Home Mchanganyiko MAFUNZO KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU CHANJO YA KIPINDUPINDU

MAFUNZO KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU CHANJO YA KIPINDUPINDU

0

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Jamii  kutoka Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii,Wazee, Jinsia na Watoto  Zanzibar Dkt. Fadhil Mohammed Abdalla akaimkaribisha Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya kufungua mafunzo ya siku moja kwa Waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali kuhusu Kampeni ya chanjo ya kipindupindu inayotarajiwa kutolewa kuanza tarehe 03 Julai, mwaka huu kwa shehia zote ambazo zimekuwa zikiathirika na kipindupindu mara kwa mara, hafla iliyofanyika Ukumbi wa ZSSF Kariakoo Mjini Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar akifungua mafunzo ya siku moja kwa Waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali kuhusu Kampeni ya Chanjo ya Kipindupindu inayotarajiwa kutolewa kuanzia tarehe 03 Julai mwaka huu kwa shehia ambazo zimekuwa zikiathirika na kipindupindu mara kwa mara, hafla iliyofanyika Ukumbi wa ZSSF Kariakoo Mjini Zanzibar.

Wadau wa Afya,Viongozi na watendaji wa Wizara ya Afya wakiwa katika picha ya pamoja na Waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali baada ya mafunzo ya siku moja kuhusu Kampeni ya Chanjo ya Kipindupindu yaliyofanyika Ukumbi wa ZSSF Kariakoo Mjini Zanzibar.

Afisa Afya ya Jamii kutoka Wizara ya Afya Bi Faiza Mohamed Abdul-kadir akitoa mafunzo kwa Waandishi wa Habari wa  Vyombo mbalimbali (hawamo pichani) kuhusu Chanjo ya Kipindupindu inayotarajiwa kutolewa kuanzia tarehe 03 Julai mwaka huu kwa Shehia ambazo zimekuwa zikiathirika na Kipindupindu mara kwa mara, hafla iliyofanyika Ukumbi wa ZSSF Kariakoo Mjini Zanzibar.

PICHA NA FAUZIA MUSSA/ MAELEZO ZANZIBAR.

******************************

Na Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar 25/06/2021

Waandishi wa Habari wametakiwa kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na Chanjo ya Kipindupindu ili ipate uwelewa zaidi na kujua muhimu wa chanjo hiyo.

Akifungua Mafunzo kwa  Waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu kutoka Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Dk Abdallah Ali Suleiman amesema  lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu kwa jamii ili kuondokana na  dhana potofu zinazotokana na chanjo hiyo

Amesema chanjo hiyo haina madhara yoyote kwa binadamu iko salama ambayo inatolewa kwa ajili ya kuikinga jamii na maradhi ya mripuko hivyo ameitaka jamii kuondoa shaka hiyo.

Ameeleza kuwa Chanjo ya Kipindupindu inatarajiwa kutolewa mwezi ujao katika shehia mbali mbali za Unguja na Pemba kwa maeneo ambayo huathirika sana kila unapotokea mripuko wa maradhi hayo.

Nae Afisa  Afya ya  Jamii Bi Fauza Mohamed Abdulkadir  amesema chanjo hiyo inatarajiwa kutolewa  kuanzia umri wa mwaka mmoja na kuendelea pamoja na wagonjwa wenye maradhi sugu yasiyoambukizwa ikiwemo presha sukari na mengineyo.

“Chanjo hiyo haitopaswa kupewa wagonjwa mahatuti na mama wajawazito na watoto chini ya mwaka mmoja”, alifahamisha Afisa huyo.

Kwa upande wake Mratibu wa Chanjo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dr. Vendelin Simon amesema kuwa chanjo iko salama tayari imeshatolewa katika nchi mbalimbali  na haijaleta madhara yoyote kwa waliotumia ambayo ni dawa ya  kunywa sio sindano hivyo ameisihi jamii kuwa na mwamko wa kushiriki kupata chanjo hiyo.

 .

Zoezi la utoaji wa Chanjo ya kipindupindu linatarajiwa kufikia zaidi ya watu laki 3 (300,000) katika Wilaya tisa za Unguja na Pemba ikiwa jumla ya shehia 58 lenye lengo la kutoa kinga kwa wananchi katika kipindi cha  miaka mitatu hadi mitano mpaka kumaliza dozi hiyo .