Home Mchanganyiko WAAJIRI NA MAMLAKA ZA NIDHAMU TEKELEZENI MAAGIZO YA TUME YA UTUMISHI WA...

WAAJIRI NA MAMLAKA ZA NIDHAMU TEKELEZENI MAAGIZO YA TUME YA UTUMISHI WA UMMA

0

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji (Mstaafu) Dkt. Steven J. Bwana (aliyekaa katikati) akisaini nyaraka wakati wa Mkutano wa Tume Na. 4 wa mwaka wa fedha 2020/2021 ulioanza jana Jijini Dar es Salaam. Wengine ni Mheshimiwa George Yambesi , Kamishna wa Tume (kushoto) na Bw. Nyakimura Muhoji (kulia) Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma. (Picha na PSC)

**************************

Waaiiri na Mamlaka za Nidhamu katika Utumishi wa Umma wamekumbushwa kutekeleza maagizo yanayotolewa na Tume ya Utumishi wa Umma kwa wakati na kama hawaridhiki na uamuzi na maagizo ya Tume wanayo nafasi na haki ya kukata rufaa kwa Mheshimiwa Rais.

Mwenyekiti  wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Dkt. Steven James Bwana amesema haya jana wakati wa Mkutano wa Tume Namba  Nne wa mwaka wa fedha 2020/2021 unaofanyika Jijini Dar es Salaam.  Katika Mkutano huu Tume itapokea na kutolea uamuzi Rufaa  107 na Malalamiko 06 yaliyowasilishwa na Watumishi mbalimbali wa Umma ambao hawakuridhika na uamuzi uliotolewa na Waajiri, Mamlaka za Ajira  na Mamlaka zao za Nidhamu.

“Tume imekuwa ikitoa maelekezo kwa Waajiri, Mamlaka za Nidhamu na Mamlaka nyingine lakini baadhi yao  wamekuwa wanakataa kutekeleza maagizo ya Tume bila kuwa na sababu za msingi. Tume ya Utumishi wa Umma imekabidhiwa Mamlaka ya kuhakikisha kuwa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma unaendeshwa kwa kuzingatia  Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo  iliyopo. Kama hawaridhiki na uamuzi na maagizo ya Tume wanayo nafasi na haki ya kukata rufaa kwa Mheshimiwa Rais, ambaye uamuzi wake ni wa mwisho”alisema Jaji (Mstaafu) Dkt. Bwana.

Akizungumza katika Mkutano huo, Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Mheshimiwa Balozi (Mstaafu) John Haule  alisema bado kuna tatizo katika utekelezaji wa maagizo yanayotolewa na Tume, mathalani baadhi ya Waajiri kutochukua hatua kwa wakati. “Ni muhimu kuchukua hatua kwa kuzingatia Sheria zilizopo” alisisitiza.

Kwa upande wake Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw.  Nyakimura Muhoji alisema Tume imekuwa ikizikumbusha mara kwa mara Mamlaka kuchukua hatua stahiki kama maelekezo ya Tume yanavyotolewa.

“Mamlaka zingine zimekuwa hazitekelezi maagizo yanayotolewa na Tume kwa wakati. Hali hii haiwezi kuendelea, ni lazima Tume itachukua hatua kwa Mamlaka ambazo zimekuwa hazitekelezi maagizo ya Tume” alisema Muhoji.

Mkutano wa Nne wa Tume  kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ulianza jana  tarehe 21 Juni na unafanyika hadi tarehe 02 Julai  2021,  Jijini  Dar es Salaam.

Tume ya Utumishi wa Umma inatekeleza majukumu haya kwa mujibu wa Kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (Marejeo ya mwaka 2019).