Home Mchanganyiko WIZARA YAKUTANISHA WADAU KUJADILI RASIMU YA UWEKEZAJI KWA WANAWAKE KIUCHUMI

WIZARA YAKUTANISHA WADAU KUJADILI RASIMU YA UWEKEZAJI KWA WANAWAKE KIUCHUMI

0

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza na Wadau wa Maendeleo ya Jamii ( hawapo pichani) wakati wa majadiliano ya rasimu ya mapendekezo ya utekelezaji wa kuwawezesha Wanawake Kiuchumi, Mkutano huo umefanyika Jijini Dar es Salaam Juni 14, 2021.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wanawake (UN Women) Bi. Hodan Addouh akizungumza na Wadau wa Maendeleo ya Jamii (hawapo pichani) wakati wa majadiliano ya rasimu ya mapendekezo ya utekelezaji wa kuwawezesha Wanawake Kiuchumi, Mkutano huo umefanyika Jijini Dar es Salaam Juni 14, 2021.

Wadau wa Maendeleo ya Jamii, Mashirika ya Umoja wa Kimataifa na Mashirika yasiyo ya Kiserikali wakiwa katika mkutano wa pamoja wa majadiliano ya rasimu ya mapendekezo ya utekelezaji wa kuwawezesha Wanawake Kiuchumi, Mkutano huo umefanyika Jijini Dar es Salaam Juni 14, 2021.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wanawake (UN Women) Bi. Hodan Addouh akiteta jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu wakati wa mkutano wa pamoja wa majadiliano ya rasimu ya mapendekezo ya utekelezaji wa kuwawezesha Wanawake Kiuchumi, Mkutano huo umefanyika Jijini Dar es Salaam Juni 14, 2021.

********************************

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara Kuu ya  Maendeleo ya Jamii, kwa kushirikiana na Wadau wa maendeleo ipo katika maandalizi ya Mkutano wa  Jukwaa la Kimataifa la kuhuisha harakati za kizazi chenye usawa (Generation Equality Forum)  utakaofanyika Mwezi June 30 hadi Julai 2 mwaka huu Jijini Mexico.

Kupitia kikao hicho Serikali ya Tanzania inaazimia kutoka na rasimu ya utekelezaji wa namna ya kuwawezesha Wanawake kiuchumi pamoja na kuondoa changamoto zinazowakabili zikiwepo za ukatili wa kijinsia, kuboresha haki za kiuchumi, haki za uzazi, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuendana na teknolojia na ubunifu pamoja na kuwa na usawa katika uongozi na ngazi za maamuzi.

Akizungumza leo Mkoani hapa katika kikao hicho Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto anayeshughulikia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt John Jingu, amesema katika Jukwaa hilo, Serikali ya Tanzania ilichagua eneo moja la kumjenga Mwanamke kiuchumi.

Dkt Jingu amesema kuwa katika Mkutano wa Afrika, uliofanyika Nchini Ufaransa hivi karibuni, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipewa heshima ya kuchagua eneo moja, alichagua eneo la kumjenga Mwanamke kiuchumi na alichagua eneo la haki za kiuchumi kutokana na kutambua kuwa uwezeshaji Wanawake kiuchumi ambalo ni nguzo muhimu katika kuleta usawa wa kijinsia.

Amesema kupitia uwezeshaji Wanawake kiuchumi katika Jukwaa hilo, Tanzania imeona mambo ya kiuchumi ni muhimu katika ustawi wa Jamii na Familia, kwani yatamjenga Mwanamke kujiamini pamoja na kukabiliana na umasikini.

 “Mheshimiwa Rais atakuwa miongoni mwa Viongozi wa kundi la utekelezaji wa masuala ya haki za Wanawake za kiuchumi, hii ni dhamana kubwa ambayo tumepewa kama nchi, ni jukumu letu kuona kuwa tunaibeba na kuitekeleza kwa ufanisi na tija” amesema Dkt Jingu.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linashughulikia masuala ya Wanawake (UN Women) Bi. Hodan Addouh amesema Wanawake ni kundi kubwa ambalo linaweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi na hivyo ipo haja ya kutoa kipaumbele kuhusiana na masuala ya uwezeshwaji wao katika mkutano huo.

Kikao hiki cha Wadau wa Maendeleo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuwataka wadau kuchambua hali halisi ya changamoto zinaziwakabili wanawake na nini kifanyike kukabiliana nazo.

Jukwaa hilo lilizinduliwa katika jiji la mexico Mwezi Machi 29 hadi 31 mwaka huu na litakamilika tarehe 30 Juni hadi 2 Julai 2021.