Home Mchanganyiko TCCIA PWANI YAHIMIZA ONGEZEKO LA WANACHAMA ILI KUJIIMARISHA

TCCIA PWANI YAHIMIZA ONGEZEKO LA WANACHAMA ILI KUJIIMARISHA

0
……………………………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Chama cha wafanyabiashara wenye viwanda na kilimo (TCCIA ) ,Mkoani Pwani ,kimewahimiza wafanyabiashara na wakulima kujiunga uanachama  ili kujiimarisha na kuongeza nguvu ya pamoja kujiinua kiuchumi.
Pia kimewaasa vijana kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kujifunza na kupata uelewa wa kujiajiri kibiashara kupitia wabobezi wa viwanda na wafanyabiashara walio kwenye chama hicho.
Akizungumzia hatua wanazozichukua kukiinua chama na vipaombele ,makamu mwenyekiti -Biashara -Fadhil Gonzi alieleza ,mkoa umesheheni viwanda ni wakati wa wenye viwanda hao kuwa sehemu ya chemba yao ili kujikwamua kimaendeleo .
Suala jingine alieleza ,ni wanachama kupata fursa ya elimu ya biashara na kuwa na elimu ya nidhamu ya fedha ili kulinda biashara zao.
Gonzi ,alieleza kwamba pia watajitahidi wanachama wao kufikia soko la ndani na nje kwani ukosefu wa soko imekuwa ni changamoto na kilio cha kila kukicha.
“Kwanini Pwani tushindwe kuandaa maonyesho makubwa kama sabasaba ,mkoa ulishaanza na ulifanikiwa kwa kiasi chake lakini bdo tuna kazi ya kuwa kuandaa maonyesho makubwa zaidi ili kujitangaza na kubadilishana uzoefu” alifafanua Gonzi .
Mwenyekiti wa TCCIA Pwani ,Saidi Mfinanga alifafanua akiwa kama mtaalamu wa masuala ya fedha ,uchumi na ushauri wa kodi atahakikisha wanashirikiana na wadau mbalimbali kutatua changamoto ya ukosefu wa masoko na kuwapa elimu ya biashara wanachama .
Alisema ni imani yake kujenga ushirikiano baina ya sekta binafsi na Serikali kwa kuhamasisha wafanyabiashara kujiunga kwenye Sacco’s na chama.
Mfinanga alielezea ,ajira bado ni changamoto duniani na Tanzania, hivyo ni muhimu kuwajengea uwezo vijana kuboresha uelewa wao katika biashara.
“Sio tu kuwaongezea upeo wa kujua biashara bali kuwapa fursa ya kujifunza kupitia kwa ambao tayari wapo kwenye mtandao wa kibiashara na uwekezaji .” aliongeza Mfinanga .