Home Mchanganyiko MITAMBO YA KUFUA HEWA TIBA (OKSIJENI) YASIMIKWA HOSPITALI ZA RUFAA ZA MIKOA...

MITAMBO YA KUFUA HEWA TIBA (OKSIJENI) YASIMIKWA HOSPITALI ZA RUFAA ZA MIKOA SABA.

0

Waziri wa Afya akimjulia Hali mmoja wa Watoto waliomo Kwenye wodi ilivyounganishwa Oksijeni Kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma.

Dkt.Gwajima akinawa mikono Mara baada ya kutoka Kwenye Duka la dawa la tiba asili lililopo Kwenye hospitali hiyo.Inashauriwa kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni.

Mmoja wa Wazazi wa Watoto waliolazwa Kwenye hospitali hiyo akiongea na Waziri wa Wizara ya Afya Dkt. Dorothy Gwajima wakati alipotbelea wodi hiyo na kujionea jinsi Oksijeni ilivyounganishwa wodini.

Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima akikagua mitambo ya kufua hewa tiba (Oksijeni) iliyosimikwa Kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma.

*******************

Na. Catherine Sungura, WAMJW-Dodoma

Serikali imeweza kujibu changamoto za wataalamu wa afya katika hospitali saba za rufaa za mikoa ili kuwahudumia kwa ufanisi wagonjwa wa dharura kwa kuimarisha kwa kusimika mitambo ya kufua hewa tiba (Oksijeni) na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji wa hospitali hizo na kuwezesha hospitali zingine za halmashauri na vituo vya afya.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati alipotembelea hospitali ya rufaa ya mkoa Dodoma kujionea jinsi walivyounganisha mitambo hiyo kwenye wodi ya wagonjwa mahututi na watoto.

Dkt.Gwajima amesema mitambo hiyo ambayo Serikali kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Dunia hivi sasa imefungwa kwenye hospitali za rufaa za mikoa saba ya Dodoma, Mtwara ,Manyara, Mbeya, Amana Geita na Songea na hivyo wizara yake ipo njiani kukamilisha kufungia hospitali zote za rufaa za mikoa hapa nchini.

“Mitambo hii imefungwa kwa gharama isiyopungua bilioni 1.4 kila hospitali na inalenga kuzalisha mitungi 200 ya hewa hiyo kwa masaa 24 , na kila mtambo unayo sehemu ya mabomba yenye mita 400 yanayosafirisha hewa hii pia mitungi 73 imenunuliwa pamoja na mitambo hii kwa hivyo, haya ni mapinduzi makubwa”. Alisisitiza.

Aidha, Dkt. Gwajima amefurahishwa na uongozi wa hospitali hiyo kwa kukamilisha kufunga mitambo hiyo na kuanza kutoa huduma kwenye wodi ya wagonjwa mahututi(ICU) pamoja na wodi ya watoto na hivyo wameweza kuunganisha vitanda 78 kutoka vitanda 10 vya awali na kufanya jumla ya vitanda 88 kupatiwa huduma hiyo hospitalini hapo.

“Hatua hii itapunguza kwa kiwango kikubwa gharama za kuhudumia mgonjwa mwenye mahitaji ya hewa hii. Wito wangu tuitumie vizuri na kuzingatia na kuhakikisha matengenezo kinga yanafanyika kwa ufanisi”.

Dkt. Gwajima amesema kuwa uwekezaji huo umeweza kujibu changamoto ya kipindi cha mlipuko wa Covid-19 ulioripotiwa nchini mwezi Machi mwaka 2020 na hivyo kusababisha kuongezeka kwa mahitaji ya hewa ya oksijeni na kuwa gharama zake zilipanda.

“Niwapongeze sana waganga wafawidhi wa hospitali za rufaa za mikoa kwa kuja na wazo hili la kufunga mitambo hiyo kwenye hospitali zetu na hivyo tutaweza kusaidia hospitali za wilaya na vituo vya afya na hivyo kuwapunguzia matumizi ya fedha ya kununua oksijeni, haya ni mapinduzi makubwa kwa Serikali yetu”. Alisisitiza Dkt. Gwajima

Aliongeza kuwa
Kwa upande kwa kuepuka magonjwa ya kuambukiza ambayo yameanza kuyakumba mataifa mengine, Waziri huyo aliwataka waganga wakuu wa mikoa na wafawidhi kwenye hospitali za rufaa za mikoa kuendelea kutoa elimu kwa umma kwa kutumia vyombo vya radio vilivyopo kwenye maeneo yao (Community radio) ili kuwaondolea wananchi hofu na kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza ikiwemo janga la Corona.

“Serikali kupitia sekta ya afya kwa kushirikia na wadau wake nchini iko makini kufuatilia kinachoendela duniani na kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama na imara katika kudhibiti milipuko ya magonjwa mbalimbali ikiwemo huu wa Covid-19”.Alisema Dkt. Gwajima.

Dkt. Gwajima aliwakumbusha wadau,wataalam pamoja na wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari muhimu ambazo zimekuwa zikielimishwa mara kwa mara dhidi ya kujikinga na kudhibiti magonjwa mbalimbali ikiwemo C0vid-19 kwa kuepuka hofu, kuimarisha tabia ya kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni, kufanya mazoezi,kula lishe au vyakula vya mbogamboga kwa wingi na matunda,kutumia tiba asili, kuepuka misongamano isiyo ya lazima na mwisho kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mara unapoona dalili za maradhi yeyote.

Naye Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa Dodoma Dkt. Ernest Ibenzi amesema wanatarajia kufunga mitambo ya kujazia hewa tiba hiyo ili kuweza kusaidia vituo vya afya vilivyo jirani na kusambaza huduma hiyo kwenye hospitali nzima.
-Mwisho-