Home Mchanganyiko MAADHIMISHO YA SIKU YA SHINIKIZO LA JUU LA DAMU DUNIANI TAREHE 17/5/2021

MAADHIMISHO YA SIKU YA SHINIKIZO LA JUU LA DAMU DUNIANI TAREHE 17/5/2021

0

**************************

Tarehe 17/5/2021 ni siku ya kuadhimisha siku ya Shinikizo la juu la Damu Duniani. Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya ya Ubungo katika kuadhimisha siku hii tutafanya upimaji wa magonjwa ya Moyo bila malipo kwa wananchi wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake katika viwanja vya ofisi ya mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo iliyopo Mbezi Luis eneo la Luguluni.

Upimaji huo utaenda sambamba na utoaji wa elimu ya lishe na afya bora kwa mwili wako. Ripoti ya shirika la afya duniani (WHO) linaonyesha kila kina mama wanne mmoja anatatizo hili (1:4) na kila kina baba watano mmoja ana tatizo hili (1:5). Taarifa inandelea kwa kusema zaidi ya watu billioni moja duniani (Tanzania ikiwemo) wana tatizo hili.

Ugonjwa wa Shinikizo la juu la damu (High Blood Pressure) hutokea wakati nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa ya damu kuwa kubwa kuliko kawaida. Ongezeko hilo husababisha moyo kufanya kazi kwa nguvu zaidi ili kusukuma damu katika mishipa hiyo iliyobana (narrow/vasocontricted).

Hatari kubwa zaidi ugonjwa huu hauna dalili maalum (no specific symptoms), ila linapo dumu kwa muda mrefu bila tiba lina madhara makubwa kiafya (uharibu viungo vingi mwilini). Hii ni moja ya sababu Taasisi yetu tukishikiana na uongozi wa wilaya ya Ubungo siku hiyo ya tarehe 17 Mei, 2021 tunafanya upimaji wa afya yako mwananchi ikiwamo urefu, uzito, shinikizo la damu (BP), sukari na kupewa ushauri nasaha wa afya yako. Upimaji huu utahusisha watu wote watoto na watu wazima. Kwa wale watakaokutwa na matatizo ya moyo watafanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu siku hiyo hiyo au kupewa rufaa kuja kutibiwa kwenye Taasisi yetu (JKCI).

Visababishi 

Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu unaweza kuwa wa kurithi (historia ya ugonjwa katika familia yako) au uliosababishwa na magonjwa mengine mbalimbali kama figo, kisukari nk. Asilimia kubwa (95%) ya wagonjwa wa shinikizo la juu la damu hawana sababu inayoweza kujulikana kisayansi unknown cause/idiopathic). Matatizo mengine ambayo pia yanahusishwa na ugonjwa huu ni uzito mkubwa kupindukia, matumizi ya chumvi nyingi, kutofanya mazoezi, uvutaji wa sigara, ulaji wa vyakula vyenye mafuta au wanga mwingi, umri mkubwa, msongo wa mawazo, kinamama wakati wa ujauzito (hili mara nyingi hupona mara baada ya kujifungua).

Madhara 

Ugonjwa huu unaweza kusababisha athari nyingi mwilini kama vile kiharusi (stroke), mshtuko mkubwa wa moyo (heart attack), nguvu ya moyo kupungua (heart failure), moyo kuwa mkubwa (dilated cardiomyopathy), ugonjwa wa figo (kidney failure, kupunguza nguvu za kiume (erectile dysfunction), kupunguza hamu ya tendo la ndoa kwa kinamama (reduced libido).

Kinga 

Haya yote unaweza kuepuka kwa kinga kama vile kufanya mazoezi, kuzingatia lishe bora kwa kula matunda, mboga mboga, vyakula vyenye madini ya potassium vile vile kupunguza kula vyakula vyenye kiasi kikubwa cha mafuta, wanga na chumvi, kuepuka uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri, kutambua kiwango cha sukari katika mwili wako, kupima afya yako kila mwaka angalau mara moja.

Kama Taasisi tutahakikisha tunaendelea kutoa huduma bora zaidi za magonjwa haya ya moyo kwa wananchi kwa kutoa elimu kwa jamii ambayo itawasaidia kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusiana na magonjwa haya ambayo ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza na yanaepukika kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.

Tunawaomba wananchi muadhimishe siku hii kwa kujitokeza kwa wingi kupima afya zenu.

Kauli mbiu: Pima Shinikizo la damu; Ishi maisha marefu