Home Mchanganyiko Tanzania Kinara Uhuru wa Vyombo vya Habari-Bashungwa

Tanzania Kinara Uhuru wa Vyombo vya Habari-Bashungwa

0

*******************************

-Awataka Waandishi kuwa wazalendo, kufuata Sheria

-Aahidi Neema Bodi ya Ithibati, Baraza huru la Habari

Na Grace Semfuko-MAELEZO

Mei 03, 2021

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofuata misingi, Sheria na kanuni za uendeshaji wa Vyombo vya Habari na kwamba mpaka sasa Serikali imevipa uhuru vyombo hivyo kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Akizungumza wakati akifungua mkutano wa Waandishi wa Habari katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Jijini Arusha Mei 3, 2021,  Waziri Bashungwa ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali ya Tanzania inafanya kila jitihada za kuhakikisha Watanzania wanapata habari za kweli  nchini kote

Akijibu hoja ya Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania kwa niaba ya vyama vyote vya tasnia ya Habari, ambao walisema kuna anguko la tasnia ya habari nchini Tanzania, Bashungwa amesema kutokana na Tanzania kuwa  na uhuru wa vyombo vya habari, imefanikiwa kusajili vyombo vingi vya habari kuliko nchi yeyote Afrika kama vile Magezeti 246, Redio 194, Television 53, Redio za mtandaoni 23, blogs 120 na OnlineTV 440.

“Nina hakika takwimu sahihi hazifiki kunakohusika, Tanzania tunaheshimu uhuru wa vyombo vya habari”, Waziri Bashungwa.

Ameongeza kuwa vyombo vya habari vinatakiwa vihakikishe  viwajibike kufuata sheria na kanuni za nchi ili vifanye kazi zao kwa ufanisi mkubwa katika kuuhabarisha Umma wa Watanzania kwa kitenda haki na bila upendeleo wowote.

“Ndugu zangu Wanahabari, nyinyi nyote ni mashahidi kuwa uhuru wa vyombo vya habari hapa Tanzania ni mkubwa ukilinganisha na nchi zingine, tumesajili vyombo vingi vya habari, lakini uhuru huo uendane na wajibu, naomba sana tuhabarishe kwa kufuata misingi ya sheria, ni muhimu kufuata sheria zilizopo ili kuepukana na baadhi ya  changamoto” , Waziri Bashungwa.

Akijibu hoja ya waandishi wa habari kuhusu hali ya uchumi wa waandish wa habari Waziri Bashungwa amesema kuwa  Sheria  Na. 12 ya Huduma za  Habari ya mwaka 2016 iliweka wazi uanzishwaji wa Bodi ya Ithibati na Baraza Huru  ili kuweza kutatua changamoto za wanahabari kama vile kutokuwa na mikataba, bima ya afya, mishashara isiyoridhisha yatatuliwa tu kupitia Taasisi hizo.

“Sheria yetu ya Huduma za Habari imeainisha kuwepo kwa bodi ya ithibati na baraza huru la habari, napenda niwataarifu tu vyombo hivyo vitaanza hivi karibuni, lengo ni kuwafanya Waandishi kuwa na sauti moja katika kusimamia kazi zao wenyewe na kukumbishana kufuata sheria” amesema Waziri Bashungwa.

Aidha, akiongelea sauala la taswira ya nchi vizuri kimataifa Waziri aliwataka Waandishi wa Habari kuwa wazalendo na nchi yao kwa kutoa habari sahihi zitakazoijengea heshima Tanzania na kuvutia uwekezaji pamoja na kujenga diplomasia imara ya kiuchumi.

“Ili kuvutia wawekezaji kuwekeza hapa nchini na kuwa na diplomasia imara kiuchumi hatuna budi kuhakikisha tunaitangaza vyema nchi yetu ndani nan je ya nchi, Tunapokuwa na kampeni hasi kwenye vyombo vya habari kuhusu nchi yetu tunajiua wenyewe kiuchumi, mfano Wawekezaji wanapopata taarifa hizi mbaya hawawezi kuja nchini kwetu, kwanza tunaathiri  diplomasia na uchumi, wote tuwe wazalendo,tusemee nchi yetu kwa mazuri, hata kama kuna mabaya tuwe na lugha fulani ya kufikisha ujumbe serikalini na sio kwenye vyombo vya habari,haitusaidii kama nchi” amesema Waziri  Bashungwa.