Home Mchanganyiko MBUNGE MTENGA AWAPA POLE WANANCHI WA JIMBO LA KONDE

MBUNGE MTENGA AWAPA POLE WANANCHI WA JIMBO LA KONDE

0
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MBUNGE wa Jimbo la Mtwara Mjini, Hassan Mtenga amewapa pole wanafamilia, wananchi wa Jimbo la Konde kisiwani Pemba,wabunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Chama cha ACT Wazalendo kutokana na kifo cha Mbunge wao, Khatib Said Haji (ACT Wazalendo) kilichotokea jana na maziko yake kufanyika siku hiyo hiyo kisiwani humo.

Ameyasema hayo muda mfupi baada ya taarifa ya kifo cha mheshimiwa Haji kutangazwa bungeni jijini Dodoma Mei 20, 2021 na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Tulia Ackson.
Kifo cha mbunge huyo kilitokea jana alfajiri katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ambapo hivi karibuni hakuweza hakuhudhuria vikao vya Bunge kutokana na kuumwa.
Mheshimiwa Mtenga amesema kuwa, kifo hicho kimekuwa cha huzuni kubwa kwani alikuwa mtu wa watu na alikuwa mcheshi mwenye utani mwingi hali ambayo ilimfanya kuwa na marafiki wengi kwa muda mfupi waliokutana nae bungeni.
‘’Namfahamu vyema ni mbunge ambaye alikuwa na mahusiano mazuri na watu ndani na nje ya Bunge, alikuwa mcheshi mwenye utani na ndani ya bunge alikuwa ni mtetezi mzuri wa chama na mtu wa msimamo,’’amesema Mbunge Mtenga.
Amesema kuwa,amesikitika sana kutokana na kifo hicho na imekuwa ni kilio kwa wabunge wote kwani pia alikuwa kati ya wabunge ambao hajafungamana na chama chochote.
“Marehemu wakati wa uhai wake alikuwa ni kiongozi kwenye jamii kwani alikuwa haegemei upande wowote huku akitoa hoja za mashiko kwa maslahi ya nchi yetu na kuwatetea watu mbalimbali katika jamii,”ameongeza Mtenga