Home Mchanganyiko TFCG, MJUMITA, MCDI  WATOA MAOMBI 7 BUNGENI

TFCG, MJUMITA, MCDI  WATOA MAOMBI 7 BUNGENI

0
Mbunge wa jimbo la Lulindi Issa Mchungahela akichangia kwenye semina ya siku moja kwa wabunge wajumbe wa Kamati za Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira iliyoandaliwa na Mashirika ya TFCG, MJUMITA na MCDI iliyofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa bungeni Dodoma.
Mbunge wa jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, Dk. Charles Kimei akichangia kwenye semina ya siku moja kwa wabunge wajumbe wa Kamati za Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira iliyoandaliwa na Mashirika ya TFCG, MJUMITA na MCDI iliyofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa bungeni Dodoma.
 …………………………………………………………..
Na Suleiman Msuya
KATIKA kuhakikisha rasilimali misitu inakuwa endelevu Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) na Shirika la Mpingo na Maendeleo  (MCDI) wametoa maombi saba kwa Bunge.
Maombi hayo yamewasilishwa bungeni na Meneja Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), Charles Leonard kwa niaba ya taasisi hizo wakati wakitoa mafunzo kwa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Leonard amesema pamoja na mafanikio ambayo yamepatikana kupitia Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) wanaomba mambo saba hayo yafanyike kwa maslahi ya nchi.
Amesema Tanzania ina hekta za misitu milioni 48.1 ambapo hekta milioni 22.1 ipo kwenye vijiji na hekta milioni 2 ndio inasimamiwa na vijiji jambo ambalo ni hatari kwa miaka 50 ijayo kwani misitu inaweza kutoweka nchini.
Meneja huyo alitaja ombi la kwanza kuwa kuangalia sera, sheria na kanuni na taratibu zinazokinzana kwenye sekta ya ardhi, misitu, kilimo, nishati na maji baadhi ya vipengele vinakwamisha usimamizi wa rasilimali misitu.
Amesema wanaamini wabunge wanaweza kusaidia kwenye kuangalia namna ya kurekebisha vipengele hivyo.
“Ombi la pili tunaomba wabunge mtoe kipaumbele kwenye kuendeleza na kuhamasisha uwekezaji katika usimamizi wa misitu ya jamii.
Pia kuhamasisha uvunaji,  usimamizi na uhifadhi endelevu wa rasilimali za misitu ya asili katika ardhi za vijiji, hali itakayochangia ongezeko la thamani la mazao ya misitu na kupeleka kwa vijiji vingine vyenye misitu,” amesema.
Meneja huyo amesema kupitia msukumo wa wabunge kwenye eneo hili wataweza kupunguza upotevu wa misitu ambapo kwa mwaka zaidi ya hekta 469,000 zinapotea.
Amesema USMJ inapunguzia kazi Serikali kwa kuwa fedha zinazopatikana zinatekeleza miradi ya maendeleo ya alimu, afya, maji na mingine mingi.
Leonard amesema ombi lingine ni kuwataka wabunge waunge mkono shughuli za USMJ kwa kuhamasisha vijiji vyenye misitu ya asili kuhifadhi, kutunza na kuendeleza kwa njia endelevu.
Meneja huyo alitaja ombi lingine kuwa ni wabunge waendelee kuishauri Serikali kuhakikisha sheria ya misitu namba 14 ya mwaka 2002 inayowapa mamlaka vijiji kumiliki, kuhifadhi na kusimamia misitu inatekelezwa bila vikwazo.
“Kuishauri Serikali kuhusu haki na wajibu kupitia sheria zilizopo ili wananchi waweze kunufaika vizuri na rasilimali misitu zilizopo kwenye vijiji.
Vilevile tunaomba muendelee kuishauri Serikali kuhusu kanuni za misitu zilizotoka mwaka 2019 kwenye tangazo la Serikali namba 417 ambazo zinaonesha kurudisha nyuma USMJ,” amesema.
Meneja alitaja ombi lingine wanalopeleka kwa wabunge ni kuwa tayari kutembelea maeneo ambayo miradi imetekelezwa ili kujionea kinachoendelea ili waweze kuthibitisha kwa vitendo yanayoelezwa.
Leonard amesema TFCG, MJUMITA na MCDI wameamua kupigania rasilimali misitu nchini ili kuhakikisha inanufaisha jamii hivyo wanaamini watunga sheria, sera na kanuni wakiwa kitu kimoja misitu inatakuwa salama na endelevu.
Akizungumza baada ya ombi hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Aloyce Kwezi amesema wamechukua maombi yote yaliyowasili na taasisi hizo na kuahidi kufanyia kazi.
Kwezi amesema TFCG, MJUMITA na MCDI wanachokifanya ni cha kuigwa na wadau wengine ili kuhakikisha rasilimali misitu inakuwa salama na endelevu.
“Ninapenda kuahidi kuwa sisi kama kamati tumechukua maombi yenu kwani yamejikita kulinda rasilimali misitu ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi,” amesema.
Amesema changamoto zilizopo watazifanyia kazi na kuomba TFCG, MJUMITA na MCDI kuendelea kushirikiana nao ili kuendeleza rasilimali misitu.
Kwa upande wake Mbunge wa Lulindi Issa Mchungahela amesema wananchi wapo tayari kuhifadhi mazingira ila changamoto ya kipato ni tatizo.
Aidha, amesema pamoja na manufaa ambayo yametajwa ni mengi ila inaonekena elimu bado haijafika kwa kiwango cha kuridhisha.
Mjumbe huyo wa Kamati ya Viwada, Biashara na ?Mazingira amesema jamii ikinapaswa kutambua faida za uhifadhi ya misitu ili kuweza kuachia urithi kwa vizazi vijavyo.
Mbunge wa Vunjo, Dk.Charles Kimei amesema jamii inaweza kulinda rasilimali misitu iwapo itanufaika nayo kiuchumi, maendeleo na jamii.
“Nadhani kuna juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha dhana ya ushirikishi inatimia kwani wanavijiji wengi waliopo pembezoni mwa misitu au hifadhi hawanufaiki nayo,” amesema.
Mbunge wa Kuteuliwa, Riziki Lulida amesema mafanikio yaliyopatikana kwenye misitu ya vijiji kupitia mashirika hayo yanapaswa kusambaa kila kona ya nchi ili kulinda misitu yote.
Amesema rasilimali misitu ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na wananchi iwapo itatumika kwa kufuata sheria, sera na kanuni zilizopo.