Home Mchanganyiko VIONGOZI WA VYAMA VYA USHIRIKA SONGEA WAONYWA

VIONGOZI WA VYAMA VYA USHIRIKA SONGEA WAONYWA

0

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Menas Komba akizungumza na watendaji na madiwani Lundusi mji Mdogo wa Peramiho picha ya maktaba

…………………………………………………………………………………

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Menas Komba amewaonya Wenyeviti wa Vyama vya Msingi vya Ushirika na wadau wa ushirika kujiepusha na udanganifu wa kuiba mazao ya wakulima kwa njia ya kuchezea mizani.

Komba ametoa onyo hilo katika kikao cha viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika na wataalamu wa Kilimo na Ushirika wa Halmashauri hiyo kilichofanyika jana  katika ukumbi wa Halmashauri hiyo uliopo mji mdogo wa Peramiho.

Komba amesema kumekuwa na malalmiko mengi toka kwa wakulima wakiwalalamikia viongozi na wadau wa Ushirika kuwaibia mazao yao kwa njia za ujanja ujanja ikiwemo kuchezesha mizani kwa lengo la  kuwadhulumu haki yao.

“Sipendi kusikia malalamiko toka kwa wakulima,kuibiwa mazao kupitia vipimo”,amesema  komba.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo wa Halmashauri amesema Ushirika uliundwa kwa lengo la kusimamia shughuli za wakulima na kuwasaidia na kwamba viongozi na wadau wa ushirika wanatakiwa kuwa makini katika kuwahudumia wakulima.

Amewaagiza viongozi wa Ushirika wa Halmashauri hiyo kushiriki kikamilifu katika zoezi la kudhibiti utoroshaji wa mazao toka ndani ya Halmashauri kwenda Halmashauri nyingine kwasababu kitendo hicho kinaikosesha Halmashauri hiyo mapato yanayotokana na ushuru wa mazao.

Ameongeza Halmashauri ya Wilaya ya Songea ni Halmashauri yenye rasilimali za kutosha kama vile mito inayotiririsha maji kipindi chote cha mwaka,eneo kubwa linalofaa kwashughuli za kilimo,mvua za  kutosha na shehena ya madini ya makaa ya mawe,ambapo amesema kinachohitajika ni ushirikiano katika usimamizi na ufuatiliaji  kwenye eneo la ukusanyaji wa mapato.

Kwa upande wao viongozi wa vyama hivyo wamesema kutokuwepo kwa bei elekezi ni changamoto kwao kwasababu kampuni zinakuwa huru kupanga bei wanazozitaka jambo linaoneka kumnyonya mkulima.

Wamesema msimu wa kilimo wa mwaka 2020 /2021 hapakuwa na bei elekezi badala yake Wizara ya Kilimo Ushirika na Umwagiliaji iliagiza mazao kuuzwa kulingana bei ya soko ya siku husika kitendo ambacho kiliwasikitisha wakulima.

Naye Meneja wa Chama kikuu cha Ushirika cha SONAMCU Juma Mwanga ametoa wito kwa wakulima kuzingatia usafi wanapoandaa mazao yao kwa nia ya kuyafikisha sokoni kwa vile kampuni zinanunua mazao ya wakulima katika baadhi ya maeneo, mazao yanakuwa  machafu hivyo kukosa  sifa kwamnunuzi.

 Mwanga ametoa rai kwa viongozi hao kuonesha moyo wa uzalendo na kudumisha mshikamano kwa kurudisha fadhira kwa wanachama kuchangia ujenzi na utekelezaji wa miradi ya kijamii mara wanapolipwa ushuru wao.

Afisa ushirika wa Halmashauri hiyo Damian Lwena amesema ushirika ni nyenzo muhimu  katika kufanikisha malengo ya wakulima, hivyo viongozi wasimamie vema ushirika na kuacha tabia za ubadhirifu wa mali za chama.

 Lwena amesema kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2021 /2022 wanakadiria kuvuna tani 3,304 za mazao yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ambayo ni ufuta tani 2678, soya tani 473 na mbaazi tani 253.

Halmashauri ya Wilaya ya Songea ina jumla ya vyama vya msingi vya ushirika 16 ambavyo vimesajiliwa na vinafanyakazi kwa mujibu wa kanuni,taratibu,na Sheria za nchi.