Home Mchanganyiko MHE.JAFO-UOTO WA ASILI WA MLIMA KILIMANJARO UNAPASWA KULINDWA

MHE.JAFO-UOTO WA ASILI WA MLIMA KILIMANJARO UNAPASWA KULINDWA

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua dampo la Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro alipofanya ziara ya kikazi leo Mei 22, 2021.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akisikiliza maelezo kutoka kwa mtaalamu wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua dampo la kisasa la Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro alipofanya ziara ya kikazi leo Mei 22, 2021.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo (kulia) akizungumza na Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro Mhe. Stephen Kigaigai wakati alipofika ofisini kwake kabla ya kuanza ziara katika dampo la kisasa la Manispaa ya Moshi leo Mei 22, 2021

Muonekano wa dampo la kisasa la Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro ambalo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo alilikagua na kuridhishwa na namna wanavyohifadhi taka ngumu zinazo zalishwa kila siku katika Manispaa hiyo. 

***********************

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amesisitiza kwamba uoto wa asili wa Mlima Kilimanjaro unapaswa kulindwa ili kuufanya uendelee kuwa kivutio kwa watalii wengi wanaokuja hapa nchini. 

Jafo ametoa msisitizo huo wakati wa kikao kifupi na Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro Mhe. Stephen Kigaigai katika ziara yake ya kikazi mkoani hum oleo Mei 22, 2021 kwa ajili ya kukagua uzingatiaji wa hifadhi ya mazingira.

Alisisitiza kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) inaendelea kusimamia uhifadhi wa mazingira hapa nchini kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Kigaigai amemuhakikishia Waziri Jafo kwamba atahakikisha juhudi za Serikali za kulinda mazingira anazisimamia ipasavyo katika mkoa wake.

Katika ziara hiyo Waziri Jafo alitembelea dampo la kisasa katika Manispaa ya Moshi ambapo aliwapongeza viongozi na watendaji wa manispaa hiyo kwa namna wanavyohifadhi taka ngumu zinazozalishwa kila siku katika Manispaa hiyo.  

Akikagua shughuli zinazofanyika katika dampo hilo, waziri huyo alifurahishwa na namna wataalamu wanavyosimamia vyema utupaji wa taka hizo sambamba na ubadilishaji wa baadhi ya taka hizo kuwa mboji.

Kutokana na hali hiyo alizitaka Halmashauri nyingine hapa nchini kuiga mfano wa Manispaa hiyo ya Moshi katika uhifadhi bora wa taka ngumu.

Aidha, pamoja na ukaguzi wa dampo hilo alifanikiwa kutembelea kiwanda cha China Paper Industry ambapo aliwataka wamiliki wa kiwanda hicho kutafuta njia ya kutumia nishati mbadala kwani kwasasa wanatumia magogo mengi kwa ajili ya nishati na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Hivyo Waziri Jafo amewapa mwaka mmoja wamiliki wa kiwanda hicho kuja na njia nyingine ya nishati mbadala wa magogo yanayotumika sasa ili kuepusha ukataji wa miti ovyo. 

Pia waziri huyo amewataka wamiliki wa kiwanda cha kutengeneza nondo cha Five Star Steel kinachotumia chuma chakavu kuepuka kununua vyuma vinavyotoka katika miundombinu ya umma ikiwemo madaraja, alama za barabarani na kutoka kwa watu binafsi ili kutoleta hasara kwa jamii.

Hata hivyo, Jafo amekipongeza kiwanda hicho kwa kudhibiti kusambaa kwa moshi katika kiwanda hicho ambapo kwa siku za hivi karibuni umekuwa ni kero kwa raia wanaoishi jirani ya kiwanda hicho.