Home Mchanganyiko Dkt. GWAMAKA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA KATIKA KIWANDA CHA IRON AND STEEL...

Dkt. GWAMAKA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA KATIKA KIWANDA CHA IRON AND STEEL KILICHOPO JIJINI DAR ES SALAAM

0

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samwel Gwamaka, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ukaguzi katika kiwanda hiko. 

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Muhandisi Samwel Gwamaka (wa tatu kushoto), akiangalia moshi unaotoka kiwandani hapo nakuelekea kwenye makazi ya watu katika kiwanda cha Iron and Steel Industry kinachojihusisha na uzalishaji wa nondo kilichopo Mikocheni Jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi Msaidizi wa Kiwanda cha Iron and Steel Industry Bw.Laurence       Manyama (wa pili kushoto), akitoa ufafanuzi kwa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Muhandisi Samwel Gwamaka (katikati) akiwa anafanya ukaguzi kiwandani hapo

**************************************

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Muhandisi Samuel Gwamaka, ametoa miezi sita kuletwa kwa mtambo wa kudhibiti uchafuzi wa hewa unaotokana na moshi na vumbi katika kiwanda cha Iron and Steel kilichopo mikocheni jijini Dar es Salaam. Kiwanda hicho kinajishughulisha na ununuzi wa vyuma chakavu na uzalishaji wa nondo.

Aidha Dkt. Gwamaka ametaka kiwanda hicho kutekeleza maagizo hayo ili kuweza kuepusha malalamiko yanayoletwa na wananchi wanaokaa karibu na kiwanda hicho. Amesema kuwa kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa Wananchi juu ya moshi mwingi unaotoka katika kiwanda hicho na kwenda kwenye makazi ya watu.

“Malalamiko ya Wananchi ni ya muda mrefu na NEMC imetembelea kiwanda hicho mara nyingi na kutoa maelekezo namna ya kudhibiti moshi unaoenda kwenye makazi ya watu ili kuepusha uchafuzi wa mazingira na malalamiko kutoka kwa wakazi wa eneo hilo. Tumetoa miezi sita kwa kiwanda hicho kununua mtambo wa kudhibiti moshi kama watakuwa hawajafunga mitambo na kudhibiti uchafuzi wa hewa maana yake kiwanda kitafungwa” amesema Dkt. Gwamaka.

Ameendelea kusema pamoja na hayo wamiliki wa kiwanda wanatakiwa kuandika barua ya kujieleza kuwa endapo hawajatekeleza agizo hilo kiwanda kifungwe. Dkt Gwamaka amesema kuwa  kutokana na uchafuzi wa mazingira unaoendelea katika kiwanda hicho ametoa faini ya shilingi million thelathini ambayo inatakiwa kulipwa ndani ya siku kumi na nne.

“ Kwa hiyo adhabu wamepata na watatekeleza na tumewaambia waendelee kutupa taarifa mara kwa mara juu ya maagizo tuliyotoa, pia tumewaambia katika kipindi hicho wafanye marekebisho kwa mapungufu yote tuliyoyaona ikiwemo kutokuwa na vifaa vya kujikinga kwa wafanyakazi wanapofanya uzalishaji katika kiwanda, kutengeneza kizimba cha kuhifadhia taka na kuwa na sehemu sahihi ya kuhifadhia mafuta machafu pamoja na kuweka vyuma chakavu katika sehemu iliyoezekwa kuepusha naji ya mvua kuingia na kupeleka kwenye mifereji” Amesema Dkt. Gwamaka

Naye Meneja wa Kanda ya Mashariki Kasikazini (NEMC) Bw. Arnold Mapinduzi, amesema kuwa amewaomba Wananchi wasichoke kutoa taarifa kwani mazingira ni yetu sote na uharibifu wa mazingira unapotokea una athari kwa viumbe vyote bila kubagua.

“Mazingira ni uhai endelevu wa binadamu, unapoharibu mazingira unaathiri afya zetu wenyenyewe na kama sio sisi leo basi kizazi kijacho. Mazingira yanapoharibiwa katika eneo moja huharibu maeneo yote kutokana na mfumo uliopo. Maji ya viwandani yanayomwagwa hapa Mikocheni hayaishii hapa tu bali yanaenda mpaka Kawe na maeneo yote yanayotuzunguka. Hivyo niwaombe wananchi kuendelea kutoa taarifa pale wanapoona uharibifu wa mazingira unafanyika”

Kwa upande wake Mwananchi anayekaa karibu na kiwanda hicho Bw. Khalid Salum, amesema kuwa wenye viwanda hivi maeneo ya mikocheni hawana makazi hapa hivyo wanapofanya uzalishaji baadaye wanaenda majumbani kwao yao ambayo ni mbali na maeneo ya viwanda hivyo.

“Uchafuzi wa mazingira katika viwanda maeneo ya Mikocheni ni wa muda mrefu ila tunashukuru NEMC kutupa ushirikiano na matarajio yangu kuwa watabadilika. Hata hivyo wamiliki wa viwanda hivi sio wakazi wa hapa hivyo hii athari tunayoipata wao kwao haina shida, wanajali pesa kuliko afya kitu ambacho hakina utu” amesema Bw. Khalid.

Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi wa Kiwanda Bw. Laurence Manyama, amesema kuwa kutokana na maelekezo waliyopewa wako tayari kutekeleza, kwani kiwanda kikifungwa itakuwa ni hasara kwao pamoja na wafanyakazi walioajiriwa hapo. Ameendelea kusema kuwa japo hawajafikia kiwango cha juu cha utunzaji wa mazingira lakini wamejitahidi kutekeleza kwa kiasi chake tofauti na kipindi cha nyuma hivyo maagizo yote waliyopewa na Mkurugenzi wa NEMC watayafanyia kazi ili kuepusha malalamiko kutoka wa Wananchi.

Dkt. Gwamaka amemaliza kwa kusema kuwa kuna baadhi ya viwanda wanatekeleza maagizo wanayopewa na kuzalisha bidhaa zake bila ya kuathiri mazingira. Hivyo amewaomba wazalishaji katika viwanda kufata yale wanayoelekezwa na Baraza ili kuepusha malalamiko kutoka kwa Wananchi. Ameendelea kusema kuwa ukaguzi utaendelea katika viwanda vingine na endapo watabainika wanachafua mazingira hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.