Home Mchanganyiko MKOA WA DODOMA WAJA NA MPANGO WA KUONGEZA UFAULU SHULE ZA MSINGI...

MKOA WA DODOMA WAJA NA MPANGO WA KUONGEZA UFAULU SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI

0

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa elimu Mkoa wa Dodoma waliokutana kuweka mikakati ya kuongeza ufaulu katika mkoa huo kwa shule za Msingi na Sekondari Kikao kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma.

Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Maduka Kessy akizungumza wakati akiwasilisha tamko la mikakati ya kuongeza ufaulu kwa Mkoa wa Dodoma katika kikao cha wadau wa elimu Mkoa wa Dodoma waliokutana kuweka mikakati ya kuongeza ufaulu katika mkoa huo kwa shule za Msingi na Sekondari Kikao kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma.

Mtoa maada katika kikao cha wadau wa elimu Mkoa wa  Dodoma Profesa Shaaban Mlacha akiwasilisha maada ya changamoto zinazoikumba Mkoa wa Dodoma na kupelekea kushindwa kufaulisha vizuri baada ya kufanya utafiti kwa Mkoa mzima wa Dodoma Kikao kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma.

Mbunge wa Jimbo la Kongwa ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa elimu Mkoa wa Dodoma waliokutana kuweka mikakati ya kuongeza ufaulu katika mkoa huo kwa shule za Msingi na Sekondari Kikao kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma.

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Antony Mavunde  akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa elimu Mkoa wa Dodoma waliokutana kuweka mikakati ya kuongeza ufaulu katika mkoa huo kwa shule za Msingi na Sekondari Kikao kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma.

………………………………………………………………………………………

Na.Alex Sonna,Dodoma

Katika kuhakikisha kiwango cha ufaulu kwa shule za Msingi na Sekondari kinapanda kwa Mkoa wa Dodoma kila halmashauri imetakiwa kuweka mikakati mizito na kuifuatilia kwa kina ikiwamo kuwashirikisha wazazi na wadau wa elimu katika kufikia malengo ya kupandisha ufaulu kwa mkoa huo.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma wakati akiwasilisha tamko la Mkoa katika kikao cha wadau wa elimu katika Mkoa huo waliokutana kwa lengo la kushirikishana mbinu katika kuboresha elimu ya Mkoa ili kupandisha kiwango cha ufaulu.

Amesema ni lazima kila Halmashauri kuhakikisha inakuwa na mkakati sambamba na kuupangia bajeti ili kuweza kupunguza kiwango kufeli kwa wanafunzi na kushughulikia vikwazo vyote vinavyopelekea Watoto kushindwa kuzingatia masomo na kushindwa kufaulu.

“Kila halmashauri kuwe na ufuatiliaji wa kina wa ufundishaji wa kila shule na kila mwalimu, Mkuu wa Wilaya asimamie Wakurugenzi wake na Mkurugenzi asimamie wakuu wa idara hadi ngazi za chini tunataka ufaulu upande hapa tulipo ni aibu tupu” amesema Maduka.

Amesema Dodoma ya sasa si Dodoma ya miaka mitano ya nyuma kwa sasa Dodoma ni Mkoa wa kisera na utawala hivyo ni aibu kuona Mkoa ukishika nafasi za chini katika kiwango cha ufaulu amebainisha kuwa wameweka mikakati mbalimbali baada ya miaka mitatu wawe nafasi ya 15 na 2025 kuwa namba chini ya 10 kitaifa.

Ameongeza “Katika halmashauri zetu tunataka ziondoke huko kwa sasa na kila Halmashauri lazima iwe chini ya 100 kitaifa ili kiwango cha kimkoa kipande yote haya yatafanikiwa ufuatiliaji wa kina kila ngazi ukifanyika” amesema.

Amesema kila Halmashauri ziweke utaratibu wa kuweka mikutano na wazazi ili kuwashirikisha katika mambo mbalimbali na siku hiyo itumike kusoma matokeo ya wanafunzi ili mzazi wake ajue nafasi yam toto wake hiyo itaweza kusaidia kuongeza hamasa kwa wazazi kuwasimamia Watoto na Watoto kuongeza kujituma katika masomo.

Katika tamko hilo limetaka Halmashauri zenye shule na wanafunzi wake wanazidi wanafunzi 800 kwa shule ya Msingi na wanafunzi 500 kwa shule za Sekondari kuanza kujiandaa kujenga shule nyingine au kujenga shule shikizi na katika chumba kimoja cha darasa kwa shule za msingi wasizidi wanafunzi 50 na kwa Sekondari wasizidi 40.

Amesema ili kufikia malengo ni lazima kila robo ya mwaka kufanyika kwa tathmini ya maendeleo kwa kila Halmashauri ili kushirikiana katika changamoto zilizopo katika kutekeleza hayo kufikia malengo yaliyowekwa ya kuongeza ufaulu.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge wakati akifungua kikao hicho amewataka wakuu wa Wilaya na wakurugenzi kwenda kusimamia hayo sambamba na kuwasimamia waratibu wa shule na kuwa wabunifu katika kutekeleza tamko hilo.

Ameongeza kuwa “ tutakuwa tukikutana na kamati kutathmini nini kimefanyika Chemba na nini kimefanyika Kondoa lengo letu ni kuhakikisha haya tunayokubaliana yanatekelezeka na mnapokutana na ugumu wowote tushirikishane lengo tufike tulipopataka” amesema Dkt Mahenge.

Katika kikao hicho Mbunge wa Kongwa ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai amesema kuna haja ya kufanyika tathmini kwani viongozi wengi ngazi ya kata hawatekelezi majukumu yao hivyo wafuatiliwe ili watekeleze majukumu yao kikamilifu.