Home Mchanganyiko THBUB YATOA TAMKO KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI JUNI 5,2021

THBUB YATOA TAMKO KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI JUNI 5,2021

0

………………………………………………………………….

KESHO Juni 5, 2021 ni Siku ya Mazingira Duniani, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), inaungana na wadau wote ulimwenguni kuadhimisha siku hii muhimu.

Siku hii ya kimataifa ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Disemba 15, 1972 kupitia Azimio Na. A/2994 (XXVII), na ilianza kuadhimishwa rasmi Juni 5, 1974. Tangu wakati huo, kila ifikapo tarehe 5 Juni dunia imekuwa ikiadhimisha siku hii ya Mazingira. Lengo la kuwepo kwa siku hii pamoja na mambo mengine ni kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mazingira, hasa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Kimataifa maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo: “Rejesha mfumo wa ikolojia,” (“Restore Ecosystem”), lengo likiwa ni kuhimiza usafi wa mazingira, hifadhi ya usimamizi wa mazingira, udhibiti wa taka ngumu, hifadhi ya vyanzo vya maji, kilimo, ufugaji na uvuvi endelevu. Kitaifa maadhimisho haya yamebeba kauli mbiu isemayo: “Tutumie Nishati Mbadala: Kuongeza mfumo wa ikolojia.”

Tume ambayo ni Taasisi ya Kitaifa ya Haki za Binadamu na Msimamizi wa Utawala bora (Ombudsman) inatambua kuwa uharibifu wa mazingira unaathiri maisha ya viumbe, kilimo na uvuvi endelevu ambavyo ni vichocheo vya kufurahia haki ya kuishi, haki ya afya, haki ya hewa safi, haki ya maji salama, kilimo endelevu na haki za kitamaduni. Haki ya kuishi ambayo imetamkwa katika Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sura ya 2 ya Sheria za Tanzania, inategemea kila mtu kutekeleza wajibu wa kulinda maliasili za Nchi  kama ilivyotamkwa katika Ibara ya 27 (1) ya Katiba hiyo.  

Aidha, Ibara ya 24 ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na Ibara ya 11 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni pia zinaweka masharti ya kuzingatia haki ya kiwango bora cha maisha ili kuhakikisha binadamu wote duniani wanafurahia haki za kuishi, afya, kumiliki mali zilizoainishwa katika Katiba na Mikataba mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa.

Tume pia inatambua kuwa Ibara ya 27(1) ya Katiba ya Nchi inaweka wajibu kwa jamii kulinda maliasili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nchi pia imeweka mifumo ya kisheria kama: Sheria ya Ardhi ya Vijiji Sura ya 114; Sheria ya Ardhi Sura ya 113; Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Tanzania Bara Sura ya 191; na Sheria ya Misitu Sura ya 323.

Sheria nyingine zilizowekwa ili kulinda maliasili ya nchi ni: Sheria ya Uvuvi Sura ya 279; Sheria ya Hifadhi ya Wanyama Pori Sura ya 283;  Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura ya 282; Sheria ya Ulinzi na Hifadhi za Bahari Sura ya 146; Sheria ya Madini Sura ya 123; na sheria nyingine ambazo zinalinda mazingira kwa ujumla, ikiwemo ulinzi wa bioanuwai, ikolojia na duru mrishano wa viumbe hai. 

Pamoja na Baraza la Taifa la Utunzaji wa Mazingira Tanzania Bara (NEMC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA)  kupewa dhamana ya kisheria ya usimamizi wa mazingira, zipo pia taasisi nyingine kama Idara ya  Uvuvi; Tume  ya Madini; Kitengo cha Ulinzi na Hifadhi ya Bahari (MPRU); Shirika  la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Taasisi ya Hifadhi ya Wanyamapori (TANAPA).

Wadau wengine wenye dhamana ya hifadhi ya mazingira ni: Wakala wa Misitu (TFS); Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA); Wananchi na  Asasi za Kiraia (AZAKI). Taasisi na wadau hawa wote wana wajibu wa kikatiba na kisheria kuhakikisha hifadhi ya mazingira kwa uhai wa viumbe, ambavyo ni chimbuko la haki za binadamu zinazotegemeana na ambazo mwanadamu hawezi kunyang’anywa.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inapenda kuchukua fursa hii kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuweka mifumo mizuri ya kuhakikisha uhifadhi wa maliasili, ikolojia na mazingira. Pia inazipongeza taasisi na wadau wote kwa juhudi zao za kuhifadhi mazingira nchini. 

Katika hatua nyingine, Tume inazihimiza Serikali kupitia taasisi zake za uhifadhi wa  mazingira kama NEMC na ZEMA; TANAPA; TAWA; MPRU; Tume ya Madini; TFS; Taasisi nyingine za Umma zenye uhusiano na utunzaji wa Mazingira kama mamlaka za Serikali za Mitaa; AZAKI; wananchi; Jumuiya ya Kimataifa na wadau wa maendeleo kuungana na Serikali ya Tanzania na Shirika la Kimataifa la Hifadhi ya Mazingira (UNEP) kuchukua hatua zinazopaswa katika kulinda na kurejesha mfumo wa ikolojia unaotishiwa na shughuli za kibinadamu kwa ustawi na haki za wakazi wote duniani.  

Mwisho, Tume inaikaribisha jumuiya za kimataifa kutembelea Tanzania ili kushuhudia na kufurahia wanyama na ndege asili wa kuvutia, aina mbalimbali ya miti iliyotunzwa vyema, vipepeo; samaki na viumbe bahari wengine, ikiwa ni matokeo chanya ya utunzaji wa mfumo wa ikolojia na duru mrishano pamoja na bioanuwai.