Home Mchanganyiko WAZIRI WA AFYA AFANYA KIKAO NA WATUMISHI WAKE KUTEKELEZA WIKI YA UTUMISHI...

WAZIRI WA AFYA AFANYA KIKAO NA WATUMISHI WAKE KUTEKELEZA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA

0

****************

Na.Catherine Sungura,Dodoma

Viongozi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wametakiwa kuwa na utaratibu wa vikao kila baada ya miezi mitatu pamoja na mawaziri wao kwa lengo la kujadili mafanikio na changamoto na kuziwekea mpango wa pamoja wa kuzipatia majibu.

Rai hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa kikao chake na watumishi wa Idara mbili zilizopo Kwenye wizara yake(Afya na Maendeleo ya Jamii) Cha kusikiliza na kutatua changamoto zinazoikabili wizara hiyo zikiwemo za watumishi hao.

Mkutano huo ambao umefanyika Kwenye viwanja vya wizara hiyo zilizopo Kwenye mji wa Serikali Mtumba ikiwa ni Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza tarehe 18-23 Juni, 2021.

Dkt.Gwajima amesema anatamani kuona wizara hiyo inakuwa ya mfano wa katika kutambua na kuzipatia majibu changamoto zinazowakabili watumishi wake na wateja wake hivyo, amewataka wakurugenzi kuweka utaratibu wa kukutana kila baada ya miezi mitatu.

“Changamoto nyingi zinaweza kutatuliwa ndani na viongozi yaani zipo ndani ya uwezo wetu kinachohitajika ni uratibu baina yetu, hivyo upo umuhimu wa kukaa pamoja kila baada ya miezi mitatu na kuongea na watumishi wetu kwa ajili ya kuchota mawazo na uzoefu”.Alisisitiza

Hata hivyo Dkt. Gwajima aliwataka watumishi hao kuwajibika na kuwa waadilifu wanapotekeleza majukumu yao na pia kutengeneza mfumo ambao utawajenga watumishi hao katika utumishi wenye viwango stahiki vya kitaifa na kimataifa.

Akielezea kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Kujenga Afrika tunayoitaka, kupitia utamaduni wa uadilifu ambao unastawisha uongozi wenye maono hata Katika mazingira ya migogoro”, Dkt. Gwajima alisema panapo migogoro wanapaswa kuchukua kama fursa kwa maana katika kuchambua asili ya mgogoro huo watapata mfumo utakaozuia kutokea kwa mgogoro siyo huo tu bali na mingine mingi na taasisi itaenda mbele zaidi.

Katika Maadhimisho haya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatoa huduma ya kuwasikiliza watumishi na wananchi kwenye viwanja vya ofisi zake zote zilizopo jijini Dodoma pia itafanya usafi kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma pamoja na kuwatembelea wagonjwa Kwenye vituo vya kutolea huduma jijini hapa.