Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha David Lymongi akifungua kikao cha kufunga mradi wa Mlango.
kaimu Mkurugenzi wa THPS, Sisti Moshi akizungumzia mradi wa Mlango.
……………………………………………………………………………..
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha David Lymongi amesema kuwa mradi wa Mlango unaotekelezwa na taasisi inayojishughulisa na masuala ya kuboresha afya(THPS) umeweza kuzuia kusambaa kwa maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI kwa kiasi kikubwa kwa makundi hatarishi kutokana na kuwasaidia kurudi katika maisha ya kawaida.
Lyamongi aliyasema hayo wakati akifungua kikao cha kufunga mradi huo ulioanza mwaka 2018 na kuisha mwaka 2020 ambapo alisema kuwa mradi huo ulilenga kuwasaidia makundi ya watu walioathika na VVU, wanaofanya biashara ya ngono pamoja na walioathirika na madawa ya kulevya kwa kuwapa tiba pamoja nakuwatafutia shughuli mbalimbali za kufanya ikiwemo biashara.
“Shughuli hizo zimewafanya watu hawa wakati wote kuwa katika utafutaji hali iliyowafanya kuweza kujimudu kimaisha na kupambana na tabia hatarishi ambazo zingeweza kusambaza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI,” Alisema Lyamongi.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa THPS, Sisti Moshi alisema kuwa mradi wa mlango ni mradi unaofadhiliwa na Global fund kupitia AMREF ambapo wanachokifanya ni kuwatambua na kuwafikia waathirika hao na kuweza kuwapa huduma pamoja na kuwasaidia kuanzisha miradi mbalimbali ili waweze kupata kipato.
Alifafanua kuwa mradi hou uliotekelezwa katika wilaya tatu za mkoa wa Arusha ambazo ni Monduli, Arusha jiji pamoja na wilaya ya Ngorongoro umeweza kuwafikia watu wengi ambao baadhi ni waathirika wa UKIMWI, biashara ya ngono, wengine wakiwa ni waathirika wa madawa ya kulenya na kuyafanya maisha yao kuwa bora kwakuwa katika maisha ya kawaida.
“Tunawasaidia watoke katika njia ambazo zinaweza kuiathiri jamii kwani wakiwa katika biashara zao wanakosa muda wa kwenda kukaa vijiweni, muda wa kwenda kuvuta madawa ya kulevya lakini anajiingizia kipato ambacho kinawasaidia kuachana na tabia atarishi,”Alisema Moshi.
Nao wanufaika wa mradi huo akiwemo Rehema Saidi ambaye aliathiriwa na matumizi ya madawa ya kulevya alisema kuwa madawa yalimsababisha akayaharibu maisha yake pamoja na maisha ya watoto wake kwani mmoja anaosha vioo vya magari barabarani na mwingine yupo katika kituo cha kuhudumia waathirika wa madawa ya kulevya kilichopo Kisongo lakini hivi sasa ameimarika na kwakuwa yeye amepona na anabiashara anayoifanya anaendelea kuimarisha familia yake.
Amina Hamasi kutoka Monduli ambaye alikuwa anafanya biashara ya ngono aliishukuru THPS kwa kuwapa mtaji ambao umewawezesha kufungua biashara ya kuuza matunda pamoja na duka dogo la vitenge na kanga hali iliyowafanya kurejesha heshima yao katika jamii inayowazunguka pamoja na kuwa jasiri wa kuweza kuzitambua afya zao.
“Binafsi nimeweza kuacha tabia zile mbaya ambazo zilikuwa ni hatari kwa afya yangu lakini na kwa wengine na kwa sasa nina mchumba ambaye tunatarajia kuoana hivi karibuni ambapo tunaomba mradi huu uwe wa kudumu,” Alieleza Amina.