Home Mchanganyiko WAFUGAJI NA WAKULIMA WANAOENDESHA SHUGHULI ZA KIBINADAMU KATIKA BONDE LA WEMBERE WILAYANI...

WAFUGAJI NA WAKULIMA WANAOENDESHA SHUGHULI ZA KIBINADAMU KATIKA BONDE LA WEMBERE WILAYANI IGUNGA WATAKIWA KUONDOKA

0

Mkuu wa Wilaya ya igunga John Mwaipopo akitoa maelezo ya utangulizi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati(hayupo katika picha) kwa ajili ya kuwasilikiza wakazi wa Kijiji cha Makomero na kutoa uamuzi wa serikali kuhusu bonde la Wembere

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati akiwahhutubia wakazi wa kijiji cha Makomero jana alipokuwa akitafutia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa wafugaji na wakulima waliokuwa wakitumia Bonde la Serikali la Wembere la wilayani Igunga.

Picha na Tiganya Vincent

*****************************************

 NA TIGANYA VINCENT

RS TABORA

SERIKALI Mkoani Tabora imewataka wafugaji na wakulima ambao walikuwa wamepatiwa kwa muda kutumia Bonde la Wembere linalomilkiwa na serikali ambalo lipo wilayani Igunga kuondoka hiari ndani ya wiki mmoja.

Hatua imechukuliwa na Serikali kufuatia kuzuka kwa mapigano ya mara kwa mara baina ya pande mbili za wakulima na wafugaji na kutishia maisha yao.

Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati wakati alipokutana na pande mbili hizo katika Kijiji cha Makomero kwa ajili ya kuwasikiliza na kuutafutia ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo.

Alisema ndani ya siku hizo saba watu wanaondesha shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo wale waliojenga kaya 13 kinyume cha Sheria ndani ya bonde hilo wawe wameondoka na kubomoa kwa hiari nyumba walizojenga.

Dkt. Sengati alisema bonde hilo lina  maslahi mapana ya  Nchi  kwa sababu kuna ndege aina ya Flamingo ambao wanapatikana maeneo machache hapa duniani na ni chujio la maji yanayokwenda Ziwa Eyasi ambalo ni kivutio cha Utalii.

Aliongeza kuwa eneo hilo ni muhimu kwa Taifa na lazima lilindwe kwa kuwa kuna utafiti mkubwa wa utafutaji wa gesi na mafuta unaendelea katika bonde hilo na pia ni njia ya wanyamapori kuelekea Pori la akiba la Rungwa.

Kufuatia hatua Dkt. Sengati alisema ofisi yake itafanya majadiliano na  Ofisi ya Makamu Rais Mazingira, Wizara ya Maliasili na Utalii , Wizara ya Nishati , Wizara ya Maji na Wizara ya Ardhi na maendeleo ya Makazi ili kuona kama kuna eneo kati ya Bonde hilo linaweza kutolewa kwa ajili ya shughuli za wakulima na wafugaji na kuahidi kuwa baada ya majidiliano hayo atakwenda kuwa majibu.

“Serikali ilikuwa na nia nzuri ya kuwapa bonde hilo mlitumie kwa muda kwa shughuli na kilimo na malisho ya mifugo yenu …lakini eneo hilo hivi sasa nimegeuka sehemu ya mapambano na wengine kujimilikisha na kujenga nyumba wakati wanajua kuwa ni mali ya Serikali …mimi kama msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali siwezi kuona kuona hali hiyo ikiendelea” alisistiza.

Akijibu hoja za wakulima ambao tayari wameshalima mazao, Dkt. Sengati aliwahakikishia watu wote ambao walikuwa wameshalima ndani ya bonde hilo, mazao yao yatalindwa na ikifika kipindi kuvuna wataambia wakavune kwa usimamizi wa Serikali na kuongeza kwa kipindi hiki hakuna mtu anayeruhusiwa kwenda kulima wala kuchingia mifugo yake ndani yake.

“Mazao yenu yatalindwa kwa sababu hata wafugaji hawataki kuingiza mifugo yao ndani ya bonde kuanzia sasa” alisema

Alisema wamekuwa wakitumia kisingizio cha uwepo wa mazao kama kigezo cha kuendelea kuingia ndani ya bonde hilo kila mwaka na shughuli za kibinadamu ndani yake.

Katika zoezi hilo linafanyika kikamilifu aliiagiza kamati ya usalama ya Wilaya ya Igunga kuhakikisha ndani ya wiki  moja wakulima na wafugaji waliokuwa wamepewa kwa muda kulima na kuchungia mifugo yao katika Bonde la Serikali la Wembele wanasitisha shughuli zao na wameondoka.

Kiongozi wa kundi la Wakulima Kilimanjalo Masandu Masaganya alisema hawapingani na wazo la kuondoka katika Bonde hilo ,lakini wanaomba wapatiwe muda wa kuvuna mazao yake.

Alisema mazao yao yamekaribia kukomaa na anahofu na wafugaji wanaweza wakaingiza mifugo na kulisha kwenye mimea yao.

Kulwa Maganga alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Tabora kuwasaidia ili wafugaji wasiweze kuchungia mifugo yao katika mashamba yao pindi watakapokuwa mbali.

Alisema wanaunga mkono zoezi la kuhama pale bado wanachomba ni usalama wa mazao yao kwa kuwa zoezi hilo limekuja tayari wameshalima.

Mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Bonde ambalo ni la Serikali la Wembere umedumu kwa iaka 17 na umesababisha baadhi ya watu kuumizwa vibaya na wengine kupata ulemavu.