amesema Dk Mazengo.

 

Katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Simanjiro, Mosses Makeseni amesema katika kuadhimisha siku 100 za uongozi wa Rais Samia, kwa kushiriki shughuli hizo za kijamii pamoja na wanachama wa chama hicho wa eneo hilo.

 

Katibu wa UVCCM Kata ya Loiborsiret Matei Damas amesema wao kama vijana wameona fahari kushiriki shughuli hiyo ya vitendo Kwa kumpongeza Rais Samia kwa kutimiza siku 100 za uongozi wake.

 

Mwanachama wa CCM Semeni Yombe, amesema wamefanya shughuli hizo za kijamii kwa furaha kwenye kituo cha afya Mirerani  katika maadhimisho hayo ya siku 100 za utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.