Home Mchanganyiko WATANZANIA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA ZINAZOPATIKANA SADC

WATANZANIA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA ZINAZOPATIKANA SADC

0

Watanzania wamehimizwa
kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatina kwenye mtangamano wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwemo biashara, uwekezaji na soko la
bidhaa mbalimbali za Tanzania ili kunufaika na Jumuiya hiyo.

Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe
wakati akifungua rasmi Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya Jumuiya ya
Maendeleo Kusini  mwa Afrika (SADC)  lililofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)
na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.

Mhe. Prof. Mwamfupe amesema
kwamba, katika kipindi cha miaka 40 tangu kuanzishwa kwa SADC mwezi Aprili  1980, wigo wa fursa umeongezeka ambapo sasa
Jumuiya imejikita katika kuwanufaisha  wananchi wake kiuchumi baada ya kukamilisha jukumu
la kuzikomboa kisiasa  Nchi za Kusini mwa
Afrika ambalo lilikuwa moja ya lengo la kuanzishwa kwa Jumuiya ya SADC.

Kadhalika alisema kuwa maadhimisho
ya miaka 40 ambayo yamebeba kaulimbiu isemayo “Miaka 40 SADC ya Kuimarisha
Amani na Usalama, Kuhamasisha Maendeleo na Ustahimilivu wa Changamoto
Zinazoikabili Dunia” yanalenga pamoja na mambo mengine kuenzi mchango wa
waaanzilishi wa SADC, lakini pia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu Mtangamano
wa SADC na faida za uanachama wa Tanzania kwenye Jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja
na kuwaeleza wananchi fursa zinazopatikana za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Pia aliongeza kuwa,
maadhimisho haya yanalenga kuangazia mafanikio yaliyofikiwa pamoja na kuongeza
hamasa kwa makundi mbalimbali kama vile wafanyabiashara, vijana, wanawake,
makundi maalum na wananchi kwa ujumla kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii
zinazopatikana SADC.

“Leo tunaposherehekea miaka
40 ya SADC tunafungua wigo kwa wadau mbalimbali hususan wafanyabiasha na vijana
kuwaonesha namna gani wanaweza kunufaika na Jumuiya hiyo kutoka ile ya
kufundishwa darasani hadi SADC inayotuwezesha kupanga mipango yetu ya maendeleo
kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, vijana na makundi
mengine. Hivyo tuna kazi kubwa moja ya kuhakikisha elimu kuhusu fursa
zinazopatikana SADC inawafikia wananchi wote” alisema Prof. Mwamfupe.

Awali akizungumza kuwakaribisha
Washiriki wa Kongamano hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof.
Faustine Bee alisema anashukuru Chuo hicho kuwa sehemu ya maadhimisho ya miaka
40 ya SADC kwani ni heshima kubwa kwao ambayo imewezesha wadau mbalimbali kukutana
na kubadilisha mawazo ya namna ya kuiimarisha Jumuiya hiyo.

Aliongeza kusema kwamba,
wakati Nchi Wanachama wa SADC zikiadhimisha miaka 40 ya Jumuiya hiyo, Chuo
hicho kinatambua faida za SADC kwani tayari kinashirikiana na Nchi za Jumuiya
hiyo ambapo Tanzania kwa sasa inapokea wanafunzi kupitia ushirikiano huo.
Alisema mfano mzuri ni ule uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji ambazo tayari
zinashirikiana katika kubadilishana wanafunzi kupitia utaratibu wa TAMOSE
(Tanzania –Mozambique Students Exchange Program) ambapo tayari wanafunzi kutoka
Msumbiji wanasoma UDOM na Vyuo vingine hapa nchini na vivyo hivyo wapo
wanafunzi kutoka Tanzania wanaosoma nchini Msumbiji.

Kadhalika alisema, Chuo
hicho ambacho kinapokea wanafunzi kutoka Nchi zingine za SADC kama Comoro,
Afrika Kusini, Zambia, Malawi, DRC na zingine kimejiwekea malengo ya kuingia kwenye
vyuo bora 20 katika Afrika kufikia mwaka 2030. Alisisitiza kuwa, lengo hilo
litafanikiwa endapo Chuo kitapokea wanafunzi wengi kutoka nje ya nchi ikiwa ni
moja ya kigezo  cha kupima ubora wa chuo na
alitoa ombi kwa Serikali kukisaidia Chuo hicho kuongeza wanafunzi kupitia
ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi zingine na ule wa kikanda na
kimataifa.

Wakati wa Kongamano hilo, ambalo
limeandaliwa kwa uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa ikiwemo “Kuimarisha Amani na Usalama katika Kukabiliana
na Changamoto za Ulimwengu
” iliyowasilishwa na Mkuu wa Chuo cha Diplomasia
Mstaafu, Dkt. Mohammed  Maundi na mada isemayo          “Kuhamasisha Maendeleo
na Uhimilivu katika kukabiliana na Changamoto za Ulimwengu
” ambayo
iliwasilishwa na  Mhadhiri na Mkuu wa
Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Ajali
Mustafa.

Viongozi wengine
walioshiriki Kongamano hilo ni Mkuu wa Chuo cha Mipango, Prof. Hozen Mayaya, Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa
cha Hombolo, Dkt. Michael Msendekwa,
 Naibu
Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma anayeshughulikia Taaluma, Prof. Alexander
Makulilo na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda kutoka Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Agnes Kayola. Pia,
kongamano lilihudhuriwa na Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu
cha Mipango na Chuo cha Serikali za Mitaa kilichopo Hombolo jijini Dodoma.

Mgeni Rasmi ambaye ni Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe akifungua rasmi Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) hivi karibuni. Kongamano hilo ambalo liliandaliwa chini ya uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki lilihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi kutoka UDOM na Vyuo vingine vya Dodoma. 

Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma (UDOM), Prof. Faustine Bee akiwakaribisha Washiriki wa Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC Chuoni hapo

Mkuu wa Chuo cha Diplomasia Mstaafu, Dkt. Mohammed Maundi akiwasilisha mada kwa Washiriki kuhusu Kuimarisha Amani na Usalama katika Kukabiliana na Changamoto za Ulimwengu wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC lilifanyika UDOM

Mhadhiri Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Ajali Mustafa nae akiwasilisha mada kuhusu Kuhamasisha Maendeleo na Uhimilivu katika Kukabiliana na Changamoto za Ulimwengu wakati wa Kongamano la kuadhimisha miaka 40 ya SADC.

Sehemu ya Washiriki waliohuria Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bibi Agnes Kayola, Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo, Dkt. Michael Msendekwa  na Mkuu wa Chuo cha Mipango, Prof. Hozen Mayaya 

Sehemu nyingine ya Washiriki wa Kongamano

Washiriki wa Kongamno wakiwemo wahadhiri wakifuatialia uwasilishwaji wa mada mbalimbali

Sehemu ya Wanafunzi wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC

Sehemu nyingine ya Washiriki

Washiriki wa Kongamano la maadhimisho ya miaka 40 ya SADC kama wanavyoonekana pichani

Sehemu nyingine ya washiriki

Waandishi wa Habari wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC

Washiriki kama wanavyoonekana pichani

 

Mmoja wa Wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma akichangia jambao wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC

Mmoja wa Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma akiuliza swali wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC

 

Mwanafunzi kutoka Chuo cha Mipango nae akichangia jambo wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC

Picha ya pamoja

Meza Kuu katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali