Home Michezo WAZIRI BASHUNGWA KUFUNGA MASHINDANO YA UMISSETA KWENYE UWANJA WA NANGWANDA SIJAONA

WAZIRI BASHUNGWA KUFUNGA MASHINDANO YA UMISSETA KWENYE UWANJA WA NANGWANDA SIJAONA

0

*********************

MTWARA- Julai 1, 2021                                  

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) kesho Julai 2, 2021 anatarajia kufunga Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari (UMISSETA) kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara. 

Mashindano haya yamejumuisha mikoa yote kutoka Tanzania Bara na Visiwani, yamefanyika kwenye viwanja vya Nangwanda Sijaona, Chuo cha Walimu Mtwara (TTC kawaida) Chuo cha Walimu Ufundi maarufu kama Mwasandube, na viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ufundi Mtwara ambapo yalinza Juni 21, 2021 baada ya kumalizika Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) yaliyofunguliwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Julai 08, 2021. Mashindano haya yameandaliwa na Wizara tatu zinazohusika na Elimu, Michezo na TAMISEMI chini ya Kamati ya Uratibu ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu wa Wizara hizo.

Michezo iliyoshindaniwa katika mashindano haya ni mpira wa miguu kwa wasichana na wavulana, mpira wa miguu maalum kwa wavulana (wenye ulemavu wa kusikia) mpira wa pete, mpira wa wavu kwa wasichana na wavulana, mpira wa mikono kwa wasichana na wavulana, mpira wa kikapu kwa wasichana na wavulana, mpira wa meza kwa wasichana na wavulana, riadha jumuishi, kwaya na ngoma. Pia kumekuwa na mashindano ya usafi katika mazingira wanayoishi. Fainali za mashindano hayo zinakamilika leo isipokuwa kwa mechi ya fainali kwenye mchezo wa soka itakayochezwa kesho mbele ya mgeni rasmi, ambapo zawadi mbalimbali zitatolewa kwa washindi. 

Mashindano ya mwaka huu yamekuwa na hamasa kubwa kwa kuwa yamepambwa na wasanii wa kizazi kipya ili kutoa hamasa na burudani. Kesho wasanii mbalimbali wa kizazi kipya wanaotamba hapa nchini pamoja na vikundi vya kwaya na ngoma za asili vilivyoshinda katika mashindano haya vitatoa burudani.

Baadhi ya wasanii ambao watapanda jukwaani kesho ni pamoja na Maarifa, Kala Jeremiah,GNacko,Mr.Blue, Shishi, Nandy na Sholo Mwamba.

Pia mashindano yamekuwa na mvuto wa kipekee kwa kuwa mikoa takribani yote imeleta wanamichezo wenye vipaji na hivyo kuzaa ushindani mkubwa. Aidha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyama vya michezo, mashirikisho na vilabu vya michezo mbalimbali vilialikwa kuja kuangalia vipaji mbalimbali.

Kauli mbiu ya michezo ya mwaka huu ni “Michezo, Sanaa na Taaluma kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda”