Home Makala WAJUMBE MSILEGEZE KAMBA, WEMBE NI ULE ULE

WAJUMBE MSILEGEZE KAMBA, WEMBE NI ULE ULE

0
……………………………………………………………………
Na Emmanuel J. Shilatu
Iyena! Iyena! Wajumbe mkutano mkuu maalum wa Chama Cha Mapinduzi Taifa nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Natumai mmeitikia “kazi iendelee”.
Tarehe 30/04/2021 mnaandika historia mpya nchini, Afrika na Dunia kwa kwenda kumchagua Mwenyekiti CCM Taifa  Mwanamke wa kwanza kabisa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuiongoza Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa katika historia yote ya maisha yake tangu kizaliwa mwaka 1977. Ikumbukwe CCM ni chama cha kwanza Afrika na cha pili Duniani kwa ukubwa, ukongwe na kushikiria madaraka kwa muda mrefu, Wajumbe mkaongeze rekodi nyingine ya kumfanya Ndugu Samia kuwa  Mwanamke wa kwanza kuwa Mwenyekiti CCM Taifa.
Si suala geni Mwanamke kuaminiwa ndani ya chama, walikuwepo akina Hayati Bibi Titi Mohamed ambao walionyesha uwezo wa hali ya juu ndani ya chama na kupitia jumuiya ya Wanawake (UWT), leo hii hatupaswi kuwa na hofu na mashaka na Ndugu Samia Suluhu Hassan kiutendaji, tumpe nafasi ataivusha salama CCM.
Wajumbe, Ndugu Samia kwa muda mrefu maisha yake ameishi CCM, amekitumikia CCM hivyo anaijua CCM kiunaga ubaga. Ndugu Samia ni mwana CCM kindaki ndaki si wa kuoteshwa na hajawahi kuyumba, hakuna mwenye mashaka na uanachama wake na uwezo wake pia.
Ndugu Samia ana uzoefu wa muda mrefu kiutendaji ndani ya chama na serikalini. CCM inakwenda kumpata Mwenyekiti jasiri, hodari, imara, Mzalendo, Mchapa kazi kwa mujibu wa historia yake ndani ya chama na Serikalini. Kama ni pishi basi limekwiva kweli kweli.
Nasikia vikao vya Kamati KUU CCM Taifa, Halmashauri KUU CCM Taifa vimeruka mtego wa wasioitakia mema CCM kwa kumpitisha kwa asilimia 100 kwa 100 kwa mapendekezo Ndugu Samia Suluhu Hassan kuwa Mwenyekiti CCM Taifa na sasa Wajumbe mkutano mkuu mkamalizie kazi kubwa iliyokwisha anzwa na mkaidhihirishie Dunia kuwa CCM imejaa umoja, ushirikiano, upendo na inayoendeshwa kwa mujibu wa vikao na Katiba na si maneno ya barabarani.
Wajumbe msilegeze kamba, wembe ni ule ule kumkabidhi Ndugu Samia Suluhu Hassan Uenyekiti CCM TAIFA ambao ni ndugu mmoja na Urais. Ngumu kutenganisha kofia hizi kwa Mtu mmoja. Namwombea kura za ndiyo Ndugu Samia Suluhu Hassan awe Mwenyekiti CCM Taifa
*Shilatu, E.J*