Home Mchanganyiko DC MTATIRO AFUTURISHA MAKUNDI MBALIMBALI YA WANANCHI

DC MTATIRO AFUTURISHA MAKUNDI MBALIMBALI YA WANANCHI

0

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro, akiwaongoza waumini wa dini ya kiislam na  baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo kupata futari jana katika viwanja vya Ikulu ndogo iliyoandaliwa na ofisi ya Mkuu wa wilaya ambapo makundi mbalimbali yalishiriki katika hafla hiyo.

Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Tunduru wakipata futari jana iliyoandaliwa na ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo  katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan  kabla ya waumini wa Dini ya Kiislam kumaliza mfungo wa Ramadhan.

Picha na Muhidin Amri

************************

 Na Muhidin Amri,
Tunduru

MKUU wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro, amefuturisha makundi mbalimbali ya Wananchi  wa wilaya hiyo na kutoa wito kwa jamii kuendeleza mshikamano na mahusiano mema bila kujali itikadi zao za Dini.

Mtatiro, amewashukuru wananchi  walioitikia wito huo na kujitokeza katika hafla hiyo ya futari ambayo ni sehemu ya ibada muhimu  kwa waumini wa dini ya Kiislam katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha watumishi wa umma kujikita kutatua kero mbalimbali za wananchi,  badala ya kufanya kazi kwa maslahi binafsi kwani tabia hiyo imechangia sana kuongezeka kwa malalamiko na migogoro isio ya lazima katika maeneo mbalimbali.

Alisema, nafasi  walizonazo zinapita na wakumbuke kuna watumishi na viongozi wengine waliowahi kushika nafasi hizo,kwa hiyo ni vyema wahakikishe wanatoa haki na huduma nzuri kwa wananchi wanaofika kwenye maeneo yao ya kazi.

“natoa wito kwa viongozi na watendaji wengine wa serikali,shughulikieni haraka matatizo yanayoletwa na wananchi katika ofisi zenu,hakuna sababu ya kuchelewa kutoa  majibu na huduma bora, kwa sababu sasa hivi Dunia ni kama kijiji na kutambua kwamba nafasi walizo nazo ni  za muda mfupi sana”alisema Mtatiro.

Kwa mujibu wake, anachukizwa  na tabia ya baadhi ya watendaji na viongozi wanaochelewa kutoa majibu ya kero za wananchi kwa makusudi na kusisitiza kuwa,ni wajibu wao kusikiliza na kutoa majibu ya kero na changamoto  zilizopo kwenye jamii.

Alisema, bado jamii ya wana Tunduru ina wajibu wa kujenga umoja na mshikamano ili kudumisha amani kama walivyofanya viongozi na wananchi waliotangulia  ambao walijitolea  kwa hali na mali kutetea maslahi ya nchi yetu bila kujali tofauti zao za kidini na ukabila.

Aidha,amewapongeza wafanyabishara wa bidhaa  hasa  chakula kwa kufuata maagizo ya serikali kwa kutopandisha bei ya bidhaa wakati wote wa Mwezi wa Ramadhani.

Amewataka kuendelea kuwa waaminifu kwa kuuza  bidhaa zao kwa bei ya kawaida ambayo wananchi wengi wataendelea kumudu  na kujiepusha  na tamaa ambayo itapelekea wananchi wa kipato cha chini kushindwa kupata mahitaji yao.

Kwa upande wake Katibu wa Baraza kuu la Waislam(Bakwata)wilayani humo Zuber Mnandi amempongeza Mkuu wa wilaya kwa kuandaa futari katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambayo mbali na kuwakutanisha waumini wa Dini mbalimbali imesaidia kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwao.

Imamu wa msikiti wa Taqwa Shekhe Ibrahim, Maulidi amewaasa Waislam kuendelea kutenda mambo mema  sio katika Mwezi wa Ramadhani tu, bali wakati wote wa  maisha yao ili kupata baraka za Mwenyezimungu.

Amewataka wananchi wa Tunduru  kufanya kazi kwa bidii na kuacha tabia ya kulalamika,  kwani  inarudisha nyuma wilaya yao licha ya kubarikiwa  kuwa na rasilimali nyingi ambazo kama zitatumika vizuri wilaya hiyo itapiga hatua kubwa ya maendeleo.

Amewaomba Watanzania kuendelea kuishi kwa kuheshimiana na mshikamano  ili nchi yetu iendelea  kuwa na amani na utulivu ulioachwa na Waasisi wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume.

Kwa upande wake mchungaji wa kanisa la Angliana ambaye ni makamu mwenyekiti wa umoja wa Makanisa wilaya ya Tunduru Charles Said,amewapongeza waumini wa Dini ya Kiislam kwa kutekeleza moja kati ya nguzo muhimu ya Dini yao na kuwaomba waendee kumcha  Mwenyezimung hata baada ya kumalizika kwa mfungo wa Ramadhani.

Alisema, umoja wa makanisa  utaendelea kushirikiana na waislam katika mambo mbalimbali  ya maendeleo ikiwemo suala la kudumisha amani,umoja na mshikamano.