Home Mchanganyiko SHIRIKA LA RECODA LAJA NA MFUMO MPYA WA RIPAT UTAKAOINUA WAKULIMA WADOGO...

SHIRIKA LA RECODA LAJA NA MFUMO MPYA WA RIPAT UTAKAOINUA WAKULIMA WADOGO NCHINI

0

*************************

Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na utafiti, ushauri wa kitaalamu na miradi ya maendeleo na jamii la RECODA (Research Community and Organizational Development Associates) limetengeneza mfumo mpya wa ugani wa RIPAT (Rural Initiative for Participatory Agriculture Transformation –yaani Jitihada Shirikishi za Kuleta Mageuzi ya Kilimo Vijijini) utakaosaidia kuongeza kipato na uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa wakulima wadogo nchini.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la RECODA, Dkt. Dominic Ringo alipofanya semina na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji jijini Dodoma jana.

“Tunatoa mafunzo yanayolenga kuwezesha maendeleo ya jamii ya wakulima wadogo ili wafanye kilimo chenye tija kupitia kuongeza uzalishaji na matumizi ya mnyororo wa thamani unaotokana na jamii kuwezeshwa kutumia rasilimali na fursa zilizopo” amefafanua Dkt. Ringo.

Ameongeza kuwa mfumo huo una sifa kuu nne zinazoufanya ufanikiwe ambapo sehemu ya kwanza ni kapu la uchaguzi ambapo mkulima anafanya uchaguzi wa aina ya mazao au ufugaji anaoutaka, sehemu ya pili ni vikundi imara vya wakulima vinavyowezesha wakulima kupata ujuzi wa masuala ya kilimo.

Sifa nyingine alizotaja za mfumo huo ni wakulima kuendelea kufanya kazi kwa pamoja hata baada ya mradi kuisha, na sifa ya nne ni uwepo wa mwongozo wa hatua za namna taasisi inavyoweza kufanya kazi na wakulima wadogo.

Aidha, amesema matokeo ya tafiti ya matumizi ya mradi huo yameonesha matokeo chanya.

“Matokeo ya utekelezaji wa mradi huu yalionyesha kuongezeka kwa uhakika wa chakula na kipato, uboreshwaji wa lishe hasa kwa watoto na wazee, kuenea kwa teknolojia, mfumo kuwa sehemu ya mitaala ya chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo na kuanzishwa kwa vikundi vya wakulima ambavyo baadae vinakuwa taasisi za kijamii” amesema Dkt. Ringo.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Dkt. Christine Ishengoma amelipongeza Shirika la RECODA kwa kuleta mfumo huo utakaosaidia wakulima nchini.

“Ni mfumo mzuri kwa kweli tutahakikisha tunaufikisha kwa Waziri wa Kilimo kisha tutautetea bungeni ili uweze kutumika rasmi kusaidia wakulima kutoka kwenye umaskini na nia na madhumuni yetu ni kufanya uzalishaji wenye tija” Dkt. Ishengoma amesema.

Mradi wa RIPAT unatekelezwa na Shirika la RECODA kwa kushirikiana Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) na ulianza rasmi mwaka 2006 na mpaka sasa una miradi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero (vijiji 10) na Morogoro (kata 5).