RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Maadhimishi ya Siku ya Wafanyakazini Duniani Mei Mosi yaliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
………………………………………………………………………………
Na Mwashungi Tahir ,Maelezo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ina malengo mazuri ya kuzitatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi ili kutekeleza vyema majukumu yao.
Hayo ameyasema leo huko katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil huko Kikwajuni wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa umma wa sekta mbali mbali wakiwemo wa Serikali na binafsi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ambayo huadhimishwa duniani kote.
Amesema Serikali inathamini na kutambua mchango muhimu wa wafanyakazi katika kufikia harakati za maendeleo na utekelezaji mzuri na kuhakikisha kuwa iko wazi kwa ajili ya kuwatumikia wafanyakazi wake.
Amefahamisha kuwa Serikali ina dhamira njema kwa watumishi kwani imeandaa mazingira mazuri kwa lengo la kufanya kazi kwa ufanisi katika nyanja zote za uchumi na katika kujipatia maendeleo .
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mudrik Ramadhani Soraga amesema wizara yake ina mshirikiano makubwa na Shirika la Kazi duniani (ILO) kwani imesaidia kutoa mafunzo kwa vijana wapatao 200 na kujipatia ajira.
amesema janga la corona bado linaathiri wafanyakazi katika kukwamisha maendeleo na pia kuathiri uchumi wa Nchi na hivyo wizara itaendelea kushirikiana na vyama shirikisho kuona hali inaimarika kwa kila sekta katika utendaji wa kazi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa shirikisho wa vyama vya wafanyakazi Mwatum Khamis Othmani akisoma risala amesema bado kuna baadhi ya watendaji wenye nyadhifa za juu hujifanyia marekebisho katika mishahara yao na kuwadhalilisha wafanyakazi wa chini.
Siku hii ya maadhimisho kwa wafanyakazi hufanyika kila mwaka Duniani kote ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni Uwajibikaji na haki ndio msingi wa maendeleo Zanzibar.