Home Mchanganyiko WAUZAJI NA WASAMBAZAJI NYAVU HARAMU KIKAANGONI

WAUZAJI NA WASAMBAZAJI NYAVU HARAMU KIKAANGONI

0

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega akizungumza wakati wa mkutano na baadhi ya wakazi wa Kijiji cha
Kanyala kilichopo Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza,   na kubainisha kuwa serikali imepanga kuweka
utaratibu wa kutambua hatua mbalimbali za upatikanaji wa nyavu za uvuvi tangu
kutengenezwa kwake hadi kusambazwa na kumfikia mvuvi ili kudhibiti usambaaji wa
nyavu zisizohitajika kisheria hapa nchini. (Picha
na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

 

Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mhe. Eric
Shigongo, akizungumza wakati wa mkutano wa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega na baadhi ya wakazi (hawapo pichani) wa Kijiji cha Kanyala
kilichopo Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza, ambapo Mhe. Shigongo amekemea
vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya watendaji katika kudhibiti uvuvi
haramu. (Picha na Edward Kondela, Afisa
Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega (kulia) akiteta jambo na Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mhe. Eric
Shigongo, wakati wa mkutano na baadhi ya wakazi (hawapo pichani) wa Kijiji cha
Kanyala kilichopo Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza. Naibu Waziri Ulega amefika
katika Wilaya hiyo kwenye Halmashauri ya Buchosa kwa mwaliko wa Mbunge wa Jimbo
la Buchosa Mhe. Shigongo ili kutatua kero mbalimbali za wavuvi. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari –
Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega
(katikati), Mbunge wa Jimbo la Buchosa
Mhe. Eric Shigongo (kulia) na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya
Sengerema Mhe. Mark Makoye wakiwa kwenye boti kuelekea Kijiji cha Zilagula,
ambapo Mhe. Ulega amefanya ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo ili
kutatua kero mbalimbali za wavuvi na kuhamasisha ushirika.
(Picha
na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega akiangalia boti sita za Chama cha Ushirika wa Wavuvi Zilagula zilizotengenezwa
kwa ajili ya uvuvi wa dagaa baada ya chama hicho kupokea mkopo wa Shilingi
Milioni 100.7 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB). Naibu Waziri Ulega
ameridhishwa na maendeleo ya matumizi ya fedha za mkopo huo wakati akiwa kwenye
ziara kikazi ya siku moja wilayani Sengerema. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega (wa kwanza) akikagua na kupatiwa maelezo juu ya uwekezaji wa
vichanja vya kuanikia dagaa kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa
Wavuvi Zilagula Bw. Joram Yuda (mwenye koti jeusi) baada ya chama hicho
kupatiwa mkopo wa Shilingi Milioni 100.7 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo
(TADB). (Picha na Edward Kondela, Afisa
Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega (aliyeshika boti)) akikagua na kupatiwa maelezo juu ya
matengenezo ya boti tatu kati ya tano alizozikagua kwa ajili ya uvuvi wa samaki
aina ya sangara kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wavuvi Zilagula
Bw. Joram Yuda (mwenye suti nyeusi) baada ya chama hicho kupatiwa mkopo wa
Shilingi Milioni 100.7 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB). (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari –
Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

 

Na. Edward Kondela

Serikali imepanga kuweka utaratibu
wa kutambua hatua mbalimbali za upatikanaji wa nyavu za uvuvi tangu kutengenezwa
kwake hadi kusambazwa na kumfikia mvuvi ili kudhibiti usambaaji wa nyavu
zisizohitajika kisheria hapa nchini.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega amebainisha hayo jana (22.05.2021) wakati akizungumza na baadhi
ya wakazi wa Kijiji cha Kanyala kilichopo Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza,
akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo na kubainisha kuwa
serikali inataka suala la kuchoma nyavu lipungue au liishe kabisa.

“Tumejipanga vyema sana wavuvi
mmekuwa mkipata sintofahamu kubwa unaenda dukani kununua nyavu ya milimita nane
(8) ukija nayo huku ikipimwa inaonekana iko chini ya milimita hizo ambapo ni kinyume
na sheria na wewe kuchukuliwa hatua, sasa tutapambana na wauzaji na wasambazaji
wa nyavu hizo.”
Amesema
Mhe. Ulega

Ameongeza kuwa ili kuhakikisha nyavu
za uvuvi zinakuwa katika viwango vinavyotambulika, wizara itaweka pia utaratibu
wa kuwepo kipimo kimoja ambacho kitatambulika nchi nzima kwa kushirikiana na
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kumuokoa mvuvi asiendelee kuumizwa kwa kuarifiwa
kuwa nyavu zake ziko kinyume na sheria.

Naibu waziri huyo amewapongeza pia
wakazi wa Kijiji cha Kanyala kwa kuonesha uelewa mpana juu ya kutotumia zana
haramu kwa kushirikiana na serikali jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limepunguza shughuli
za uvuvi zisizozingatia sheria za nchi.

 

 

Kuhusu kuanzishwa kwa vyama vya
ushirika vya wavuvi Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema
serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa Rais Samia
Suluhu Hassan imepanga kuwawezesha wavuvi kupitia vyama hivyo kwa kupata mikopo
ili waweze kununua vyombo vya kisasa zaidi vya shughuli za uvuvi.

