Home Michezo MKALAPA: TANURU LA KUPIKA WACHEZAJI TISHIO WA ‘VOLLEYBALL’ NCHINI

MKALAPA: TANURU LA KUPIKA WACHEZAJI TISHIO WA ‘VOLLEYBALL’ NCHINI

0

Mwanahawa Elisha (Jezi namba 10) wa Mtwara ambaye ni ‘seta’ bora wa mpira wa wavu kwa wasichana Tanzania akijaribu kupiga ‘spike’ dhidi ya Dar es salaam katika mchezo wao wa fainali ya UMISSETA dhidi ya Dar es salaam ambapo Mtwara ilishinda seti 3-0.

Mchezaji Elizabeth Gesi ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Makongo kutoka mkoa wa  Dar es salaam akijaribu kuudokoa mpira kwa wapinzani wao Mtwara katika mchezo mkali na wa kusisimua wa fainali ya UMISSETA ambapo Mtwara walishinda kwa seti 3-0.

Nahodha Msaidizi wa Mtwara Proscovia Conrad akiongea na waandishi wa habari mara baada ya mchezo wao wa fainali dhidi ya Dar es salaam

Kocha Mkuu wa Mtwara Gabriel Joshua ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Ardhi halmashauri ya wilaya Masasi akitoa tathmini ya micheo ya UMISSETA mwaka huu baada ya fainali kati ya Dar dhidi ya Mtwara ambapo Mtwara walishinda seti 3-0

******************************

Na Mathew Kwembe, Mtwara

Katika mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA yaliyomalizika hivi karibuni mkoani Mtwara, moja kati ya timu zilizokuwa moto wa kuotea mbali dhidi ya wapinzani wake kwenye mchezo wa mpira wa wavu (Volleyball) kwa wasichana ni timu mwenyeji ya Mtwara.

Timu hii ambayo inaundwa na vijana wadogo wa umri kati ya miaka 13 na 16 kutoka kijiji cha Mkalapa kilichopo umbali wa kilometa 35 kutoka mji wa Masasi, imezifunga timu zote ilizokutana nazo katika mashindano ya UMISSETA mwaka huu ikiwemo timu ya wavu wasichana ya mkoa wa Dar es salaam ambayo ilikubali kipigo cha seti 3-0 katika mchezo wao wa fainali.

Na hata katika mchezo wa robo fainali Mtwara waliifunga Tabora kwa kishindo seti 3-0 ambapo katika seti ya pili walishinda pointi 25-0.

Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa timu hiyo Gabriel Joshua, timu hiyo inaundwa na watoto kutoka kijijini Mkalapa, ambapo kila siku wamekuwa wakifanya mazoezi makali ya kujifua na michezo mbalimbali.

Gabriel ambaye ni mtumishi wa halmashauri ya wilaya ya Masasi kama Mkuu wa Idara ya ardhi kila siku baada ya muda wa kazi hulazimika kwenda Mkalapa kuwafundisha watoto hao mbinu mbalimbali.

Amesema timu yake imekuwa kali kwa sababu wachezaji wamezoeana kwa muda mrefu na alianza kuinoa timu hiyo tangu mwaka 2009 alipohamia Masasi na anasaidiwa na walimu wawili mmoja wa shule ya msingi na mwingine wa sekondari Mkalapa.

Amesema timu hiyo imekuwa na mafanikio mbalimbali pamoja na kuwa washindi wa pili wa ligi ya Muungano imefanikiwa kuwa mabingwa wa UMISSETA tangu mwaka 2018 na imetoa wachezaji wengi ambao sasa wanachezea timu mbalimbali kubwa nchini ikiwemo Jeshi stars.

“Miaka ya nyuma wachezaji wangu wengi walikuwa wakichukuliwa na timu za Dar es salaam ikiwemo Makongo lakini sasa wanabakia Mkalapa na tutaendelea kuchukua kombe la UMISSETA kila mwaka, kama ilivyo kwenye UMITASHUMTA,” amesema

Kauli ya Gabriel inaungwa mkono na Nahodha Msaidizi wa Mtwara Proscovia Conrad ambaye pia ni Mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Mkalapa aliyeanza kucheza Volleyball tangu akiwa darasa la nne.

“Tunawaona dada zetu wanachezea timu kubwa kama Jeshi stars inatupa hamasa nasi ya kujituma zaidi ili nasi tufanikiwe kuchezea timu kubwa,” amesema Proscovia.

Mbali na kufundisha timu ya wasichana ya UMISSETA, pia Gabriel hufundisha timu ya wasichana ya UMITASHUMTA ambayo nayo huundwa na wachezaji kutoka shule ya msingi Mkalapa.

“UMISSETA ya mwakani nitakuwa na kikosi kikali zaidi kuliko hiki kwani nina vijana wazuri wanaomaliza darasa la saba ambao wataingia sekondari ya Mkalapa,” amesema.

Kocha Gabriel amesema hamasa ya kupenda mchezo huo imewaingia hadi wazazi wa watoto wanaosoma shule ya msingi na sekondari Mkalapa kwani nao hawapo nyuma katika kufuatilia maendeleo ya watoto wao ambapo katika baadhi ya michezo ya UMITASHUMTA baadhi ya wazazi walifika kuona jinsi watoto wao wanavyocheza.

Timu ya mpira wa wavu wasichana ya Mtwara imekuwa bingwa mfululizo wa mashindano ya UMITASHUMTA tangu mwaka 2013 wakati timu ya wasichana ya sekondari wamekuwa mabingwa watetezi wa kombe hilo tangu 2018.