Home Mchanganyiko UPATIKANAJI WA UMEME WA UHAKIKA KUFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI WA VIWANDA KATIKA...

UPATIKANAJI WA UMEME WA UHAKIKA KUFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI WA VIWANDA KATIKA WILAYA YA KILOMBERO NA IFAKARA

0

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Ismail Mlawa akiwasikiliza wajumbe wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Nishati Vijijini (hawapo pichani) walipomtembelea ofisini kwake tarehe 18/02/2021 walipokuwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa ujenzi wa kituo cha kusambaza na kupooza umeme cha Ifakara.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Ismail Mlawa akiongea na ujumbe wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Nishati Vijijini walipomtembelea ofisini kwake tarehe 18/02/2021 walipokuwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa ujenzi wa kituo cha kusambaza na kupooza umeme cha Ifakara.

Wajumbe wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Nishati Vijijini kutoka kulia Luis Accarro, Styden Rwebangila wakiwa pamoja na wadau wengine wanaoshiriki katika utekelezaji wa ujenzi wa kituo cha kusambaza na kupooza umeme cha Ifakara.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi wa Bodi ya Nishati Vijijini, Mhandisi Styden Rwebangila akitoa maelekezo kwa wakandarasi wanaojenga kituo cha kusambaza na kupooza umeme cha Ifakara wakati wa ziara ya Kamati yake kukagua utekelezji wa Mradi huo

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhandisi Styden Rwebangila wa kwanza kushoto akisikiliza maelezo ya ujenzi wa Kituo cha Kusambaza na Kupooza Umeme cha Ifakara kutoka kwa Meneja wa Mradi huo kwa upande wa TANESCO Mhandisi, Didas Lyamuya aliyepo kulia katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga wakati walipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhandisi Styden Rwebangila wa kwanza kushoto akiwa na wadau wanaoshiriki katika utekelezaji wa ujenzi wa Kituo cha Kusambaza na Kupooza Umeme cha Ifakara.

……………………………………………………………………………

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Ismail Mlawa amesema kuwa Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kusambaza na Kupooza Umeme cha Ifakara (Ifakara substation) utakapokamilika utachochea uanzishwaji wa viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na madini katika Wilaya ya Kilombero na Ulanga.

Mhe. Mlawa ameyasema hayo leo Februari 18,2021  alipokutana na ujumbe wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Nishati Vijijini ofisini kwake wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara ya ukaguzi wa Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kusambaza na Kupooza Umeme cha Ifakara.

“Mradi utaleta manufaa zaidi katika wilaya ya Kilombero na Ulanga na utakuwa ni kichocheo kwa wanaokusudia kufungua viwanda” alisema na kusisitiza mradi ukamilike kwa wakati.

Akizungumzia lengo la ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Nishati Vijijini, Mhandisi Styden Rwebangila alisema kuwa lengo la ziara yao ni kukagua utekelezaji wa mradi huo. Alisema kuwa mradi ukikamilika utawezesha kupatikana kwa umeme wa uhakika na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi hasa wakulima na wawekezaji wa viwanda vya kusindika nafaka.

 Aidha Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho chenye ukubwa wa MVA 20 kitawezesha kuwa na umeme wa uhakika. Alitoa wito kwa wawekezaji wa viwanda kuchangamkia fursa ya kuwekeza viwanda vya kusindika mazao hususan zao la mpunga ambalo linalimwa kwa wingi katika maeneo hayo.

Sambamba na ujenzi wa kituo hicho jumla ya vijiji 15 vitapelekewa umeme ambapo takriban wateja wa awali 1,500 wataunganishiwa umeme. Mhandisi Maganga alisema Mradi huo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 23 unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya na Serikali ya Tanzania. “Wananchi ambao wamekuwa na shida ya umeme na wameshindwa kuanzisha viwanda kwa sababu ya tatizo la umeme niwaeleze tu kuwa umeme utakuwa ni wa uhakika”