Bweni la wavulana katika Shule ya Sekondari Wino Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma ambalo ujenzi wake uliibuliwa na wananchi wa kata ya Wino kwa lengo la kuwaondolea usumbufu wanafunzi wa shule hiyo kupanga vyumba mitaani ambalo wakala wa huduma za misitu TFS kupitia shamba laWino limemalizia kujenga kwa kutoa bati,rangi na kutengeneza madirisha ambapo sasa wanafunzi 58 wanalala katika Bweni hilo.
Picha na Muhidin Amri
………………………………………………………………………………………
Na Muhidin Amri,Madaba
WANAFUNZI wa shule ya sekondari Wino Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma,wameondokana na hadha na usumbufu wa kuishi mbali na shule na wengine kupanga vyumba uraiani kufuatia wakala wa misitu TFS kupitia shamba la Wino kukamilisha ujenzi wa bweni moja la wavulana.
Wanafunzi wa shule hiyo hasa wavulana walilazimika kupanga vyumba kwenye nyumba za wenyeji kutokana na ukosefu wa mabweni hali iliyochangia kushuka kwa taaluma,matukio ya wizi na kukithiri kwa utoro kwa wanafunzi.
Mkuu wa shule ya Sekondari Wino Benaya Mkumba alisema,ujenzi wa bweni hilo ulianza tangu mwaka 2017 kwa wazazi na jamii kusimamisha boma, hata hivyo walishindwa kukamilisha kwa kukosa fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya viwandani kama bati,nondo na saruji.
Hata hivyo Mkumba alisema, baada ya muda mrefu tangu kuzimama kwa ujenzi huo wakala wa misitu Tfs kupitia shamba la miti Wino umesikia kilio chao na kutoa bati 100 zilizosaidia kuezeka bweni hilo pamoja na ofisi moja ya walimu,saruji kwa ajili ya kupiga lipu ndani na nje pamoja na sakafuni.
Alisema, mbali na vifaa hivyo Tfs imetoa rangi na kutengeneza madirisha yote ya bweni ambalo limeanza kutumika kulala wanafunzi wa madarasa ya mitihani yaani wanafunzi wa kidato cha pili na nne ili wawe jirani na shule na kupata muda mwingi wa kusoma.
Mkumba alisema,kukamilika kwa bweni hilo kumesaidia sana kudhibiti nidhamu ya wanafunzi,kuongezeka kwa taaluma na kupunguza gharama ya maisha kwa wanafunzi kupanga vyumba kwa wenyeji wa maeneo hayo.
Wakiongea huku wakibubujikwa na machozi ya furaha baadhi ya wanafunzi Faluja Halfan wa kidato cha nne na Sixtus Nuru wa kidato cha pili wameishukuru Tfs kukamilisha ujenzi wa bweni hilo kwani umewaondolea hadha ya kuishi mbali na shule pia kumaliza changamoto ya kupanga vyumba jambo lililochangia sana kushuka kwa taaluma kwa wanafunzi.
Faluja Halfan alisema, hatua hiyo imesaidia wanafunzi kupata nafasi nzuri ya kuhudhuria masomo kwa wakati tofauti na siku za nyuma ambapo wakati mwingine walichelewa vipindi kutokana na umbali wa eneo walilokuwa wanaishi hadi kufika shuleni.
Sixtus Nuru mbali na kuishukuru Tfs kutokana na mchango huo alisema,kukamilika kwa bweni hilo kutapunguza utoro na matukio ya wizi yaliyokuwa yanafanywa na baadhi ya wanafunzi watukutu wasiopenda kusoma na wenye tabia mbaya.
Alisema,wakati mwingine baadhi ya wanafunzi walilazimika kuacha shule kutokana na mazingira mabaya hasa sehemu za malazi na hivyo kurudi nyumbani kutokana na sehemu ya malazi kutokuwa rafiki,lakini kwa sasa hakuna mwanafunzi atakaye acha shule kwani mazingira ni mazuri na rafiki kwa ajili ya kujisomea.
Kwa upande wake meneja wa shamba la Wino Lucas Manyonyi alisema, kwa kipindi cha miaka mitano imeweza kutoa msaada wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa baadhi ya shule za msingi na sekondari,ofisi za serikali za kijiji, nyumba za ibada na mkakati wao ni kuendelea kufanya hivyo kadri bajeti itakavyoruhusu.
Alisema, kwa kutambua na kuthamini michango ya jamii katika kulinda na kutunza mazingira,wakala kupitia shamba la miti Wino umeendelea kushirikiana na jamii kwa kusaidia mambo mbalimbali ikiwemo kutoa miche ya miti,mbegu za miti pamoja na viriba kwa shule za msingi na sekondari na vikundi vya wakulima wa miti.