“Vikundi vya ushirika vinafanya
vizuri sana na wengine wamejitengenezea vyombo vya uvuvi, tuweke utaratibu mzuri
tusirudi nyuma nimekuja kutazama namna mnavyosonga mbele nataka kurudisha ari
ya kufanya vizuri sana, nataka nirudi tena hapa kukabidhi hundi.”
Amefafanua Mhe. Ulega

Katika kuhakikisha vyama vya
ushirika vya wavuvi vinanufaika na mikopo kupitia taasisi mbalimbali za kifedha
ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Naibu Waziri Ulega amevitaka
vyama ambavyo tayari vimepatiwa mikopo kufanya marejesho kwa wakati ili viweze
kuwa na sifa ya kukopeshwa tena pamoja na kuwezesha vyama vingine kupata mikopo
na kukuza sekta ya uvuvi.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la
Buchosa Mhe. Eric Shigongo akizungumza katika mkutano huo ameipongeza Wizara ya
Mifugo na Uvuvi namna inavyohakikisha inasimamia maslahi ya wavuvi na kuiomba
kuhakikisha inadhibiti nyavu za uvuvi zisizotakiwa kisheria kabla hazijafika
kwa wavuvi, kwa kukagua nyavu kwa watu au makampuni yaliyopewa vibali vya
kuingiza nyavu hizo nchini.

Aidha, amesema serikali haiko tayari
kukandamiza raia wake wakiwemo wavuvi na kukemea vitendo vya rushwa vinavyofanywa
na baadhi ya watendaji wakati wa ukaguzi wa nyavu za uvuvi kwa wavuvi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Sengerema
Mhe. Emmanuel Kipole amekemea pia vitendo vya rushwa na kuwataka wavuvi
wasikubali kutoa rushwa kwa mtendaji yeyote wa serikali kwani kwa kufanya hivyo
wanakuwa wanahalalisha kuendelea kuwepo kwa vitendo hivyo.

Amewataka watendaji wanaohusika na ukamataji
wa zana za uvuvi zisizotakiwa kisheria kufuata sheria za nchi kwa kuwa vitendo vya
rushwa vinabomoa nchi na kusababisha kutokuwepo kwa mahusiano mazuri baina ya
watendaji hao na wavuvi.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha
Kanyala wakizungumza katika mkutano wa Naibu Waziri Ulega, wamelalamikia baadhi
ya vyama vya ushirika vya wavuvi kukosa mikopo kutoka taasisi mbalimbali za
kifedha licha ya kufuata taratibu ambazo zimekuwa zikianishwa na taasisi hizo, jambo
ambalo Mhe. Ulega alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Mkurugenzi Mtendaji
wa TADB Bw. Japhet Justine katika mkutano huo juu ya jambo hilo ambapo
mkurugenzi huyo aliahidi kulifanyia kazi.

Wakazi hao pia wameiomba serikali
kutokomeza kabisa uwepo wa nyavu haramu ili waweze kununua nyavu zinazotakiwa
kisheria kwa kuwa wamekuwa wakipata hasara kwa kununua nyavu zisizotakiwa
kisheria bila kufahamu na hatimaye kukamatwa kwa nyavu hizo na kuchomwa moto
jambo ambalo limekuwa likiwarudisha nyuma kimaendeleo.

Akiwa katika Wilaya ya Sengerema, Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiambatana na Mbunge wa Jimbo la
Buchosa Mhe. Eric Shigongo na mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Emmanuel Kipole pamoja
na viongozi wengine, amefika katika Kijiji cha Zilagula na kukutana na Chama
cha Ushirika wa Wavuvi Zilagula na kujionea namna mkopo wa Shilingi Milioni
100.7 waliopatiwa na TADB wanavyoutumia kwa kutengeneza boti za uvuvi, vichanja
vya kuanikia dagaa, kujenga eneo la kuhifadhia samaki pamoja na kujulishwa
mikakati mbalimbali ambayo chama hicho kitaendelea kufanya kupitia fedha hizo.

Akiongea na wakazi wa Kijiji cha
Zilagula Mhe. Ulega amekitaka Chama cha Ushirika wa Wavuvi Zilagula kuwasaidia
vijana na kutaka wataalam kufikishwa katika kijiji hicho ili kutoa elimu ya
matumizi bora ya fedha za mikopo ili mkopo huo uweze kuwa na tija zaidi kwao na
jamii inayowazunguka.

Amekitaka chama hicho kufanya kazi
vizuri zaidi ili siku zijazo waweze kununua boti za kisasa zaidi za uvuvi na
kuwataka wakazi wa Kijiji cha Zilagula kuunga mkono uwepo wa Chama cha Ushirika
wa Wavuvi Zilagula.

Ameongeza kuwa kupitia chama hicho wavuvi
wataweza kuuza samaki kwa bei nzuri zaidi badala ya kulanguliwa na watu
wachache ambao wamekuwa wakinunua samaki kwa bei ndogo zaidi na wenyewe kwenda
kuuza kwa bei kubwa katika masoko mengine.