Home Mchanganyiko WANANCHI WALAZIMIKA KUZNGUKA ZAIDI YA KM 30 KUFUATA HUDUMA KWA KUKOSA BARABARA...

WANANCHI WALAZIMIKA KUZNGUKA ZAIDI YA KM 30 KUFUATA HUDUMA KWA KUKOSA BARABARA YA KM 7.3

0

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo akiongea na Wananchi wa Kijiji cha Ntumbi, Kata ya Mpui, Wilayani Sumbawanga 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo pamoja na viongozi wengine wakitoka katika jengo la Zahanati ya kijiji ya Ntumbi ambapo Mh.Mbunge wa KWela ameahidi kutoa mifuko ya Saruji 60 na Mkuu wa mkoa mifuko 40 ili kuweza kumalizia jengo hilo.

……………………………………………………………………………

Wananchi wa Kijiji cha Ntumbi, Kata ya Mpui, Wilayani Sumbawanga wanalazimika kuzunguka zaidi ya km 35 kufuata huduma muhimu ikiwemo za kimahakama, elimu pamoja na Afya katika makao makuu ya kata baada ya kutokuwepo kwa barabara ya km 7.3 inayounganisha Kijiji hicho na makao makuu ya kata hiyo.

Hayo yamejitokeza baada ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kufika katika Kijiji hicho wakati wa ziara yake ya kukagua barabara zinazosimamiwa na Wakala wa barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) ili kubaini barabara zenye umuhimu kwa mahitaji ya wananchi na hatimae kutilia mkazo katika kuziombea fedha ili kuwakomboa wananchi na adha hizo.

Wakati akielezea changamoto ya Kijiji hicho Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Apolinary Macheta alisema kuwa barabara ambayo haipo ni ya kutoka Kijiji cha ntumbi kuelekea Kijiji cha Ilembo yenye km 7.3 na barabara inayotoka Kijiji cha Ilembo kwenda Mpui yenye km 5 ipo na inatumika.

“Kwahiyo ikikamilishwa hii barabara itakuwa imetusaidia sana hasa kuokoa kina mama wajawazito inapotokea mama ameshindwa kujifungua tunamfuata haraka kwa gari kumpeleka kwenye huduma, kwahiyo tunaiomba TARURA wajitahidi kutufungulia hii njia ili itusaidie hasa kuokoa wagonjwa na wananchi wa Ntumbi,” Alisema.

Kabla ya Kumkaribisha Mh.Wangabo, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule alisema kuwa wananchi wa Kijiji hicho wanategemea huduma kutoka katika kata ya Mpui ambayo ni kilometa 15 kutoka Kijiji hapo lakini kutokana ka kukosekana kwa mtandao wa barabara wanalazimika kuzunguka Zaidi ya kilometa 30 kufika Mpui.

“Kijiji hiki kinahudumiwa na kata ambayo ni ya Mpui, kata ya mpui ipo km 15 kutoka hapa lakini huyu mwananchi hawezi kwenda pale Mpui lazima aende (Kijiji cha) Itela, akitoka Itela aende (Kijiji cha) Kaengesa,(km17.3) kisha (Kijiji cha) Mkima ndipo aende Mpui (km 15), huduma za mahakama, afya, na sekondari Watoto wao wanasoma Mpui Sekondari, tumeona ni kati ya vijiji katika wilaya yetu ambavyo havikuwa na mtandao kabisa wa barabara, hakuna maji, umeme pia haupo,” Alisema.

Mmoja wa wananchi Ditrick Bluma akielezea baadhi ya chanagamoto zilipo katika Kijiji hicho alisema kuwa toka Kijiji hicho kianzishwe hakijawahi kufikiwa na mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya amefika hapo mara ya kwanza mwaka 2020, na hivyo wana Imani kuwa changamoto zao zinajulikana na zitatatuliwa.

“Mimi nipo hapa kwa kuomba Zaidi, sijui mara mbili yake, sijui mara kumi au amara mia moja, tunaomba mjitahidi hii barabara kututobolea waheshimiwa, pia umeme tunashida sana tunauhitaji uwepo, pia na zahanati kama mnavyosema mtusaidie wazee wetu,”Alisema.

Aidha, Mkazi wa Kijiji cha Itela kilichopo njiani kuelekea Ntumbi Frank Severino alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo katika barabara hizo za TARURA kutoka Ntumbi kuelekea Kaengesa hazina mifereji wala Kalavati na hivyo wakati mvua zinapozidi husababisha maji kukata barabara hizo na kuongeza kuwa hata madaraja yalijengwa yapo chini kiasi cha maji kupita juu yake na kukatisha mawasiliano kipindi cha mvua za masika.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mhandisi Samson Karilo alisema kuwa matengenezo ya barabara ya kutoka Kijiji cha Kaengesa hadi Kijiji cha Ntumbi yenye km 17.3 yamekamilika kwa asilimia 100 huku km 4 kati ya hizo zikiwa zimetengenezwa kwa kiwango cha changarawe.

“Zimebaki km 7.3 kuifikisha Mpui na kwenye bajeti ya mwaka huu tumeiombea na lengo ni kuifikisha Mpui, changamoto zilizopo ndio zile zile tu kwamba tunakabiliwa na ufinyu wa bajeti, tunayopokea haiakisi mahitaji halisi ya barabara, chanagamoto nyingine ni mifugo inapita sana barabarani, ng’ombe wakipita barabara inapoteza sura yake,” Alisema.

Wakati akijibu kero za wananchi Mh. Wangabo aliwataka TARURA kuhakikisha wananwashirikisha wananchi kabla ya kuanza mradi wowote wa ujenzi wa barabara na madaraja katika maeneo yote ya mkoa na kukemea tabia ya watalaamu wa serikali kujifanyia mambo bila ya kushirikisha wala kuwapa taarifa wananchi na matokeo yake kushindwa kuepuka chanagamoto za uharibifu wa barabara.

Kwa upande wa mifugo Mh. Wangabo alisema, “Make serikali ya Kijiji hiki cha ntumbi Pamoja na kule Itela, serikali hizi za vijiji zikae, zidhibiti mifugo, kwasababu hilo ni jukumu la serikali za vijiji na wananchi kwa ujumla na suala hilo liende kwenye kamati ya maendeleo ya kata na hili suala liwe la kata nzima na kata nyingine zote ndani ya mkoa huu, kusimamia barabara zisiharibike, zisiharibiwe na mifugo.”