Home Mchanganyiko WAFANYABIASHARA WADOGO NA WAKUBWA RUVUMA WATAKIWA KUSAJILI BIASHARA ZAO

WAFANYABIASHARA WADOGO NA WAKUBWA RUVUMA WATAKIWA KUSAJILI BIASHARA ZAO

0

Katibu Tawala msaidizi Uchumi na Uzalishaji mkoa wa Ruvuma Deogratius Sibula kushoto akimkabidhi cheti cha usajili wa Biashara mjasilimali mdogo Belinda Lyimo wakati wa mafunzo ya utoaji elimu ya usajili ya Biashara na makampuni yaliyotolewa na  Wakala wa Usajili wa Biashara,leseni na Makampuni Brela yaliyofanyika jana mjini Songea.

Picha na Muhidin Amri

………………………………………………………………………….

Na Muhidin Amri,Songea

WAFANYABIASHARA wadogo na wakubwa mkoani Ruvuma,wametakiwa kusajili biashara zao ili ziweze kutambulika kisheria na kufungua wigo utakaosaidia kupata wateja wengi na mikopo kutoka katika taasisi za fedha.

Hayo yamesemwa  jana na Afisa Msajili msaidizi wa Wakala wa usajili wa biashara na leseni(Brela) Swalehe Yahaya wakati  akitoa  elimu  juu ya usajili wa  majina ya biashara na makampuni kwa wafanyabiashara,wasindikaji chakula na watengenezaji bidhaa ndogo ndogo wa Manispaa ya Songea katika ukumbi wa Sido mjini Songea.

Alisema,elimu hiyo itawasaidia wafanyabiasha namna bora ya kusajili  biashara zao,kujitangaza,kukuza na kulinda majina ya biashara zao ili kuepuka kuingiliwa na watu wengine.

Alitaja faida nyingine ya kusajili biashara inamwezesha  kuomba zabuni kwenye taasisi za umma ambapo kutokana na sheria mpya ni vigumu kwa mfanya biashara asiyesajili biashara au kampuni yake kupata zabuni serikalini.

Baadhi ya wafanya biashara wamepongeza hatua ya Brela kutoa elimu hiyo kwani imefungua  fursa ambayo itatangaza shughuli wanazofanya na uhakika wa kuuza bidhaa zao katika masoko mbalimbali ya ndani nan je ya mkoa wa Ruvuma.

Belinda Lyimo, ameishukuru Brela kuendesha mafunzo  na kutoa elimu ambayo  inakwenda kuwahamasisha kutengeneza bidhaa bora zenye uwezo wa kumudu  kwenye soko la ushindani kuongeza idadi ya wateja ikilinganisha na apo awali ambapo licha ya kuzalisha bidhaa bora, lakini hazikutambulika na watu wengi.

Ambinga Swai alisema,elimu ya usajili wa biashara na makampuni iliyotolewa na Brela itawezesha wafanya biashara sio kutambulika tu bali hata kulinda majina yao yasitumiwe na watu wengine kujinufaisha.

Alisema, ni jambo jema kwa wajasiriamali na wafanya biashara  kuweka mambo yao kisheria ili kulinda biashara zao,kuongeza idadi ya wateja na uhakika wa kupata zabuni kutoka kwenye taasisi za serikali.

Amewata wafanyabiashara, kuepuka kufanya  shughuli zao kwa mazoea kwani tabia hiyo ndiyo inayo changia sana kurudisha nyuma juhudi zao licha ya kuzalisha  na kuuza bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.