……………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Serikali inahitaji zaidi ya Shilingi Trilioni nane kwa ajili ya kusambaza miundombinu ya umeme katika vitongoji ambavyo havina umeme.
Hayo yamesemwa leo Mei 7,2021 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Bodi ya REA Wakili Juliusi Kalolo,wakati wa Mkutano wa pamoja baina ya Wakala wa Nishati Vijijini REA na Wafadhili wa mradi huo kutoka Norway, EDPG wenye lengo la kuangalia maendeleo ya miradi inayotekelezwa na Wakala huyo nchini.
Wakili Kalolo amesema kuwa kazi ya kusambaza miundombinu ya umeme katika vijiji vilivyobaki inaenda sambamba na kupeleka umeme katika vitongoji kupitia miradi ya “ujazilizi”.
“Vijiji vilivyobaki ni kidogo hivyo kwa wakati huu pia tunaendelea na zoezi la kupunguza idadi ya vitongoji ambavyo havina umeme” amesema Wakili Kalolo
Wakili Kalolo amesema katika kikao hicho REA watawasilisha Mpango Kazi wa Mwaka ujao wa Fedha pamoja na Mpango wa Miaka Mitano wa REA kwa ajili ya kujadiliwa na Wabia wa Maendeleo kwa lengo la kutathimini utekelezaji wa mipango hiyo.
“Moja ya mambo tunayotarajia katika kikao hiki ni kupata ahadi toka kwa wafadhili kwamba watasaidia katika baadhi ya maeneo. Lazima tujenge hoja zinazokidhi vigezo vyao vya kupata ufadhili” amesema Wakili Kalolo.
Awali akifungua Mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja amesema utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijiji umeongeza fursa za uwekezaji katika maeneo ya vijijini na kutoa wito kwa wananchi kutumia umeme kwa ajili ya shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuanzishara biashara ndogo ndogo na za kati pamoja na viwanda.
“Umeme ni nyenzo muhimu kwa ajili ya maendeleo, ukiwa na umeme fursa nyingi za biashara zinafunguka” amesema Mhandisi Masanja
Mhandisi Masanja alitoa wito kwa viongozi wa vijiji na mitaa kuwahamasisha wananchi kutoa maeneo yao kwa ajili ya kupitisha miundombinu ya kusambaza umeme pamoja kutoa ushirikiano kwa kutunza na kulinda miundombinu hiyo.
“Nchi yetu imepiga hatua kubwa sana katika kusambaza umeme vijijini, mwaka 2015 ni vijiji takribani 2,000 tu vilikuwa na umeme, lakini leo tunazungumzia vijiji 10,400 vyenye umeme kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara” amesema
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini, Mhandisi Jones Olotu amewataka wananchi kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme ili waweze kuanzisha miradi mbalimbali itakayowainua kiuchumi.
Mhandisi Olotu amesema katika baadhi ya maeneo mwitikio wa wananchi kuunganisha umeme bado upo chini na kuwataka kuunganisha umeme kwa bei nafuu ya Shilingi elfu 27 na kwa ambao hawamudu gharama za kutandaza waya katika nyumba zao watumie kifaa maalum kijulikanacho kama Umeme Tayari ambacho ni mbadala wa wiring.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Wabia hao wa Maendeleo, Børjn Midthun ameiongeza REA kwa kazi nzuri ya kusambaza nishati vijiji na kuongeza kuwa imefungua fursa ya uwekezaji wa miradi ya nishati vijijini.