Home Mchanganyiko RC MAHENGE AWATAKA WANANCHI KUJITOKEZA KWA WINGI KUMUAGA MAGUFULI

RC MAHENGE AWATAKA WANANCHI KUJITOKEZA KWA WINGI KUMUAGA MAGUFULI

0

 

…………………………………………………………………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma

MKUU wa mkoa wa Dodoma Dk. Binilith Mahenge,amewataka wakazi wa Dodoma pamoja na wananchi jirani kujitokeza kwa wingi kutoa heshima zao za mwisho kumuaga  aliyekuwa Rais wa awamu ya tano John Magufuli.

Kauli hiyo ametoa leo Machi 20,2021 wakati  akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya kuupokea mwili wa hayati Rais Magufuli aliyefariki Machi 17,2021 jijini Dar es saalam.

Aidha Mahenge amesema kuwa mpaka sasa maandazi yote ya muhimu kwa ajili ya shughuli za kuaga mwili wa hayati Rais Dk. John Magufuli yamekamilika.

“Mwili wa Mpendwa wetu Dk. John Pombe Joseph Magufuli utawasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma Jumapili tarehe 21 Machi, 2021 majira ya saa 10:00 jioni”amesema Dk. Mahenge

Dk.Mahenge amesema kuwa  mara baada ya kuwasili mwili huo utaelekea Ikulu ya Chamwino kwa kupitia barabara za Chako ni chako, Barabara ya Nyerere, Round about ya Mkuu wa Mkoa, Bunge, Morena, Bwigiri- Chamwino-Ikulu,  wanachi wote wa maeneo haya wanaombwa kujipanga kwenye barabara hizo kutoa heshima zao.

“Tarehe 22 Machi, 2021, Saa 12:00 asubuhi, mwili wa Mpendwa wetu Hayati Rais Dk. John Magufuli utatoka Ikulu kuja Uwanja wa Jamhuri kwa kupitia barabara mpya ya Mfugale, Bwigiri, Morena, Bunge, Round about ya Mkuu wa Mkoa, Barabara ya Nyerere, Uwanja wa Jamhuri, wananchi wa maeneo hayo mnaombwa kujitokeza kwa wingi.”amesema Dk.Mahenge

Dk.Mahenge amesema kuwa siku ya jumatatu Machi 22 itakuwa siku ya mapumziko hivyo ni siku ya kuaga Mwili na kutoa heshima za Mwisho kwa Hayati Rais Dk. John Magufuli katika Mkoa wetu wa Dodoma wananchi wache kwa wingi.

Mahenge amesema kuwa miongoni mwa shughuli zitakazofanyika ni gwaride la mazishi kutoka Jeshi la Wananchi la Tanzania, dua na sala, salamu za maombolezo na kutoa heshima za mwisho

”Nawaomba wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani wajitokeze kwa wingi katika uwanja wa Jamhuri Dodoma kumuaga aliyekuwa Rais wetu Mpendwa John Magufuli  katika uwanja wa Jamhuri Dodoma ili waje watoe heshima zao za mwisho”amesisitiza Mahenge

Aidh amewataka Wananchi kujitokeza  kuja kusaini vitabu vya maombolezo ambayo imeanza leo katika Uwanja wa Nyerere Square na katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa hapa Dodoma.