Home Mchanganyiko NEMC IMEWATAKA WAWEKEZAJI KUKUTANA NA KUJADILI NAMNA YA KUTATUA CHANGAMOTO ZAO

NEMC IMEWATAKA WAWEKEZAJI KUKUTANA NA KUJADILI NAMNA YA KUTATUA CHANGAMOTO ZAO

0

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka akizungumza na wanahabari katika ofisi za baraza hilo leo Jijini Dar es Salaam.

(Picha na Emmanuel Mbatilo)

********************************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC) limewataka wawekezaji kujitokeza ili kufanya mazungumzo yatakayokuwa na manufaa kwa pande zote mbili ambapo watajadili masuala ya ucheleweshwaji wa mchakato wa kufanya tathmini ya athari kwa mazingira (EIA).

Mkutano huo utafanyika Aprili 17 katika Ukumbi wa Kisenga Millenium Tower Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wanahabari leo Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka amesema kuwa mazungumzo hayo yatakuwa na nia ya kuboresha na kupokea changamoto za kiutendaji kutoka kwa wadau wa sekta ya Mazingira na tayari wameandaa namna bora ya utoaji wa vibali.

“Tukikaa pamoja ndo tutafahamu ni wapi tutataka kuweza kuboresha ili kuweza kufanya huu mchakato ambao unatija na hatimae uwekezaji usikwamishwe kwaajili ya sababu zingine zozote ambazo sio za msingi”. Amesema Dkt.Gwamaka.

Aidha Dkt. Gwamaka amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita haina malengo ya kukwamisha maendeleo katika Taifa hivyo mkutano huu umeitishwa kwa lengo la kutathmini ni wapi panahitaji kurekebishwa ili uwekezaji usikwamishwe kwa sababu zisizo za msingi.

Katika hatua nyingine Dkt. Gwamaka amesema suala la vifungashio vya plastiki visivyo na viwango kwa sasa limefikia mwisho na endapo mtu akikutwa anauza au kutumia vifungashio vya plastiki ambavyo havijakidhi viwango hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Hatutegemei kuona kifungashio kisichokua na kiwango, elimu imeshatolewa vya kutosha na tulifanya kikao na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) na wametuhakikishia kwamba viwanda vipo na vinatengeneza vifungashio vyenye kiwango kulingana na matumizi ya mtumiaji. Hivyo ukikutwa na kifungashio hakijakidhi kiwango utachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Kanda zote za NEMC Tanzania wameshaanza ukaguzi na utekelezaji unafuata endapo tutabaini mtu anauza au kutumia vifungashio visivyo na viwango” alisema Dkt Gwamaka