Home Mchanganyiko NDALICHAKO AITKA SUMA JKT KANDA YA MAGHARIBI KUKAMILISHA UJENZI WA CHUO KIPYA...

NDALICHAKO AITKA SUMA JKT KANDA YA MAGHARIBI KUKAMILISHA UJENZI WA CHUO KIPYA CHA UALIMU KABANGA IFIKAPO JUNI 2021

0

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akisikiliza maelezo kuhusu ujenzi wa Chuo kipya cha Ualimu Kabanga kutoka kwa Msimamizi wa ujenzi Luteni Kanali Onesmo Njau.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akijadili jambo na Msimamizi wa ujenzi Luteni Kanali Onesmo Njau Muonekano wa baadhi ya majengo yanayoendelea kujengwa katika Chuo kipya cha Ualimu Kabanga Wilayani Kasulu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akimwelekeza kitu msimamizi wa ujenzi wa Chuo kipya cha Ualimu Kabanga Luteni Kanali Onesmo Njau alipofanýa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho.

*************************************************

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknojia Profesa Joyce Ndalichako ameitaka SUMA JKT Kanda ya Magharibi kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa Chuo Kipya cha Ualimu Kabanga ifikapo Juni 2021.

Profesa Ndalichako ametoa agizo hilo mjini Kasulu baada ya ukaguzi kazi ya ujenzi wa chuo hicho na kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji mradi huo.

“Ujenzi wa Chuo cha Kàbanga ulianza Machi 19, 2019 na ulipaswa kukamilika Juni 2020, pamoja na mkandarasi kuongezewa muda wa miezi nane bado kazi haijakamilika, hili halikubaliki,”alisema Waziri Ndalichako

Waziri Ndalichako amesema Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 10.6 bado unasuasua, na hata katika eneo la ujenzi hakuna wafanyakazi wala vifaa huku SUMA JKT wakiwa tayari wameshalipwa bilioni sita.

“Nimetembelea na kukagua kila jengo hapa, majengo mengine hayana wafanyakazi na yaliyo na wafanyakazi ni wachache na wala hakuna vifaa vya kufanyia kazi hapa. Mradi huu umekuwa ukisuasua tangu umeanza” amesema Waziri Ndalichako

Amesisitiza kukamilika kwa ujenzi huo ili kuokoa wanachuo wanaoendelea kutumia majengo ya chuo cha zamani ambayo ni hatarishi na kwamba ubovu wa majengo ya Chuo cha zamani ndio umepelekea
Serikali kuja na uamuzi huo wa kujenga upya Chuo hicho.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Ualimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Huruma Mageni amemwambia Waziri kuwa chuo hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili wanachuo 800 kwa mara moja ambapo awamu ya kwanza ya ujenzi utawezesha kudahili wanachuo 400.

Mageni ametaja majengo yatakayojengwa katika awamu ya kwanza ni pamoja na maktaba, bweni moja la wanachuo wa kike na moja wa kiume, ukumbi wa mihadhara pamoja na mikutano, bwalo la chakula na jiko.

Majengo mengine ni jengo moja lenye madarasa kumi, jengo la utawala, zahanati na nyumba nne za wakufunzi.

Naye msimamizi wa ujenzi kutoka SUMA JKT Luteni Kanali Onesmo Njau amesema wanashukuru wamepata fedha nyingine kutoka Wizara ya Elimu na kuwa wanakwenda kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri na watakamilisha kazi hiyo kulingana na maelekezo.

Wakati huo huo katika kuonesha msisitizo wa uhitaji wa Chuo hicho kukamilika, Ndalichako ameambatana na wakandarasi hao kuwaonesha hali halisi ya uchakavu ya majengo yanayotumika sasa.