Home Michezo KMC FC KUSHUKA KWA MAJALIWA DHIDI YA NAMUNGO KESHO

KMC FC KUSHUKA KWA MAJALIWA DHIDI YA NAMUNGO KESHO

0

Kikosi cha KMC FC kesho kitashuka katika Dimba la Majaliwa Ruangwa mkoani Lindi kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu soka Tanzania bara dhidi ya Namungo, utakaochezwa saa 16:00 jioni huku Kocha msaidizi wa Kikosi hicho Habibu Kondo akisema kuwa maandalizi ya mchezo huo yamekamilika kwa asilimia kubwa.

Habibu ameeleza kuwa kikosi chake kipo vizuri kuelekea katika mtanange huo na kwamba anaiheshimu Timu ya Namungo kutokana na kuwa bora na kwamba yupo tayari kupambania alama tatu katika mchezo wa kesho.

KMC FC ambao ni wageni dhidi ya Namungo, imekuwa namuendelezo mzuri wa michezo wa Ligi Kuu soka Tanzania bara ambapo Habibu amesema kuwa anafahamu mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na kwamba kila mmoja anahitaji kupata alama tatu.

“Tumekuja kwenye mchezo ambao kimsingi unaushindani mkubwa, ukizingatia tupo ugenini ,lakini kikubwa ni kwamba tumejiandaa vizuri na tuko hapa kupambania alama tatu ambazo hata wapinzani wetu nao wanazihitaji” amesema Habibu.

Habibu ameongeza kuwa “ sina hofu na wachezaji wangu, kwasababu wanamorali nzuri kuelekea kwenye mchezo wa kesho, lakini pia kila mmoja anakumbuka katika msimu uliopita hatukupata matokeo mazuri kwenye uwanja huu, hivyo tumekuja kufuta makosa hayo na hivyo tunahitaji kufanya vizuri hapo kesho.

Hata hivyo KMC FC katika mchezo ambao walikutana na Namungo kwenye uwanja wa Uhuru ,Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni iliibuka na ushindi wa magoli matatu kwa sifuri mchezo ambao ulikuwa ni Kiporo katika duru la kwanza.