Home Siasa WAGOMBEA 12 WATEULIWA UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA KONDE

WAGOMBEA 12 WATEULIWA UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA KONDE

0

Wananchi na wagombea wakikagua fomu za uteuzi zilizobandikwa nje ya ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Konde, Kisiwani Pemba. Jumla ya wagombea kumi na mbili (12) wameteuliwa kuwania ubunge kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo hilo unaotarajiwa kufanyika tarehe 18 Julai, 2021.

……………………………………………………………………

NEC PEMBA

Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Konde, Yasini Jabu Hamis amefanya uteuzi wa wagombea kumi na mbili (12) ambao wanawania ubunge ili kujaza nafasi iliyowazi kwenye jimbo hilo. 

Bw. Hamis amesema kwamba kati ya wagombea hao wanawake ni watatu (3) na wanaume ni tisa (9). Amewataja wagombea hao kuwa ni pamoja na Sheha Mpemba Faki wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Salama Khamis Omar wa Civic United Front (CUF), Mohamed Said Issa wa Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), Yahaya Mwinyi Ali wa Sauti ya Umma (SAU) na Abdirahim Ali Slum wa National Convention for Constitution and Reconstruction-Mageuzi (NCCR-Mageuzi).

Wengine ni Ali Kassim Hamad wa Tanzania Labour Party (TLP), Mohamed Suleiman Said wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Rashid Hamad Said wa Demokrasia Makini, Salma Abdalla Hamad wa Chama cha Kijamii (CCK), Suleiman Khamis Rashid wa United People’s Democratic Party (UPDP), Issa Shaame Hassan wa National Reconstruction Alliance (NRA) na Fatma Rajab Omar wa Tanzania Democratic Alliance (ADA-TADEA).

Msimamizi huyo wa uchaguzi amesema kwamba kampeni za uchaguzi kwenye jimbo hilo zinatarajiwa kuanza tarehe 28 Juni, 2021 na kuhitimishwa tarehe 17 Julai, 2021 na kwamba uchaguzi unatarajiwa kufanyika tarehe 18 Julai, 2021. 

“Kwa sasa tumebandika fomu za uteuzi eneo la wazi kwa ajili ya wagombea kuzikagua na endapo hakutakuwa na pingamizi itakayopelekea kuenguliwa kwa mgombea, wagombea wote 12 wataanza kampeni kesho (tarehe 28 Juni, 2021,” amesema.

Bw. Hamis amewataka wagombea wote walioteuliwa kufanya kampeni kwa mujibu wa sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi ambayo wagombea wote wamtia saini kuyaheshimu na kuyazingatia maadili hayo.

Jimbo la Konde linafanya uchaguzi mdogo kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Mhe. Khatib Said Haji. Uchaguzi huo unafanyika sambamba na kata sita (6) za Tanzania Bara, ambazo ni Mbagala Kuu iliyopo Mkoa wa Dar es Salaam (Temeke), Ndirigish iliyopo Mkoa wa Manyara (Kiteto), Mitesa  na Nchemwa zilizopo Mkoa wa Mtwara (Masasi na Newala), Gare iliyopo Mkoa wa Tanga (Lushoto) na Chona iliyopo Mkoa wa Shinyanga (Ushetu).

-Mwisho-