Na Dotto Mwaibale, Singida
VIJANA wa Mkoa wa wamempongeza Mama Samia suluhu Hassan kwa kula kiapo cha kuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Vijana wa Mkoa wa Singida Kaimu Afisa Vijana wa mkoa huo, Frederick Ndahani alisema wana imani kubwa na Rais Samia kwani kabla ya kushika nafasi hiyo ya juu alikuwa Makamu wa Rais ni Mama anayejua kazi na kujiamini lakini pia anaifahamu miradi yote ambayo ilianzishwa na Hayati John Pombe Joseph Magufuli mfano ujenzi wa Reli ya kisasa, Bwawa la Umeme ,madaraja na uboreshaji wa miondombinu ya barabara katika miji sambamba na uboreshaji wa usafiri wa anga na majini, ujenzi wa shule,vituo vya afya na hospitali.
” Rais Mama Samia amekuwa kiungo kikubwa katika kutatua kero za Muungano kwani ameshawahi kuwa Waziri wa Muungano na hata wizara ya Muungano ilikuwa chini yake wakati akiwa Makamu wa Rais, hivyo tunaamini muungano wetu utazidi kuimarika” alisema Ndahani.
Rais Mama Samia wakati wa kampeni alitembea nchi nzima kuomba kura katika uchaguzi wa mwaka 2015 na uchaguzi wa mwaka 2020, hivyo anaifahamu vizuri nchi yetu na mahitaji ya watanzania.
Alisema wao kama vijana wanaahidi kushirikiana vyema katika kipindi chote cha uongozi wake ukizingatia kuwa Rais aliyepita tayari alikwisha wajenga katika misingi ya uzalendo,kufanya kazi pamoja na kuipenda nchi yetu.
Ndahani alisema wanamuombea Rais Mama Samia Suuluhu Hassani kwa Mungu ampe afya njema na baraka katika kipindi chore cha uongozi wake.