Home Mchanganyiko CHARLES MESHACK: KILIMO CHANZO UPOTEVU MISITU

CHARLES MESHACK: KILIMO CHANZO UPOTEVU MISITU

0
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Charles Meshack akiwasilisha mada mbele ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira ya Bunge la Tanzania 
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpingo na Maendeleo (MDCI), Jasper Makala, akiwasilisha mada mbele ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira ya Bunge la Tanzania.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Aloyce Kwezi (kulia) akichangia kwenye warsha ya siku moja iliyoandaliwa na mashirika ya TFCG, MJUMITA na MCDI, mwingine ni Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira David Kihenzile.
Mkurugenzi Mkuu wa Mtandao wa Jamii na Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), Rahima Njaidi akiwasilisha mada mbele ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira ya Bunge la Tanzania .
*******************************
Na Suleiman Msuya
IMEBAINISHWA kuwa mahitaji ya ardhi kwa ajili ya mashamba ya kilimo  yanachangia upotevu wa misitu kwa asilimia 80.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG), Charles Meshack wakati akizungumza na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambao ni wajumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii jijini Dodoma.
Amesema kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanywa na TFCG na taasisi nyingine zimeonesha upotevu mkubwa wa misitu nchini unasababishwa na kilimo hasa cha zao la mahindi.
Amesema asilimia kubwa ya upotevu huo unatokea katika maeneo ambayo misitu yake haina mfumo wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ).
Meshack amesema utafiti unaonesha kuwa Tanzania ina jumla ya hekta milioni 48 za misitu ambapo asilimia 47 ya misitu hiyo ipo katika ngazi ya kijiji ambapo hekta milioni 2 pekee ndio ipo kwenye USMJ.
“Misitu nchini inapotea sana hapa nchini hasa katika vijiji ambao havina USMJ kwani kati ya hekta milioni 22 ya misitu hiyo ni hekta milioni 2 pekee ipo kwenye USMJ hivyo hekta milioni 20 zipo huru hali ambayo inachangia kilimo kuchochea upotevu kwa asilimia 80,” amesema.
Meshack amesema iwapo hakutakuwa na jitihada za kuilinda, kuitunza na kuindeleza baada ya miaka 40 ijayo misitu itakuwa imekwisha.
Mkurugenzi huyo amesema mfumo wa USMJ umeweza kuchochea uhifadhi, ulinzi na utunzaji huku maendeleo yakipatikana.
“Faida ya USMJ ni kubwa sana kuliko kujikita kwenye kilimo hivyo ni jukumu la wadau wote kushirikiana kunusuru misitu inateketea.
Ushahidi upo kuwa USMJ umeweza kuongeza thamani mazoa ya misitu nchini, lakini pia miradi ya elimu, afya, maji, uhifadhi ikifanikishwa kwa uendelevu,” amesema.
Meshack amesema iwapo Serikali inahitaji kupunguza hekta 469,000 zinazopotea kwa mwaka ni vema iwekeze kwenye USMJ kwa kuwa imeonesha mafanikio mazuri.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mpingo na Maendeleo (MCDI), Jasper Makala amesema kupitia USMJ wameweza kuilinda misitu na kukuza kipato kwa wananchi wanaozungukwa na misitu.
Amesema MCDI, imekuwa ikijijita kutoa elimu namna ya kukabiliana na moto, kuunganisha na masoko ya mazoa ya misitu na uhifadhi wa mazingira na misitu.
“Kupitia uwepo wetu tumewezesha mapato kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 baada ya kuachana na kuuza magogo.
Pia tumewezesha kuongeza ajira kwa wanavijiji wengi jambo ambalo limechochea uhifadhi zaidi,” amesema.
Makala amesema MCDI kwa kushirikiana wadau mbalimbali kama Program ya Kuongeza Mnyororo wa Thamani (FORVAC) na WWF wameweza kutoa mashine nne za Norwood ambazo zinaongeza tahamani ya mazoa ya misitu kwa asilimia 60.
“Pia tumenunua mashine ya kukausha mbao hali ambayo imezidi kuongeza kuongeza thamani kwa mazao ya misitu hasa mbao,” amesema.
Makala amesema kwa ujumla wanachofanya kwenye vijiji kwa sasa ni kuongeza wingi wa mazao na mapato.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), Rahima Njaidi amesema USMJ umegawanyika katika maeneo wawili muhimu ambayo ni vijiji na halmashauri kusimamia misitu na USMJ.
Njaidi amesema MJUMITA na wadau wengine walikuja na USMJ ili kuhakikisha rasilimali misitu inakuwa salama.
“Tumekuwa tukisimamia uhifadhi, utunzaji na uendelevu wa misitu kwa kuafuata Sheria ya Misitu ya mwaka 2002, Sera ya misitu ya mwaka 1998 pamoja na kanuni zake kuhakikisha rasilimali hiyo inanufaisha watu wote na nchi,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema USMJ ni nyenzo muhimu kwenye ulinzi wa misitu nchini.
Aidha, amesema wametambua umuhimu wa wananchi katika ulinzi wa misitu iwapo dhana ya USMJ itapewa nafasi kwa ngumu kubwa.
Naye Mbunge wa Lulindi Issa Mchungahela amesema USMJ inapaswa kusambaa nchini kote kwa kuwa inagusa maisha ya wananchi.
Mchungahela amesema miradi hiyo ni moja ya maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mbunge wa Kinondoni Askofu Josephat Gwajima amesema misitu ni muhimu kwa maisha ya binadamu hivyo inapaswa kutunzwa kwa nguvu zote.