Home Mchanganyiko NAIBU WAZIRI NDEJEMBI AIELEKEZA TPSC KUWAANDAA WATUMISHI KIDIJITALI

NAIBU WAZIRI NDEJEMBI AIELEKEZA TPSC KUWAANDAA WATUMISHI KIDIJITALI

0

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Watumishi wa TPSC Makao Makuu na Kampasi ya Dar es Salaam leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa TPSC.

Baadhi ya Watumishi wa Umma wa TPSC Makao Makuu na Kampasi ya Dar es Salaam wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius (hayupo pichani) Ndejembi alipokuwa akizungumza nao leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa TPSC.

Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Selemani Shindika akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji ya Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Dar es Salaam kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na Watumishi wa TPSC Makao Makuu na Kampasi ya Dar es Salaam leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa TPSC.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wanafunzi kwenye moja ya madarasa ya TPSC Kampasi ya Dar es Salaam leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa TPSC.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akipata maelezo ya utunzaji wa kumbukumbu kutoka kwa Msajili Msaidizi, Bw. Faraja Mbwilo wa TPSC Kampasi ya Dar es Salaam leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa TPSC.

Makamu Mkuu wa Chuo, Utawala, Fedha na Mipango, Bibi. Asantina Sebastian akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi leo jijini Dar es Salaam wakati Naibu Waziri huyo akipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa TPSC.

………………………………………………………………………….

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameuelekeza uongozi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kutoa mafunzo yatakayowezesha kuwa na kizazi cha Watumishi wa Umma wanaoendana na mabadiliko ya teknolojia katika utoaji wa huduma. 

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha ziara yake ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa TPSC Makao Makuu na Kampasi ya Dar es Salaam.

Mhe. Ndejembi amesema, TPSC haina budi kutoa mafunzo ya kidijitali ili kutekeleza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa ya kidijitali ikiwa ni pamoja na kuuboresha Utumishi wa Umma kuwa wa kidijitali.

Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, ili kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa wakati, Watumishi wa Umma nchini wanapaswa kujengewa uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa njia ya kidijitali.

Akihimiza utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ya kuwataka waajiri kuwapeleka watumishi wao TPSC ili kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji, Mhe. Ndejembi amesema maelekezo hayo sio ombi bali ni lazima, hivyo akiwa ni msaidizi wa Waziri Mchengerwa atahakikisha anafanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa agizo hilo.

“Haiwezekani, Waziri mwenye dhamana ya Utumishi na Utawala Bora atoe maelekezo halafu yasitekelezwe na viongozi wanaosimamia taasisi za umma, hivyo nitahakikisha ninafanya ufuatiliaji,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, kwa bahati nzuri Chuo cha Utumishi wa Umma kina kampasi sita zilizoko Mbeya, Mtwara, Tabora, Tanga, Singida na Dar es Salaam, hivyo waajiri hawana kisingizio cha kutowapeleka watumishi wao kupata mafunzo kwani TPSC inatoa huduma hiyo kila kanda kupitia kampasi zake na kuongeza kuwa watumishi hao wanaweza kuhudhuria mafunzo hayo kwa awamu.

Mhe. Ndejembi amesema Waajiri watakaoshindwa kuwapeleka Watumishi wao TPSC kupata mafunzo watalazimika kutoa maelezo ya kimaandishi juu ya sababu za kutotekeleza maelekezo hayo.

Aidha, amewaasa Watumishi wa Umma kuhakikisha wanatekeleza maelekezo ya Mhe. Mchengerwa kwa kuwakumbusha waajiri kuwapatia fursa hiyo ya mafunzo TPSC.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Selemani Shindika amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuweka msisitizo wa maelekezo ya Mhe. Mchengerwa ya kuwataka waajiri kuwapekeleka watumishi wao TPSC kupata mafunzo.

Dkt. Shindika amesema, chuo chake ni jiko halisia la kuwapika Watumishi wa Umma kwani kinafundisha maadili na miiko ya Utumishi wa Umma ili Watumishi wa Umma watekeleze wajibu wao kikamilifu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji katika Kampasi ya Dar es Salaam ikiwa ni baada ya kuzitembelea Kampasi za Mbeya, Tabora, Mtwara, Singida na Tanga.