Home Mchanganyiko WATOT WAMFUKUZA MAMA YAO ILI WARITHI MALI ALIZOACHA BABA YAO

WATOT WAMFUKUZA MAMA YAO ILI WARITHI MALI ALIZOACHA BABA YAO

0

…………………………………………………………………………………….

Mali iliyochumwa na wanandoa wawili (matrimonial property) mmoja akifa umiliki unahamia kwa mwanandoa aliyebaki, na watoto hawana haki ya kugawana wala kudai chochote kwa kuwa sheria haiwatambui watoto isipokua kama wazazi wameamua kuwagawia watoto.

Hayo yamesemwa na Afisa Mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa ambaye Kitaaluma  ni mwanasheria Bw. Philoteus J. komba wakati akisuluhisha mgogoro wa Mjane Mariam Gama aliyefukuzwa na mwanae Feruzi Miteo ili arithi ardhi ya marehemu baba yake,  katika Ofisi ya  Kijiji cha Mango Kata ya Kihagara Wilayani Nyasa.

Afisa ardhi huyo amefafanua kuwa, sheria haiwatambui watoto katika mali za wanandoa hivyo mwanandoa mmoja akifariki umiliki wa mali unahamia kwa mwanandoa aliyebaki na hatakiwi kubugudhiwa, kwa kuwa sheria inamtambua kuwa ni mmiliki halali na watoto watakuwa na uhalali ikiwa wazazi wote wawili wamefariki.

Aidha amemtaka Kijana huyo Ferudhi Miteo  kuacha mara moja kumnyanyasa  na kumfukuza mama yake katika maeneo yake kwa kuwa ni mmiliki halali na Sheria inamtambua. Amewaelekeza Viongozi wa Vijiji kumchukulia hatua za kisheria mara moja endapo akiendelea na tabia ya kumnyanyasa mjane huyo. 

Awali mjane Mariam Gama (70) aliwasilisha malalamiko kwa Kamishina wa Ardhi Msaidizi  Mkoa wa Ruvuma  naye akatoa maelekezo kwa Afisa Mteule wa Wilaya ya Nyasa  kutatua mgogoro huo wa kifamilia ambao mtoto alikuwa akimtaka mama yake kuondoka mara moja katika ardhi ya marehemu baba yake, kwa kuwa aliyemleta hapo amekwisha fariki dunia yeye anasubiri nini kuondoka katika maeneo ya baba yake.

Aidha alivitaja vitendo anavyofanyiwa na mwanae ni kuzuiliwa kulima mashamba aliyoachiwa na marehemu mume wake,kushambuliwa kwa lugha za matusi zilizomsababishia kuugua na kufukuzwa katika nyumba anayoishi, licha ya kuwepo wosia wa kimaandishi aliouacha marehemu mumewe wa kuwagawia kila mtoto eneo lake.

Mara baada ya kumuuliza mwanae Ferudhi Miteo amekiri kutenda vitendo hivyo kwa kuwa naye ana haki ya kumiliki ardhi ya Marehemu baba yake, na anaifahamu thamani ya ardhi, hivyo anafanya kila linalowezekana kumwondoa mama yao, ili aweze kumiliki ardhi hiyo ya baba yake, licha ya kuwa, wosia huu upo katika Ofisi ya Kijiji cha Mango na akakiri yeye binafsi anao.

Kwa upande wao Viongozi wa Vijiji ambao ni Telesphor Ndunguru wa kijiji cha Mango na Abeli lukuwi wa kijiji cha Songambele, wamekiri uwepo wa mgogoro huo na hawakujua sheria inasemaje kuhusu mali ya wanandoa, hivyo wamempongeza Afisa ardhi wa Wilaya ya Nyasa kuja kutatua mgogoro huo na kuahidi kuhakikisha kuwa kuanzia leo hakuna mjane atakayenyanyaswa katika Kijiji hicho na kumtaka Afisa huyo kutoa Elimu ya Sheria katika Mikutano ya Hadhara mara kwa mara ili kutatua migogoro ya ardhi pamoja na mirathi.

“Afisa ardhi Tunakushukuru sana kwa kutupa elimu hii kwa kweli tunakuomba siku nyingine uje, kwani unyanyasaji huu unafanyika kwa wajane wengi, hivyo elimu hii ikitolewa kwa watoto wetu itasaidia kupunguza manyanyaso kwa wajane, kwa kuwa tunafahamu haya yanatokea kwa kutokujua sheria”.