*******************
Mwenyekiti taifa wa chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA ) Hashim Rungwe amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutoa tamko la kuruhusu mikutano ya vyama vya siasa.
Hashim Rungwe ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanahabari ambapo amesema kitendo Cha kufungiwa kufanya mikutano ya kisiasa kinaminya haki yao ya kikatiba .
Amesema ibara ya tisa (G na H) inasema kwamba serikali na vyombo vyake vyote vya Umma vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote bila kujali rangi, dini au hali ya mtu na kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu,au upendeleo zinaondolewa nchini.
Aidha Rungwe akielezea yale aliyoyatekeleza Rais Samia katika siku mia moja za uongozi wake amesema ni miongoni mwa kazi za Rais kwa kuwa katiba inamtaka kuyatekeleza.
Hashim Rungwe ni miongoni mwa wanasiasa waliogombea nafasi ya Urais katika uchaguzi uliopita Octoba 2020 kupitia chama cha CHAUMMA hata hivyo kura zake hazikutosha kuwa Rais.