Home Mchanganyiko SERIKALI KURATIBU MPANGO MKAKATI WA KUTOKOMEZA MAUAJI YA WAZEE

SERIKALI KURATIBU MPANGO MKAKATI WA KUTOKOMEZA MAUAJI YA WAZEE

0

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari leo Juni 10,2021 jijini Dodoma wakati akitoa tamko kuelekea siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee.

……………………………………………………………………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma

KUELEKEA siku ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya wazee June 15 mwaka huu, serikali inaratibu utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kutokomeza mauaji ya wazee 2018/ 2019 – 2022/2023, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ulinzi na usalama wa wazee wasiojiweza na ambao hawana watu wa kuwatunza.

Kauli hiyo imetolewa leo June 10,2021 jijini Dodoma na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia ,Wazee na Watoto Dk.Doroth Gwajima wakati akitoa tamko kuelekea siku ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya wazee ambayo hufanyika June 15 kila mwaka,amesema kuwa serikali imeendelea kuzitambua  familia masikini wakiwemo wazee na kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi. 

Dkt.Gwajima amesema kuwa maadhimisho haya yanalenga kuelimisha jamii juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee zinazotokana na mila na desturi potovu,pamoja na fursa walizonazo na suala zima la uzee na kuzeeka.

“Siku hii inakumbusha umuhimu wa kuwatetea na kuwalinda wazee ili wawe na maisha bora na yenye matumaini wakati wanapostaafu au wanapokuwa na umri mkubwa”amesema Dkt.Gwajima

Aidha Dkt.Gwajima amesema kuwa kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya wazee ukiwemo ukatili wa kimwili,kihisia na kiuchumi basi wajue kuwa mkono wa sheria ni mrefu na ni suala la muda tu kwani watawafikia wote na sheria itachukua mkondo wake.

Amesema hao wanaofanya vitendo hivyo lazima wakumbuke hata wao watazeeka na hayo wanaowafanyia wengine na wao watafanyiwa  maana nguvu ya kuzuia mabaya inatokana na umoja wa jamii katika kuyakataa mabaya dhidi ya wengine.

Hata hivyo ameitaka jamii kuhakikisha ulinzi na usalama wa wazee wote nchini huku akiahidi Serikali kuendelea kulinda na kuwatunza wazee.

Kuhusiana na siku hiyo,Waziri Gwajima amesema inatakiwa kutumiwa kutafakari changamoto mbalimbali zinazowakumba wazee hapa nchini na kushirikiana kwa pamoja katika kuzitatua.

Waziri Gwajima amesema kwa upande wa Serikali imeendelea kuwapatia familia maskini wakiwemo Wazee kuwawezesha kupata mahitaji muhimu kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini ( Tasaf) ambapo hadi kufikia Desemba mwaka 2019,jumla ya wazee 680,056 wanaume 258,674 na wanawake 421,382 wamenufaika na mpango huo.

kaulimbiu ya siku ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya wazee inasema ‘’Tupaze Sauti Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee’’