Home Makala UPATU HARAMU KICHOCHEO CHA UMASIKINI KWA JAMII INAYOTUZUNGUKA

UPATU HARAMU KICHOCHEO CHA UMASIKINI KWA JAMII INAYOTUZUNGUKA

0

NA EMMANUEL MBATILO

Mojawapo ya changamoto ambazo hujitokeza katika katika historia ya usimamizi wa sekta ya fedha ni kuibuka kwa mipango ya upatu haramu. Changamoto hii imeongezeka zaidi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na maendeleo ya kiteknolojia hususan inteneti na mifumo ya malipo ya kielektroniki inayowawezesha waendeshaji wa upatu haramu kujificha. 

Mataifa mbalimbali yamekuwa yakifanya jitihada ya kupambana na upatu haramu kutokana na madhara makubwa yanayoweza kuletwa na mipango hiyo. 

Wengi Hujiuliza Upatu Haramu ni Nini?

Ingawa upatu haramu unafanyika katika jamii yetu lakini kuna baadhi ya watu bado hawajafahamu kuhusu suala hilo pasipo kuwa na elimu.

Upatu haramu ni mpango wa kuchangisha fedha unaoendeshwa na mtu au kikundi fulani cha watu kwa ahadi ya kuwapatia wachangiaji kiasi kikubwa cha faida katika kipindi kifupi. 

Utaratibu au mpango huu pia hujulikana kama mpango wa piramidi kutokana na muundo wake, wa watu wengi kuchangia watu wachache.

Upatu haramu au mipango ya piramidi hujitokeza katika miundo mbalimbali. Hivi sasa maendeleo makubwa ya TEHAMA yamesababisha kuibuka kwa aina nyingi mpya za upatu haramu yenye kushirikisha mamilioni ya watu kimya kimya.

Hili linatokana na wepesi wa kuwafikia watu kwa njia kama vile inteneti na urahisi wa kufanya malipo mtandaoni.

Utaratibu wa Upatu Haramu

Katika utaratibu wa upatu haramu unaofanyika hufanyika ili kuvutia wateja zaidi, waendesha mpango wa piramidi hulazimika kuongeza kiasi cha faida hadi wanaposhindwa kufanya malipo waliyoahidi. Hali hii husababisha hofu na mashaka na kusababisha washiriki kutaka kuokoa fedha zao.

Hata hivyo wakati jitihada hizo zikiendelea waendesha mpango wa piramidi hutoroka au hukamatwa na vyombo vya dola kwa hatua za kisheria.

Katika siku za mwanzo, mpango huo huchanua na kupata umaarufu kutokana na faida kubwa wanayopewa watu waliowekeza mwanzoni. Watu hao hutumika kushawishi watu wengine kujiunga.

Aidha Mpango wa piramidi hukua hadi kufikia mahali ambapo fedha inayotakiwa kulipwa kwa wateja wa mwanzo ni kubwa kuliko makusanyo kutoka kwa wateja wapya.

Muundo wa Biashara Mtandao

Wahalifu wengi wametumia mwanya wa maendeleo ya biashara mtandao (network marketing) au biashara ya ngazi (multi-level marketing) kuendesha upatu haramu.Hii inapeleka watu wengi kuibiwa na kushindwa kusaidika kwa urahisi zaidi

Wakati mwingine washiriki hushawishiwa kujiunga kwa kutoa kiasi fulani cha pesa kama kiingilio na kisha kupatiwa bidhaa zenye thamani kidogo kuliko kiingilio alichotoa.

Pia mshiriki hulazimika kununua bidhaa kwa bei ya juu kutoka kwao kila mwezi na kutafuta washiriki wapya ili wajiunge na mtandao huo.

Baadhi ya sifa zinazotofautisha upatu haramu na biashara halali za mtandao ni:

 • Msisitizo huwa kwenye kudahili wateja wapya badala ya bidhaa;
 • Huuzwa kwa bei ya juu sana kuliko thamani halisi ili kuwezesha upatu haramu kulipa malipo kwa washiriki wake;
 • Hupendelea bidhaa zisizokuwa na utambulisho rasmi ili kuficha thamani halisi.
 • bidhaa hizo kwa kawaida huwa hazihitajiki sana kwa matumizi ya kawaida na hivyo kutokuwa na soko.

Mbinu Zinazotumiwa na Waendesha Upatu Haramu  

 • Ahadi ya kuzalisha fedha nyingi (hata maradufu) kwa muda mfupi;
 • Kutumia taasisi au vikundi vinavyoaminika kama dini na hivyo kuwa rahisi kurubuni waumini wao;
 • Kufanya mikutano ya kushawishi washiriki wapya kwa ufanisi;
 • Waendesha mpango kuonyesha orodha ya watu mashuhuri kijamii na kisiasa ambao wanadaiwa kushiriki upatu huo na kufanikiwa;

Pia washiriki kutopewa muda wa kutosha kutafuta ushauri kwa  maelezo kwamba watakosa bahati.

Madhara ya Kiuchumi yanayotokana na Upatu haramu

 • Watu huondoa mitaji kutoka kwenye shughuli za uzalishaji na huzielekeza kwenye upatu haramu usiokuwa na tija kiuchumi;
 • Waweza kusababisha uhamishaji wa mitaji kwenda nje ya nchi (capital flight) na hivyo kuzorotesha shughuli za ndani na kusababisha upungufu wa fedha za kigeni.
 • Watu walioathiriwa na upatu haramu hugeuka kuwa mzigo mzito kwa serikali na jamii iliyowazunguka kutokana na kutomudu gharama za maisha.
 • Wananchi huzama katika lindi la mawazo ya kuvuna mapesa tu na hivyo kutoshiriki ipasavyo katika shughuli za uchumi kama kilimo, viwanda na biashara.

Mipango na biashara kama hizo zimewahi kujitokeza siku za nyuma na hivi karibuni na kusababisha wananchi wengi kupoteza fedha zao. Mifano ya mipango na biashara hizo ni pamoja na:

 • Development Enterprise Community Initiatives (DECI);
 • Rifaro Africa Limited;
 • IMS Marketing Tanzania Limited(Wakala wa One Coin);
 • D9 Club;
 • Kuku Farmers Limited; na

Nyingine zinazoendelea kuchunguzwa.

Imeandaliwa na Emmanuel Mbatilo kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania BoT

0673956262